Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa kwa wanachama, wafuasi wake na kwa wananchi wote kuwa Septemba 08, 2025 Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam itaanza kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao wa Taifa, Tundu Lissu.
Awali kupitia mfumo wa mashauri ya Mahakama, kesi hii ilionesha kupangiwa Septemba 12, 2025 lakini kwa mujibu wa Mahakama (summons) alioupokea Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, usikilizwaji wa kesi sasa rasmi utaanza Septemba 08, 2025.
"CHADEMA tunaona wazi kuwa kesi hii haina sura ya kawaida ya jinai bali ni mwendelezo w mipango ya kisiasa ya Serikali ya Rais Samia Suluhu dhidi ya Mwenyekiti Lissu na chama chetu kwa lengo la kukandamiza haki za msingi za wananchi" - Taarifa ya CHADEMA
CHADEMA kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Brenda Rupia ametoa wito kwa wananchi wote, wananchama, wanaharakati, vijana, wanawake, wazee, pamoja na jamii ya kimataifa kufuatilia kwa karibu na kufika Mahakamani kwa wingi siku hiyo.