Mahakama yaamuru Prof Mahalu na mwenzake wana kesi ya kujibu
Na Tausi Ally
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Afisa utawala wa ubalozi huo, Grace Martin, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wamepatikana na kesi ya kujibu.
Balozi huyo na afisa wake pia wanatuhumiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh2 bilioni.
Uamuzi huo ulitangazwa jana asubuhi na Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Sivangilwa Mwangesi, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani ili itolewe uamuazi.
Akitoa uamuzi huo, hakimu Mwangesi alisema amepitia maelezo ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na vielelezo tisa vilivyotolewa ili kuthibitisha makosa dhidi ya watuhumiwa hao na kushawishika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, watuhumiwa wanatakiwa kuanza kujitetea Mei 4, mwaka huu na kuwataka washtakiwa hao kupitia mawakili wao kueleza njia watakayotumia katika kujitetea.
Hali kadhalika, wataje idadi ya mashahidi wao katika kesi hiyo.
Akijibu hoja hiyo, wakili Bob Makani anayemtetea Balozi Mahalu alidai kuwa mteja wake atajitetea yeye mwenyewe kwa njia ya kiapo na kwamba mashahidi wataitwa katika utetezi utakavyokuwa unaendelea.
Kwa upande wake, wakili Malima anayemtetea Martin, alidai mteja wake ataanza kujitetea yeye mwenyewe kwa njia ya kiapo na kwamba wataita mashahidi watatu.
Mara ya mwisho, ushahidi kuhusu kesi hiyo, ulichukuliwa katika ukumbi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam ambako mahakama ilikuwa inamsikiliza shahidi mmoja akiwa Roma Italia.
Hatua hiyo ilikuja baada ya shahidi huyo Marko Papi ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Italia kushindwa kuja Dar es Salaam, kutoa ushahidi wake.
Hatua hiyo iliulazimisha upande wa mashtaka, kuchukua ushahidi wake kwa njia ya video.
Hata hivyo kabla ya kuanza kuchukuliwa kwa ushahidi huo, kulitokea malumbano kati ya upande wa utetezi na ule wa mashitaka, malumbano yaliyodumu kwa dakika 45.
Mmoja wa mawakili wa upande wa utetezi Mabere Marando, alipinga kupokelewa kwa ushahidi huo kutoka Italia kwa madai kuwa ni kinyume na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Shahidi huyo aliyewahi kutoa ushahidi wake Machi 14, mwaka jana alidai kuwa yeye alipokea mkataba wa mauzo wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia wa Euro 1, 032, 913.80 ambao unatambulika kisheria nchini humo.
Alidai sheria ya Italia inaruhusu mkataba mmoja wa wazi kama ule mauzo aliosaini yeye.
Baada ya kusikiliza hoja zote, hakimu Mwangesi aliutaka upande wa utetezi kufunga ushahidi kwa kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuleta mashahidi.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Septembe 23 mwaka 2002 huko Roma Italia, Mahalu na Grace Martin wakiwa waajiriwa wa Serikali ya ya Tanzania, walisaini hati ya malipo yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58.
Inadaiwa kuwa maelezo hayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.