Date::10/29/2008
Mbunge Mkono aitishia kuikataa ripoti ya kamati ya Kikwete
Na Daniel Mjema,Dodoma
Mwananchi
MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ameikataa ripoti ya kamati iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kupitia sekta ya madini nchini, chini ya Jaji Mark Bomani hadi atakapopata maelezo ya kutosha kuhusu mgodi wa Buhemba na kampuni za Meremeta na Tangold.
Nilidhani Ripoti ya kamati hii ya rais ingetupa tatizo hasa la Buhemba, lakini nayo inakuja na maelezo kuwa haikupata maelezo ya kutosha kutoka serikalini
sasa kama Tume ya Rais inashindwa kupata ripoti, mimi Mbunge itakuwaje, alihoji.
Mkono alisema fedha zilizoibwa Buhemba ni nyingi kuliko za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na kusisitiza kuwa hataunga mkono hoja hiyo hadi apatiwe majibu kuwa kampuni ya Tangold inamilikiwa na nani kama iko nchini Mauritius .
Kuna wenzetu hapa wakiwa Bungeni walipiga kelele sana, lakini wakiwa ndani (Tume ya Rais) wanakaa kimya wamepewa nini hawa
au tuko hapa kuleta usanii," alihoji Mkono na kushangaa kutoona machahari ya Zitto Kabwe katika suala la Buhemba.
Mkono, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema ni lazima kampuni za Tangold na Meremeta zichunguzwe huku akionyesha kushangazwa na namna mgodi wa Buhemba ulivyoachwa mashimo matupu huku dhahabu ikiwa imechukuliwa.
Awali katika mchango wake wa asubuhi, Kabwe alihoji namna mwekezaji wa mgodi huo alivyowekeza Dola 20 milioni za Kimarekani (zaidi ya Sh22 bilioni za Tanzania), lakini akaiuza kwa mwekezaji mwingine kwa dola 300 milioni za Kimarekani.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka(CCM) alishangaa kutofanyiwa kazi kwa ripoti ya Jenerali Mboma ambayo ilichunguza mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na kampuni ya Tanzanite One.
Akionyesha kukerwa na uundwaji wa kamati na tume kila mara, alisema binafsi asingeshauri kuundwa kwa kamati au tume nyingine kabla ya kuzifanyia kazi taarifa za kamati zilizotangulia kama ile ya Jenerali Mboma, ambayo imewekwa kabatini.
Alishangaa serikali kupokea mrabaha wa dola 1.4 milioni za Kimarekani kwa miaka 10 kutoka kampuni ya Tanzanite One akisema huo ni wizi kwa sababu kampuni hiyo imekuwa ikipata mapato makubwa ukilinganisha na kile ilicholipa serikalini.
Katika hatua nyingine, Bunge limemshauri Rais Jakaya Kikwete kufanya maamuzi mazito kwa maslahi ya nchi, ikiwemo kusitisha utiaji saini wa mikataba mipya ya madini hadi sheria mpya itakapopitishwa na chombo hicho.
Mbali na suala hilo, Bunge limependekeza kufanyika kwa uchunguzi maalumu wa jinsi serikali ilivyouza hisa zake zake za migodi mitatu na mahali fedha zilipotumika na taarifa ziwasilishwe Bungeni.
Hisa ambazo serikali iliziuza ni zile zilizokuwa katika migodi ya Kiwira, Bulyanhulu na Mwadui na pia serikali imeshauriwa kusitisha uuzaji wa hisa zake katika migodi mingine ikiwamo ya Buckreef Gold Mine, Kiwira Coal Mine na Williams Diamonds Ltd.
Kadhalika Bunge limependekeza kuwa asilimia 70 ya fedha zote zinazotokana na mauzo ya madini nje ya nchi zirejeshwe nchini kwa matumizi ya ndani badala ya makampuni kuzitumia nje ya nchi.
Mapendekezo hayo yamo katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu taarifa ya Kamati ya Rais ya kuishauri serikali kuhusu usimamizi wa sekta ya madini iliyowasilishwa Bungeni jana.
Taarifa hiyo ya kamati, ambayo inaonekana kuwa msumari wa moto kwa wawekezaji wa kigeni na kuwarejeshea Watanzania matumaini, iliwasilishwa bungeni na mwenyekiti wake, William Shelukindo.
