HATIMA ya Mkuu wa zamani wa Upelelezi mkoani Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake tisa ya kurudi kazini ipo mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) baada ya mkrugenzi huyo kukamilisha mchakato wa rufani.
Zombe na wenzake Jumatatu walishinda kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mhaenge, mkoni Morogoro na dereva teksi mmoja mkazi wa Manzese, jijini Dar es salaam iliyokuwa ikiendeshwa katika Mahakama Kuu chini ya Jaji Salum Massati.
Akizungumza katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Msemaji Msaidizi wa jeshi hilo, Suzan Kaganda alisema hati ya watu hao itategemeana sana na serikali upande wa jamhuri kukata rufaa ama la.
"Kwasasa hivi hatuwezi kusema kama watarudi kazini ama la kwa sababu, kwanza hatujapata ile hukumu rasmi mbali ya kusoma katika vyombo vya habari. Labda baada ya siku saba kuanzia leo tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusema kitu," alisema Kaganda na kuongeza:
"Kusema kama watarudi kazini ama vipi itategemea kama kweli serikali itakata rufaa ama vipi. Kama serikali itakuwa imekata rufaa hatutaweza kusema chochote kwa sababu kesi itakuwa imerudi mahakamani."
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Sheria ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amelilaumu jesho hilo kwa kushindwa kufanya upelelezi wa kutosha katika kesi hiyo.
Alisema Jeshi la Polisi ama lilizembea au lilifanya makusudi kuficha ushahidi wa kumtia hatia Zombe na wenzake.
"Ili mtu aweze kushitakiwa ni lazima kuwepo na ushahidi usio na mashaka kuthibitisha kosa lake. Lakini ushahidi uliopelekwa Mahakama Kuu na jeshi ulikuwa haujitoshelezi.
Ukweli ni kwamba, Watanzania hatuna jeshi la polisi linalofanya kazi kwa maadili. Mimi tangu nianze kazi ya uwakili sijawahi kushindwa kesi na waendesha mashitaka wa polisi. Kwanza hawajui kazi na wamesomea sheria kwa miezi sita tu. Ndiyo maana hata upelelezi walioufanya kwenye kesi ya Zombe ulikuwa ni wa kibabaishaji," alisema Lissu na kuongeza:
"Hata ukiangalia, Zombe alikuwa ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo waliofanya upelelezi ni hao hao vijana wake, unadhani wangeweza kumchoma(kumkandamiza)?"
Naye Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amesema serikali haikutakiwa kukata rufaa kupinga hukumu ya Zombe na wenzake tisa badala yake ingebadili mashitaka na kuwakamata tena watuhumiwa hao mara baada ya kuachiwa huru.
Akizungumza na Mwananchi jana alisema serikali serikali haikupaswa kushindwa katika kesi hiyo kwa kuwa ilikuwa na kila kitu.
"Mahakama ndio imeshamuachia huru Zombe na wenzake ingawa Watanzania waliamini kuwa watuhumiwa hao wangeswekwa jela, ila serikali imesababisha hali hiyo, kwani ilikuwa na uwezo wa kubadilisha mashitaka na kuwakamata tena akina Zombe," alisema Mtikila na kuongeza:
"Hivi karibuni tumeona katika kesi inayomkabili Liyumba (Amatus), aliachiwa huru, lakini muda huo huo hati ya mashitaka ikabadilishwa na akakamatwa tena, hivyo kitendo cha serikali kusema kuwa itakata rufaa hawa watu wanaweza kukimbia."
Mtikila alisema hukumu hiyo imetokana na jaji huyo kutumia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kusisitiza kuwa katika kesi yoyote kama ushahidi utatolewa kinyume, hukumu inaweza kuwa tofauti na kosa lenyewe.
Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki Binadamu (LHRC) kwa upande wake kimeunga mkono msimamo wa Jamhuri wa kutokuridhishwa moja kwa moja na hukumu hiyo na sababu zilizotolewa na Jaji Masatti za kuwaachia huru washtakiwa wote katika kesi hiyo.
