Afya ya Ballali bado
Waandishi Wetu
Januari 2, 2008
Yaelezwa anakula kwa mashine
HALI ya afya ya Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Ballali, inazidi kutatanisha na kuna habari kwamba hakuwa anaweza kula chakula katika hali ya kawaida, na haijafahamika mara moja kama hali hiyo kwa sasa imetengamaa ama la.
Vyanzo mbalimbali vya habari kutoka Marekani na Dar es Salaam, vinasema kwamba hali yake ya imekuwa ya kutatanisha kabla na baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa.
Habari zinasema kwamba Ballali (65) pamoja na mambo mengine, alifanyiwa upasuaji mkubwa katika moja ya hospitali kubwa nchini Marekani iliyopo Jimbo la Massachusetts, jiji la Boston, lakini hakuna taarifa rasmi za hasa alifanyiwa upasuaji gani.
Akizungumza na RAIA MWEMA kwa simu kutoka Washington D.C, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Ombeni Sifue, alisema jana Jumanne kwamba Balali bado yuko hospitali Boston, lakini hakuwa anafahamu ni hospitali gani aliyolazwa na wala hana taarifa za ugonjwa unaomsumbua.
"Ninavyojua yuko hospitalini Boston na hali yake inaendelea vizuri japo kwa taratibu sana. Pamoja na kuwa taarifa za ugonjwa wa mtu ni za siri, sifahamu anasumbuliwa na nini na kwa kuwa sijawahi kwenda kumuona sifahamu alifanyiwa upasuaji wa aina gani," alisema Balozi Sifue.
Imeelezwa kwamba Ballali ambaye hadi sasa kujiuzulu kwake hakujathibitishwa na Serikali, anaendelea na matibabu lakini hakuna dalili ya lini hasa atapata nafuu na kuweza kuendelea na kazi, hali ambayo ilimlazimu kuchukua jukumu la kujiuzulu nafasi yake.
Hata hivyo, habari zisizo rasmi zinaeleza kwamba Ballali alitoka hospitali na kwa sasa yuko katika moja ya hoteli jijini Boston huku akiendelea kupata uangalizi wa madaktari wa hospitali hiyo.
Imeelezwa kuwa amekuwa akila chakula kwa msaada wa vifaa maalumu, lakini Balozi Sifue alisema: "Sina taarifa za undani wa matibabu anayoyapata, lakini ninavyojua anapata nafuu pole pole."
Hadi sasa Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusiana na undani wa ugonjwa wa Ballali, pamoja na kuthibitisha kwamba anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo ya Boston.
Vyanzo visivyo rasmi vinaeleza kwamba Ballali anaweza kuwa amefanyiwa upasuaji wa kichwa katika harakati za kupunguza ama kuondoa tatizo linalomsumbua kwa muda mrefu sasa na pia kwamba amefanyiwa uchunguzi wa damu.
"Upo uwezekano wa kuwa amefanyiwa upasuaji wa kichwa kutokana na matatizo yanayomsibu lakini pia wagonjwa wa aina yake wanaweza kufanyiwa upasuaji wa tumbo na kubadilishwa bandama ili kumpa afueni," kinaeleza chanzo chetu ndani ya Serikali.
Imeelezwa kwamba serikali inaendelea kugharamia matibabu ya Ballali kwa kuwa bado anatambulika kisheria kuwa Gavana wa BoT, hadi hapo Rais Jakaya Kikwete atakapokubali kujizulu kwake na kuteua mtu kushika nafasi hiyo.
Imethibitishwa kwamba Rais Kikwete hakuwahi kumtembelea Ballali alipokuwa ziarani nchini Marekani, pamoja na kuwa amekuwa akifuatilia afya yake kutumia maofisa na watendaji waandamizi wa serikali.
Rais Kikwete binafsi anaelezwa kuguswa na yanayomsibu Ballali, huku akitafakari ni nani hasa anayeweza kuchukua nafasi yake na jinsi ya kurudisha heshima ya BoT ambayo imezidi kuporomoka siku hadi siku.
Kikwete amekwisha kuziba baadhi ya nafasi nyeti zilizokuwa zikishikiliwa na watu aliowarithi kutoka kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, ikiwamo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, na hivyo kuwapo uwezekano wa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya BoT na asasi nyinginezo kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ballali ambaye anaelezwa kuingia BoT, Juni 1998, aliongezewa muda na Mkapa mwaka 2003, muda ambao awali ulielezwa kuwa ni wa miaka miwili tu, lakini kisheria muda huo unapaswa kumalizika Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha miaka miwili ya utawala wake, Jumatano iliyopita, Rais Kikwete, alikiri kufahamu kuhusu kuugua kwa Ballali, lakini alikanusha uvumi kwamba Gavana Ballali amekimbia tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa BoT.
Inaelezwa kwamba siku Kikwete alipokutana na waandishi wa habari Ikulu, ndiyo siku ambayo barua inayoelezwa kuandikwa na Ballali ilipotumwa na kupokewa Ikulu lakini hakuna taarifa rasmi za kuthibitisha hilo ambazo zimetolewa hadi sasa.