Kutokana na Tume ya Jaji Mark Bomani kubaini mapungufu na udanganyifu mkubwa katika sekta ya madini, Bunge limependekeza kufutwa kwa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa wawekezaji hao.
Sheria ya kodi ya zuio (Withholding Tax) inataka malipo yote yanayofanywa na kampuni za madini kwa kampuni za ndani na za kigeni zinazotoa huduma za menejimenti na utawala, zikatwe kodi hiyo.
Hata hivyo Shelukindo alisema Tume ya Jaji Bomani imegundua kuwa kampuni za ndani zinatakiwa kukatwa asilimia 5 wakati za kigeni ni asilimia 15, lakini baadhi ya kampuni zenye mikataba zinakata asilimia 3.
Kamati yangu inakubaliana na kamati ya rais kuwa huu ni ukiukwaji wa utawala wa sheria, Mikataba ya kibiashara inajidhihirisha kuwa na nguvu zaidi ya sheria ya nchi
hii haikubaliki kabisa, alisema Shelukindo.
Shelukindo alisema kwa kuwa suala la mikataba ya madini limeonekana kugubikwa na matatizo makubwa ya usiri, utata na vipengele vinavyokiuka sheria za nchi na hivyo sheria ya madini ya mwaka 1998 iandikwe upya.
Ili kuondoka na na wawekezaji uchwara, kamati hiyo imependekeza kuwa kwa kuanzia, ili kampuni iweze kuwa na mkataba na serikali, ni lazima uwekezaji wake uanzie dola 600,000 za Kimarekani.
Kamati hiyo imeonyesha kushangazwa na hatua ya serikali kurudisha kipengele kimoja cha kodi kinachompa mwekezaji unafuu wa ziada wa asilimia 15 kwenye gharama za uendelezaji migodi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kifungu hicho kinachotoa unafuu huo wa kuikamua nchi kilifutwa mwaka 2001, lakini mwaka uliofuata kifungu hicho kikarejeshwa tena kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2002.
Maelezo ambayo kamati ya Rais iliyapata ni kwamba serikali ilishinikiza kukirejesha tena kifungu hicho. Haya hayafurahishi kuyasikia na tunaungana na mapendekezo ya tume kuwa kifutwe mara moja, alisisitiza Shelukindo.
Kuhusu mikataba mipya ya madini, kamati hiyo imependekeza mikataba hiyo iwe wazi kwa wananchi na ipatikane katika ofisi za mikoa, wilaya na halmashauri ambazo zina migodi hiyo.
Pia kamati hiyo ipendekeza kupunguzwa kwa uhai wa mikataba ya madini kutoka miaka 25 ili itoe fursa ya kupitiwa kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kuongeza ufanisi kulingana na mabadiliko yatakayojitokeza katika uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla.
Awali kabla ya kuwasilisha kwa taarifa hiyo ya kamati, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwasilisha muhtasari wa taarifa ya Tume ya Jaji Bomani ikianisha mapungufu kibao katika sheria na sera za madini.
Ngeleja alisema kulingana na ripoti hiyo,sekta ya madini inakabiliwa na changamoto, ikiwemo mchango wake mdogo katika pato la taifa, madini kuendelea kuuzwa yakiwa ghafi na uchimbaji duni wa wachimbaji wadogo na kupendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria na sera hizo.
Waziri Ngeleja alisema kutokana na kutolewa kwa taarifa hiyo, tayari kikosi kazi kimeundwa ili kuangalia namna bora ya kutekeleza mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo ya Tume ya Rais.
Awali wabunge walipendekeza uchimbaji wa madini ya vito yakiwemo madini adimu ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee ufanywe kwa asilimia 100 na Watanzania na sio wawekezaji kutoka nje.
Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki,Anna Kilango Malecela(CCM) alienda mbali na kuitaka Serikali ivunje mkataba na kampuni ya Tanzanite One ya Mererani hata kabla ya muda wa kisheria wa mkataba kumalizika.
Akichangia ripoti ya kamati ya Rais ya kuishauri serikali kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini Bungeni jana, Kilango wachimbaji wadogo wanao uwezo wa kuchimba madini ya vito kwa kutumia mitambo midogo.
Ingawa Kilango hakuitaja Tanzanite kwa jina Bungeni lakini katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana alisema kampuni aliyokuwa akiilenga ni Tanzanite ambayo zamani ikifahamika kama Afgem.
