Wakenya sita wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakitaka serikali izuiwe kutumia fedha za umma kufadhili mechi ya kirafiki kati ya Bayern Munich ya Ujerumani na Ajax ya Uholanzi inayotarajiwa kufanyika Januari 5, 2027, katika Uwanja wa Raila Odinga International Stadium.
Katika ombi lao la Jumatatu, Novemba 2, 2026, waombaji wanaitaka mahakama kutoa amri za muda kuzuia serikali kutenga, kutoa au kutumia fedha za umma kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Waombaji hao pia wanataka serikali kuweka wazi mikataba ya udhamini, majina ya kampuni zinazofadhili tukio hilo na kiasi cha fedha kinachotolewa na kila mdhamini.
Aidha, wanataka ufafanuzi kuhusu gharama za kuwaleta timu hizo, ikiwemo malipo ya ushiriki, usafiri, malazi, ulinzi, bima na maandalizi mengine.
Katika nyaraka za kesi hiyo, wanataja ripoti zinazoonyesha kuwa maandalizi ya mechi hiyo yanaweza kugharimu takriban KSh724.6 milioni (Euro milioni 5), ingawa wanasema kiasi hicho bado hakijathibitishwa rasmi.
Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo, Elijah Mwangi, kusema kuwa serikali haitatumia fedha za umma kufadhili mechi hiyo, akidai kuwa tayari wamepata mdhamini kutoka sekta binafsi.
Rais William Ruto ndiye aliyetangaza awali kuwa Bayern Munich na Ajax zitakutana nchini Kenya katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027.
Kwa mujibu wa Mwangi, mechi hiyo itashirikisha timu za wakubwa za klabu hizo mbili, akipuuza madai kwamba zitakuwa timu za vijana, akiba au wachezaji wa zamani.
Kesi hiyo sasa inaibua maswali kuhusu gharama halisi za kuandaa mechi hiyo na kiwango cha uwazi katika matumizi ya fedha zinazohusiana na tukio hilo.
Chanzo: Tuko.co.ke