Home
*Yaomba wananchi wote wawe watulivu
*Jaji Kipenka, DCI Manumba wazungumza
*Wanasheria waponda utendaji ofisi ya DPP
Na Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kuwaachia washitakiwa wa kesi ya mauaji ya wafanyabiashara iliyomhusisha Bw. Abdallah Zombe na wenzake wanane, Serikali imesema haijaridhishwa na uamuzi huo, hivyo imeanza mchakato wa kukata rufaa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mashitaka, Bi. Mary Lyimo, alieleza ;
"Tunaanza mchakato wa kukata rufaa kwa kutoa taarifa ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania ambayo ndiyo ya juu kabisa na ya mwisho yenye kutoa msimamo sahihi wa kisheria."
Kufuatia hatua hiyo, Bi. Lyimo aliwaomba wananchi kuwa watulivu wakati taratibu hizo za kisheria zikiendelea na watafahamishwa maendeleo yake.
Wakati Serikali ikijipanga kukata rufaa, wanasheria nchini wametafsiri uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu wa kuwaachia washitakiwa hao kama msiba kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hivyo imeshauri kutokurupuka kukata rufaa kufuata shinikizo lililopo sasa kutoka kwa wananchi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, Dar es Salaam jana, wanasheria waliobobea katika taaluma hiyo, walisema katika historia ya nchi hii haijawahi kutokea ofisi ya DPP ikashindwa kesi vibaya kama ilivyotokea kwa hii ya Bw. Zombe na wenzake.
Akizungumza na gazeti hili mwanasheria aliyebobea kwenye masuala ya ushahidi , Profesa Abdallah Safari, alisema;
"
Kwa kesi kama hii DPP alitakiwa kuwa makini, kama aliona ushahidi aliopelekewa na DCI ( Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai) haujitoshelezi angemrudishia na siyo kusukumwa na matakwa ya watu."
Alisema waliohusika kufanya upelelezi wa kesi hiyo ni Polisi ambao wapo chini ya DCI, hivyo kwa mazingira ya kawaida ni vigumu askari kuwapeleleza wenzao na kuja na ushahidi mzito wa kuwatia hatiani.
"Hii inaleta mkanganyiko ni kwa nini Polisi hawakuwatafuta waliowaua wafanyabiashara hao na kuwafikisha
mahakamani?"Alihoji Prof. Safari na kuongeza kuwa kabla ya kesi kufikishwa mahakamani ni lazima DPP ajiridhishe kuwa kuna kesi inatakiwa kufunguliwa na pili awe na uhakika na ushahidi alionao kuwa utampatia ushindi mahakamani.
Alifafanua kuwa yeye aliwahi kuwa wakili wa Serikali Kanda ya Mbeya na kuna wakati alikuwa akipelekewa vielelezo vya kesi zikiwemo za mauaji zinazotakiwa kufunguliwa na alipoona hakuna ushahidi wa kutosha, alirejesha majalada kwa wapelelezi.
Pia alibainisha kuwa inawezekana kwenye kesi hiyo ushahidi ulikuwa unajitosheleza kuwatia washitakiwa hatiani, lakini ukawa umepwaya kutokana na jinsi ulivyowasilishwa na mawakili wa Serikali.
"Matokeo yake washitakiwa wameachiwa na watu hawana imani na vyombo vya dola," alisema na kuongeza kuwa hiyo imeleta picha mbaya kwa umma.
"Raia watiifu wameuawa mikononi mwa polisi, tena kwa kupigwa risasi na fedha zao zikachukuliwa...halafu ofisi ya DPP inashindwa kuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani!"Alisema kwa mshangao.
Kutokana na hali hiyo,
Prof. Safari alisema kilichotokea kwenye ofisi ya DPP ni msiba. Alisema kama ofisi hiyo ina mpango wa kukata rufaa, isifanye hivyo kwa shinikizo lililopo badala yake
itulie na kuwatafuta
mawakili wanaojitegemea (anataja majina) ili
waweze kusaidia ukataji rufaa.
"
Inawezekana kuna makosa yametendeka katika nyanja mbili, wakati wa uwasilishaji ushahidi au katika upelelezi uliofanywa na ofisi ya DCI, watulie, ikibidi wasisite kupata msaada wa watu
wengine nje ya ofisi ya DPP," alisema Prof Safari.
Akizungumzia watu hao kufia mikononi mwa Polisi, alisema hiyo ni kashfa nzito kwani hata wakati wa mkoloni haikuwahi kutokea.
"Polisi ndiyo wenye siri kubwa, watu wanashindwa kuwa na imani nao kwasababu wamefia mikononi mwao," alisema.
Alipoulizwa kama hatua ya kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao kulikuwa na shinikizo la kisiasa, Prof. Safari alikiri kuwa hilo linawezekana kwani Serikali ilitaka kuwadhihirishia wananchi kuwa inaweza kuchukua hatua, hasa baada ya kuandamwa na kashfa kadhaa.