Nimefanya utafiti wangu na kugundua kuwa leseni yao (Tanzanite One) inamalizika mwaka 2012 mimi naona huko ni mbali ukilinganisha na hasara tutakayopata tusitishe leseni yao sasaalisema Kilango.
Kilango alisema uchimbaji wa madini ya vito kwa kutumia mitambo mikubwa sio endelevu na kuonya kuwa kiasi cha madini kinachochimbwa na kuhifadhi nje ya nchi ni kikubwa huku Tanzania ikiachiwa mashimo.
Mbunge huyo ambaye ni mmoja wa Wabunge Machachari alisema ni vyema Serikali ikasitisha mkataba huo sasa na kulipa fidia ambayo inaweza kuwa ndogo ukilinganisha na madini mengi yanayochimbwa.
Alionya kwa vile kampuni hiyo sasa inafahamu kuwa uchimbaji wa madini ya Vito utafanywa na Watanzania kwa asilimia 100 wanaweza kuchimba kwa nguvu ili kufikia 2012 madini ya Tanzanite yawe yamekwisha.
Siku zote kutoa maamuzi magumu ndio kuendelea na huu ni uamuzi mgumu lakini tumwambie Rais kuwa sisi Wabunge tunamuunga mkono na tuko tayari kuchangia fidia kusitisha mkataba huualisema.
Mbunge wa Busega,Dk. Raphael Chegeni (CCM) alishangaa Tanzania kuwa nchi ombaomba wakati imebarikiwa rasilimali kubwa ya madini akitaka serikali ianye maamuzi magumu kwa maslahi ya Watanzania.
kule kwetu kuna dhahabu hebu niambieni ni wapi katika nchi mgeni anamiliki mgodi kwa asilimia 100,ni lazima tubadilike na suala la umiliki wa migodi ya madini litazamwe upyaalisema Dk. Chegeni.
Dk. Chegeni aliunga mkono mapendekezo ya kamati ya Jaji Bomani ya kutaka wawekezaji wa kigeni wanaokuja nchini wakijifanya wawekezaji na kuvuna rasilimali za Tanzania na kuondoka kama hazina mwenyewe.
wawekezaji brief case(wa mifukoni) hatuwataki wanaokuja wawe na mtaji ili kuwaengua wawekezaji uchwara
yaani wanafanya Tanzania kama shamba la Bibi wanakuja wanachukua wanaondokaalisema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Kabwe Zitto,(CHADEMA) alihoji inakuwaje madini yanachangia asilimia 40 ya mapato ya mauzo nje ya nchi lakini hapa nchini yanachangia asilimia 3 tu ya pato la Taifa.
Kabwe alitaka kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ichunguze madai ya kufukiwa kwa wachimbaji wadogo katika mgodi wa Bulyahulu akisema kamati ya Rais chini ya Jaji Bomani ilipokea malalamiko hayo.
Akiwasilisha Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,William Shelukindo alipendekeza utaratibu wa kusafirisha madini ghafi nje ya nchi kwa ajili ya usafishaji na ukataji ufutwe.
suala hili limezua mjadala sana kiasi cha kamati yangu kuhoji kama ni kweli Taifa letu halina uwezo wa kufanya shughuli hizi hapa nchinialisema Shelukindo ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.
Shelukindo aliliomba Bunge kuiagiza serikali kupeleka Bungeni muswada wa sheria ndani ya mwaka mmoja ambao utazuia usafirishaji wa madini ya vito ghafi, yakiwamo madini ya Tanzanite ambayo yanachimbwa Tanzania pekee.
Aliitaka serikali kulipa uzito suala hilo ili kujenga ajira nchini na hivyo kubakiza kiasi cha fedha ambazo zinapatikana kwa shughuli za madini hapa nchini kwani pia itasaidia kujua kiasi hali cha madini kinachosafirishwa ikiwa ni pamoja na kuyaongezea thamani.
Alisema kamati yake pia imeguswa na suala la upendeleo wa ajira katika makampuni ya kigeni ya madini kati ya Watanzania na wageni na kuitaka serikali izipitie upya sheria za kazi na pale anapohitajika kuajiriwa mfanyakazi wa kigeni basi iwe ni kwa utaalamu ambao haupo nchini.