Akizungumza na Mwananchi juzi Fulgence Massawe alisema LHRC imeipokea hukumu hiyo kwa mkanganyiko mkubwa, kwani kilichotokea ni vigumu kukubalikwa kwa jamii na wanasheria.
Hata hivyo, Massawe alisema hatua ya Jaji Massati kuwaachia huru washtakiwa hao haina maana kuwa hawakuhusika katika mauaji hayo, isipokuwa kwa kosa waliloshtakiwa nalo.
"Hatuwezi kukubaliana moja kwa moja na Jaji Massati kuwa washtakiwa wote wale hawana hatia", alisema wakili Massawe na kuongeza:
"Kuua si lazima wewe uwe 'ume-shoot' umempiga risasi. Kuna kushiriki kosa maana kuna washtakiwa wengine walikiri kuwepo kwenye tukio na hawakuwahi kutoa taarifa za tukio hilo. Katika sheria tunasema acha haki itendeke hata kama anga zitadondoka," alisema wakili Massawe.
Tayari serikali imeanza mchakato rasmi wa kukata rufaa kupinga hukumu ya akina Zombe rasmi jana.
Akizungumza na Mwananchi jana, Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo alisema tayari wamekwishawasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu tangu juzi.
"Tayari tumekwishawasilisha 'notes' (taarifa) ya kukata rufaa tangu jana (juzi)ambayo ndio mwanzo wa mchakato wa rufaa," alisema Mwipopo.
Wakili Mwipopo alisema waliwasilisha taarifa hiyo ya kukata rufaa juzi kwa Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuipeleka Mahakama ya Rufaa na kwamba, kwa sasa wanachosubiri ni nakala ya hukumu hiyo pamoja na mwenendo wa kesi hiyo.
"Kisheria tulitakiwa kuwasilisha Notes ya nia ya kukata rufaa ndani ya siku 14 tangu siku ya kutolewa hukumu, lakini sisi tumewasilisha baada ya siku moja tu," alisema Mwipopo na kuongeza,
"Kwa hiyo kwa sasa tunasubiri kupata 'copy' ya 'judgement' (nakala ya hukumu), na 'proceedings' (mwenendo wa kesi) ili tuweze kuwasilisha sababu zetu za kukata rufaa," alifafanua Wakili Mwipopo.
Katika hatua nyingine, mmoja wa mawakili wa serikali waliokuwa wakiendesha kesi hiyo walisema hatua ya washtakiwa wote katika kesi hiyo kuachiwa huru kwa maelezo kuwa hakuna ushahidi wa kutosheleza kuwatia hatia, ni kama vile wamefungwa goli la mkono wa Mungu.
Katika hukumu yake aliyoitoa Jumatatu juma hili, Jaji Massati ambaye ni wa Mahakama ya Rufaa, aliwaachia huru washtakiwa wote tisa katika kesi hiyo iliyokuwa ikimhusisha aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Dar es Salaam(RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP) Abdallah Zombe kwa maelezo kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Zombe na wenzake walikuwa wakishtakiwa kwa tuhuma za kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara wa madini Sabinu Chigumbi, Ephram Chigumbi na Mathias Lunkombe toka Mahenge, pamoja na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam Juma Ndugu.
Mbali na Zombe wakishtakiwa wengine waliokuwa wamebakia katika kesi hiyo ambao pia waliachiwa huru juma baada ya watatu kuachiwa katika hatua ya awali na mmoja, Koplo Rashid Lema kufariki dunia April 3 mwaka huu, ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (OC-CID) Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni, na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa kituo cha Polisi Urafiki Mrakibu Msaidizi wa Polis (ASP) Ahmed Makelle.
Wengine ni WP 4593 PC Jane Andrew, CPL Emmanuel Mabula, PC Michael Sonza, CPL Ebeneth Saro, C/CPL Rajab Bakari na D/CPL Festus Gwabisabi.
Washtakiwa hao walikuwa wanatuhumiwa kwamba, waliwaua wafanyabiashara hao Januari 14, mwaka 2006 katika Msitu wa Pande ulioko Mbezi Luis nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa kuwapiga risasi.