Ballali aliondoka nchini kimya kimya na hakuna mtiririko mzuri wa taarifa za hali yake ya afya pamoja na baadhi ya watu kusema kwamba ni lazima taarifa hizo zitolewe kwa mujibu wa taratibu za ‘kiserikali.'
Nakala ya barua ambayo inaaminika kuwa ni yake kwenda kwa Rais, na ambayo Raia Mwema iliichapisha, Gavana Ballali anasema ya kuwa kutokana na "sababu za kiafya" hatoweza kuendelea na wadhifa huo na hivyo anaomba idhini ya kupumzika.
Zimekuwapo taarifa hata hivyo, kuwa baadhi ya maofisa na viongozi waandamizi wa serikalini wamekwenda kumjulia hali Gavana Ballali, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman, ambao wote wanaelezwa kuguswa na kuumwa kwake.
Mmoja wa waandamizi hao anaelezwa kumtembelea Ballali Jumapili ya Desemba 2, 2007 ambako alielezwa kuonyesha mshangao wa dhahiri wa jinsi "muujiza wa Mwenyezi Mungu" ulivyomsaidia Ballali kupambana na maradhi yanayomsumbua.
Mbali ya kuguswa na "muujiza wa Mwenyezi Mungu" mazungumzo hayo yaligusia uwezekano wa Ballali kujiuzulu ili kutoa nafasi ya kuteuliwa kwa mrithi wake, lakini pia suala nyeti la kurejea ama kutorejea kwake lilikuwa sehemu ya mazungumzo hayo.
Ballali ana nyumba yake binafsi eneo la Bethesda, Maryland Kaskazini Magharibi mwa Washington, D.C. lakini habari zinaeleza kwamba tokea alazwe hospitali hajaonekana katika nyumba hiyo.
Kuugua kwake na hatimaye kutangazwa kuwa amejiuzulu, kumekuwa na maswali mengi bila majibu na wakati wote taarifa zake zimekuwa zikitolewa nusu nusu bila kuwa na undani wa kutosha na hadi sasa Wizara ya Fedha, ambayo ndio mwajiri wake haijawahi kutoa taarifa ya wazi kuhusiana na hali yake wala kuhusu kujiuzulu kwake.
Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, aliwaambia waandishi wa habari kwamba hajapokea barua ya kujiuzulu kwa Ballali, kwa maelezo kwamba taratibu zinamtaka kuwasilisha barua kwake na si kwa Rais kama ilivyoripotiwa. Hata hivyo, Meghji alikiri kufahamu kuugua kwake.
RAIA Mwema limeelezwa kwamba Gavana Ballali alilazimika kuwasiliana na wasaidizi wake walioko Dar es Salaam, ambao waliandika barua hiyo kwa maelekezo yake na baadaye ilipelekwa Ikulu kwa faksi kabla ya barua halisi kupelekwa kwa njia ya kawaida na kupokewa.
Agosti mwaka huu Rais Kikwete alifanya uteuzi wa Manaibu Gavana watatu kama sheria mpya ilivyotaka. Walioteuliwa ni; Profesa Benno Ndullu, Lila Mkila na Juma Reli. Uteuzi wa Profesa Ndullu ndio uliogusa zaidi hisia za wengi kutokana na kutajwa kama mmoja wa wanaotajwa kuwa na uwezo wa kumrithi Ballali.
Profesa Ndullu anatajwa kuwa na historia ya utendaji mzuri tokea akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anaelezwa kushiriki katika mchakato wa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kipindi ambacho Kikwete alikuwa Waziri wa Fedha.
Anaelezwa kwamba aliondoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1989 kwenda Nairobi, Kenya kuwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa African Economic Research Consortium kabla ya kujiunga na Benki ya Dunia akifanya kazi Dar es Salaam na baadaye makao makuu, Washington D.C kabla ya uteuzi wa kuwa Naibu Gavana.
Wengine wanaotajwa ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Blandina Nyoni, ambaye aliwahi kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali; Dk. Natu Mwamba wa BoT; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, ambaye alitokea BoT; Naibu Katibu Mkuu, Mipango Joyce Mapunjo, ambaye alitokea Hazina na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei.
BoT imekua ikisakamwa kutokana na tuhuma mbalimbali na hivi sasa inasubiriwa ripoti ya wakaguzi wa kimataifa kutoka Kampuni ya Ernst&Young iliyokabidhiwa kazi hiyo na Serikali kupitia ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG).
Taarifa kuhusu ripoti hiyo zimetolewa zikiwa zinatatanisha baada ya Waziri Meghji kusema itatolewa wiki hii baada ya kupitiwa na CAG, huku CAG mwenyewe, Ludovick Utoh akisema kwamba ndio kwanza ameipokea Jumapili iliyopita na kwamba atamkabidhi Rais Januari, 2008.
Kuna habari kwamba pamoja na tuhuma za ufisadi ndani ya BoT kuwagusa baadhi ya watendaji serikalini na baadhi ya watu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwakumbatia watuhumiwa hao.
Katika tukio la hivi karibuni, imeelezwa kwamba mmoja wa watu wanaotajwa sana kuhusika na upotevu wa fedha za BoT, alialikwa "kuchoma nyama" na kiongozi mmoja wa juu serikalini wakati wa Sikukuu ya Krismasi, jambo ambalo limezua maswali mengi kuliko majibu.