Kwa upande wake, DCI, Bw. Robert Manumba, alipoulizwa ana maoni gani kuhusu madai yanayotolewa kuwa ushahidi uliokusanywa na polisi ulikuwa mwepesi ndiyo maana washitakiwa waliachiwa, alisema hakuwa na jibu.
"Sina maoni yoyote siwezi kusema ushahidi ulikuwa mzito au mwepesi," alisema kisha kukata simu.
Kwa upande wake wake, Jaji Kipenka Mussa, ambaye aliongoza Tume iliyoundwa na Rais Jakaya kikwete kuchunguza utata wa mauaji hayo na kubaini kuwa waliouawa hawakuwa majambazi, alipoulizwa ana maoni gani kuhusu hukumu hiyo, alijibu; " No comment!"
Gazeti hili lilipozidi kumdodosa hasa kuhusu umma alivyopokea hukumu hiyo, alijibu;
"Sisi haturuhusiwi kutoa comments (maoni), No comments! I am not going to give any comments! (akimaanisha sina cha kuzungumza, sitasema chochote), au unataka nikufanyie ujeuri wa kukukatia simu?," alihoji Jaji huyo.
Kwa upande wake wakili wa kujitegemea Bw. Tindu Lissu, alisema, wapelelezi wa polisi wanapaswa kubebeshwa lawama kwa kupeleka ushahidi hafifu mahakamani.
Alidai kuwa kwa jinsi ambavyo polisi wamekuwa wakihusika katika baadhi ya natukio ya uhalifu, utendaji mbovu, rushwa na uozo mwingine, kuna uwezekano mkubwa kuwa upelelezi haukufanyika vizuri.
"Ninachokwambia hapa ni possibility (uwezekano), kwa kuangalia hali halisi, sio fact (usahihi) maana ingebidi tutoe ushahidi lakini katika hili ushahidi wa polisi ulikuwa wa namna gani?
Unategemea polisi wanaofanya maovu wachunguze maovu? Ili mtu ahukumiwe kufungwa au kunyongwa lazima utolewe ushahidi usiokuwa na mashaka yoyote ya msingi," alisema Bw. Lissu.
Aliongeza kusema kuwa wasiwasi uliooneshwa na watu baada ya hukumu ya kusomwa unaonesha ni kiasi wananchi hawana imani na vyombo vya utoaji haki.
"Watu wanajua kinachofanyika katika vyombo vya dola, kuanzia kwa Jeshi la Polisi, Mahakama na kwingineko ambako haki inatolewa kwa kuangalia misingi ya wenye pesa na wasiokuwa na pesa," alisema Bw. Lissu.
Pia alishangazwa na waendesha mashitaka kushindwa kuwafungulia washtakiwa hao makosa madogo mpaka makubwa ili hata kama hawakushiriki moja kwa moja katika mauaji bado wangeweza kupatikana na hatia sehemu nyingine.
"Mwendesha mashitaka mzuri anapaswa kumshitaki mtu kuanzia makosa madogo mpaka makubwa. Kwa mfano kuna ushahidi ulitolewa kuwa Zombe alikwenda Kituo cha Polisi kuvuruga ushahidi, kwa nini hawakumshtaki kwa kosa la kuvuruga haki isitendeke?" Alihoji.
Akitoa maoni yake kuhusu uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu, Mwenyekiti wa TPP-Maendeleo, Bw. Peter Mziray, alisema unaweza kumharibia Rais Kikwete na kumfanya apoteze imani ambayo wananchi waliyokuwa nayo kwake tangu washitakiwa hao walipofikishwa mahakamani.
Mbali na athari hiyo, alisema sheria zina udhaifu mkubwa na kuwafanya majaji washindwe kutenda haki. "Kama sheria inasema aliyeua hayupo, basi ni mbovu haitufai!" Alisema.
Alisema majaji wanafuata sheria kuliko namna ya kutoa haki. Alisema hawapaswi tu kuangalia nini sheria inasema, bali wanatakiwa kutoa uamuzi wao kwa kuangalia mazingira na namna ya kutenda haki.
Bw. Mziray alisema kuwa Mahakama imeelezwa katika Katiba kuwa ni chombo cha kutoa haki, lakini haki hiyo haitendeke kutokana na majaji na wanasheria kujikita kwenye sheria zaidi.
Juzi Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Salum Massati aliwaachia huru washtakiwa waaliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabishara wanne wa madini, kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Dar es Salaam baada ya kujiridhisha kuwa hawakuhusika katika tukio hilo.
Waliochiwa huru ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Zombe, ASP Christopher Bageni, ACP Ahmed Makelle, WP 4593 PC Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula, PC Michael Sonza, Koplo Ebeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Festus Gwabisabi.
Taarifa hii imetayarishwa na Reuben Kagaruiki, Edmund Mihale, Tumaini Makene na Peter Masangwa.