*Watoa siku 30 wahusika kujisalimisha Luganga
*Waomba serikali iwaletee mchanga wa kaburi
Na Francis Godwin, Mufindi
WAKATI mwili wa aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Daud Ballali umezikwa Washington, Marekani Ijumaa iliyopita, baadhi ya wazee wa kabila la Wahehe wamekuja juu na kutoa siku 30 kwa yeyote aliyehusika kwa njia moja ama nyingine na kifo hicho, kujisalimisha kijijini Luganga, Mufindi mkoani Iringa alikozaliwa gavana huyo.
Wazee hao kutoka kijiji cha Luganga na Mtwango, wameiomba serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya kifo hicho na kufanya kila linalowezekana kuresha mwili huo nchini, ikishindikana ilete mchanga wa kaburi hilo ili wafanye mazishi ya kimila.
Wakizungumza na Majira jana kwa niaba ya wenzao, Mzee Samweli Kalinga (76) na Yohanes Kalinga (85), walisema wataamini kuwa mtoto wao amekufa baada ya kupata ufafanuzi wa kina kupitia kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu kifo hicho.
Walisema wao kama wazee wa siku nyingi wa kijiji cha Luganga na Mtwango, wanashindwa kuamini kuwa mtoto wao amekufa, wataamini jambo hilo baada ya kuona maiti au picha yake akiwa amekufa.
Mzee Samweli alisema taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari hazitoshelezi kuamini kuwa ni kweli mtoto wao kipenzi, Dkt. Ballali amekufa hivyo ameiomba serikali kuunda tume haraka kuchunguza mazingira ya kifo cha gavana huyo wa zamani.
Alisema moja ya sababu inayowafanya waendelee kuamini kuwa Dkt. Ballali bado mzima ni mazingira ya sasa ya nyumbani kwao kijijini Luganga na nyumbani kwa baba zake wadogo eneo la Ziroziro, Mtwango.
" Nimeishi Mtwango tangu utoto wangu sijawahi hata siku moja kuona nyumba yenye msiba haina waombolezaji", alisema Mzee Samweli
Alisema kwa mujibu wa taratibu za kihehe, msiba unapotokea huombolezwa siku tatu mfululizo ama zaidi ambapo kwa muda huo, majirani hukusanyika nyumbani kwa wafiwa kuwafariji.
Alisema inawezekana ni kweli, Dkt. Ballali amekufa kama ilivyothibitishwa na baadhi ya ndugu zake lakini wao kama wazee wakihehe, wanasubiri serikali itoe taarifa rasmi ya kina ikiambatana na uchunguzi kamili wa kifo hicho.
"Tunaomba kuelezwa ugonjwa uliosababishia kifo cha mtoto wetu na jitihada zilizofanywa na serikali kuokoa maisha yake... Tunashindwa kuelewa serikali inapotoa pole wakati iliwahi kusema Ballali hajulikani alipo", alisema Mzee Samweli.
Kwa upande wake Mzee Yohanes alisema wanafanya mpango kukutana na ndugu wa marehemu kufanya tambiko la aina yake la kifo hicho na kuomba dua maalum kulaani kifo hicho kama kimetokana na 'mkono wa mtu'.
Mzee huyo, alisema wametoa siku 30 kwa watu waliohusika kwa njia moja ama nyingine na kifo hicho kujisalimisha kijijini hapo, vinginevyo watu hao hawatadumu kwenye nyadhifa zao.
Alisema iwapo kifo hicho kimetokana na mapenzi ya Mungu basi wanamshukuru kwa kutimiza matakwa yake na kama ni kwa mipango ya shetani na wanadamu, basi itashughulikiwa ipasavyo.
Pamoja na mwili huo kuzikwa Marekani, wazee hao wameiomba serikali kufanya kila linalowezekana kuurejesha nchini, ikishindikana waletewe mchanga wa kaburi lake ili wafanye mazishi kwa mujibu wa mila za kihehe, Luganga alikozikwa baba yake mzazi Mzee Timoth Ballali aliyefariki dunia Aprili 3 mwaka 2000.
" Hata kama imeshindika kuleta mwili wake basi wasafirishe mchanga wa kaburi tuje tufanye mazishi kwenye makaburi ya Luganga alipolala baba yake mzazi. Kumzika Marekani ni sawa na kumtenga na familia yake", alisema Mzee Yohana.
http://majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=6779