TUMETIWA moyo na kauli ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka aliyoitoa bungeni mjini Dodoma mwezi uliopita, kwamba anakusudia kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho Aprili mwaka huu, kulitaka Bunge lipitishe azimio la kurudishwa kwa nyumba za Serikali zilizouzwa na Serikali ya Awamu ya Tatu katika mazingira ya kutatanisha.
Mbunge huyo ambaye amejipambanua kwelikweli kama mmoja wa wabunge ambao wanapambana na vitendo vya ufisadi nchini, alisema hatua hiyo ya Serikali kuuza nyumba za watumishi wake haikubaliki siyo tu kwa sababu siyo endelevu, bali pia ina kila dalili za ukiukwaji wa misingi ya uadilifu na utawala bora.
Tunampongeza mbunge huyo kwa kauli yake hiyo ambayo hapana shaka itakuwa imewaliwaza wananchi wengi ambao walipinga kwa nguvu zote pasipo mafanikio kitendo cha Serikali kuuza nyumba hizo. Itakumbukwa kwamba uuzwaji wa nyumba hizo ulipingwa vikali katika kila kona ya nchi yetu siyo tu kwa kuwa ziliuzwa kwa bei ya kutupwa, bali pia kwa zoezi hilo zima kutofanyika kwa uwazi na kutofuatwa kwa taratibu zilizowekwa kuhusu uuzwaji wa mali za serikali.
Siyo siri kwamba uuzwaji wa nyumba hizo ulionekana dhahiri kufanywa kibabe. Katika macho ya wananchi wengi waliopaza sauti zao kulaani kitendo hicho ambacho bila shaka kilipata baraka za Baraza la Mawaziri, kitendo hicho kilikuwa ni unyanganyi na ukwapuaji wa wazi wa mali ya umma kinachoweza kufananishwa na uhaini. Tunasema hivyo kwa sababu viongozi wa serikali ambao ndiyo waliokuwa na dhima ya kulinda mali hiyo ya umma ndiyo waliokaa na kula njama za kujigawia nyumba hizo, ambazo zilijengwa sehemu maalumu katika miji yote nchini ili kuwawezesha viongozi wa serikali kuishi karibu na sehemu zao za kazi kwa lengo la kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi zao.
Safu hii haitoshi kuorodhesha madudu yote yaliyotokana na kitendo hicho ambacho kimepewa jina la ufisadi. Hata hivyo, yafaa kusema tu hapa kwamba uuzwaji huo ulifanyika katika staili ya chukua chako mapema na pengine ndiyo sababu nyumba hizo hazikuuzwa kwa viongozi wa serikali pekee kama ilivyotarajiwa, bali pia kwa baadhi ya viongozi wa chama tawala, ndugu, jamaa na marafiki wa viongozi hao.
Hoja ya Mbunge Sendeka ambayo inaungwa mkono na umma wa Watanzania ni kwamba uuzwaji huo haukuwa halali, bali ulikuwa ni wizi. Wananchi wangevumilia wizi huo iwapo angalao ungekuwa umeidhinishwa na Bunge ambalo mamlaka yake yanatokana na wananchi wenyewe. Kitendo cha wateule wachache serikalini kukaa na kula njama za kujigawia nyumba za umma hakika hakielezeki hata kidogo kama ambavyo hakikubaliki kwa namna yoyote ile.
Njama zilizofanywa na viongozi hao ni kukarabati nyumba hizo kwa mamilioni ya fedha za serikali kabla ya kugawiana kama njugu na baadaye kuziuza kwa watu binafsi kwa mabilioni ya fedha. Hata nyumba zilizokuwa nyeti, kwa maana ya kuwa karibu na vituo vya polisi au majengo ya vyombo vya ulinzi na usalama ziliuzwa kiholela. Ebu fikiria hili: Nyumba za mawaziri; makatibu wakuu; wakuu wa mikoa na wilaya; maafisa usalama; makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya; mahakimu na majaji; na wakuu wengine muhimu ziliuzwa.
Matokeo ya hatua hiyo ni kwamba viongozi walioteuliwa na serikali ya Awamu ya Nne walijikuta hawana nyumba, hivyo kulazimika kuponda mamilioni ya kodi za wananchi katika mahoteli ya kifahari. Kwa mfano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha aliripotiwa kuishi katika hoteli moja jijini Dar es Salaam na kulipiwa Sh60 milioni kwa mwezi.
Hayo ndiyo matokeo ya uuzwaji wa nyumba za Serikali. Ni matumaini yetu kwamba hoja binafsi ya Mbunge Sendeka itaungwa mkono na Bunge. Ni matumaini yetu pia kwamba Watanzania kwa umoja wao watazidi kupaza sauti kupinga uuzwaji wa nyumba hizo hadi zitakaporudishwa serikalini.
Mwananchi