Habari zenu Wakuu!
Nina jambo ambalo linanitesa kwa muda sasa baada ya kupita kwenye mahusiano ya nyuma ambayo niliyaona kuwa ni kila kitu kwangu. Wakati ule tulikuwa vijana, damu inachemka, na tuliamini kuwa upendo wetu ulikuwa wa kipekee kuliko wa mtu mwingine yeyote hapa duniani.
Katika hali ya kupeana ahadi za kutokuachana, tulifikia hatua mbaya ya kufanya kiapo cha damu, tulifanya uamuzi ambao leo unaninyima usingizi; tulichanja chale kwenye kidole gumba cha kila mmoja wetu, tukalamba na kugusanisha damu ya kila mmoja, na kuapa kuwa "Yeyote atakayevunja ahadi hii na kuolewa au kuoa mtu mwingine, basi maisha yake asije akapata furaha na heri maishani." Wakati huo, tulicheka na kuona ni kielelezo cha juu kabisa cha uaminifu.
Baada ya muda, mambo yalibadilika na tukashindwa kuendelea. Kila mmoja alichukua hamsini zake, na nilidhani hayo yamebaki kuwa historia na utoto ule ulishapita. Lakini sasa, miaka kadhaa mbele, niko kwenye mchakato wa kuanza maisha mapya na mtu mwingine, ndipo vitu vya ajabu vimeanza kunitokea.
Kila hatua ninayopiga kuelekea kuhalalisha mahusiano yangu ya sasa, nakumbana na vikwazo visivyoelezeka, kuanzia ndoto za kutisha hadi hali ya hofu inayoniandama kila kukicha.
Najisikia mwenye hatia na wakati mwingine nahisi kama kile kiapo ndicho kinachonishika na kunizuia kusonga mbele.
Sijui hata nifanye nini kujinasua kwenye huu mtego niliouingia kwa hiari yangu mwenyewe.