Morogoro vitunguu bora vinapatikana kwenye maduka mengi sanaaa ya pembejeo mjini Morogoro. Hizo ni mbegu bora kwa vile ni officially certified. Mbegu hizi zinadosari kubwa mbili, kwanza huwa ghari sana kwa mtu anaetaka kulima eneo kubwa kibiashara mfano ekari moja na kwenda juu. Kwa hiyo gharama ya mbegu huwa kubwa ingawa kwa kweli huwa mara nyingi ni mbegu halisi!
Tatizo la pili ni jinsi hali ya hewa ilivyoharibika Kitaifa kwamba kila biashara sasa kuna kitu-FEKI! Unanunua mbegu kwa bei mbaya inamhuri unaosomeka kabisa kuwa mbegu hiyo imekuwa packed January na wewe unainunua April unaisia inagoma kuota kabisa! Unahofia labda nimesia vibaya, unanunua nyingine tena matokeo yale yale haioti!
Mfano iliwahi kunitokea mimi mwaka mmoja nilinunua mbegu ya Pilipili Hoho za kampuni maarufu ya Holand! Muhuri ulionyesha ni mbegu mpya kabisa ya hoho lakini haikuota!! Nimekuwa nikipata mbegu ya uhakika toka kampuni ya Mkulima Seeds hizo ndiyo zilikuwa zikiota, lakini tena tatizo likaja Mbegu za Mkulima seeds nazo ni mchanganyinko, hoho zingine zilikuwa ndefu sana na nyeupe (matunda)!
Pia kuna Nyanya aina ya Tanya naijua vema tabia yake na tunda linavyokuwa, niliwahi kununua mbegu aina hiyo ya nyanya zinazozalishwa na East Africa Seed company zilipoanza kuiva ilikuwa ni uchafu tu hata wateja walisusia kununua! Ilikuwa ni mchanganyiko wa mbegu usioeleweka! Kwa ukweli usiamini mbegu yoyote eti mradi iko kwenye Kopo au pact yenye lebo nzuri ni wizi wizi tu! Mkakati wangu kwa hili ni kuzalisha mbegu mwenyewe watu hawaaminiki!
Sehemu ya pili ya kupata mbegu Morogoro ni mbegu zinazozalishwa na wakulima. Morogoro kuna eneo maarufu kwa kilimo cha vitunguu linaitwa Lumuma, wilaya ya Kilosa huko kunawazalishaji wengi sana wa mbegu za vitunguu waliopata mafunzo rasmi ya uzalishaji bora wa mbegu za vitunguu.
Mbegu za vitunguu toka kwa wakulima huuzwa kwa kupimwa kwa ujazo wa lita. Kutegemea mwaka lita huanzia sh 15,000/- hadi 30,000/- mwaka 2010 ilifikia bei ya lita moja 50,000/-! Mbegu huvunwa mwezi wa 10 huu ni muda mzuri kununua baada ya hapo bei hupanda juu. Mkulima anaetaka kulima eneo kubwa mbegu hii ndiyo inamfaa maana ni nafuu kuliko za kwenye makopo.
Tatizo kubwa la mbegu za wakulima nalo ni ulaghai! Kwa kuitazama mbegu huwezi jua kama ni mbegu aina unayoitaka, wengi huwa wanadanganya ukijapanda baadae unabaki kulia kuwa umetapeliwa! Inabidi pia uwe unajua kuzipima kama zinaota au la, wenyeji wananjia mbalimbali wengine wanatumia maji wengine moto! Kitaalamu ni budi kuotesha sample kwanza kisha angalia uotaji wake kisha ukiridhika nunua kwa wingi kutoka kwa mkulima husika.
Tatizo lingine kwenye mbegu za wakulima za vitunguu ni hili: kwa kawaida vitunguu vinatabia msimu wa kwanza havitakiwi vitoe mabomba ya maua bali vitoe vitunguu tu, msimu wa pili unapopandikiza kitunguu-mama ndiyo hutakiwa kitoe bomba, maua na hatimae mbegu. Sasa kwa wakulima laghai inapotokea kitunguu kikatoa mbegu isivyotarajiwa ule msimu wa kwanza huzivuna hizo mbegu na kuziuza!
Ukinunua mbegu kama hizo matokeo yake ni kujikuta vitunguu asilimia kubwa shambani vimetoa mabomba ya maua! Na hii ni hasara kwani vitunguu vyako hukosa ubora sokoni yaani ni msiba kwako!
Ili kuepuka hili unatakiwa uwahi kwa mkulima mzalishaji wa mbegu ukaone vitunguu vyake vikiwa bado shambani mwezi mmoja au miwili kabla hajavuna ili ujiridhishe kwamba ni aina halisi ya vitunguu unayotaka ili akivuna ununue kitu halisi.
Vinginevyo tumia wakulima waaminifu ambao akikuambia ni red ni red kweli akisema khaki ni khaki kweli! Msimu wa mwisho nilimwamini kijana mmoja alikuwa akileta mbegu toka Singida, kumbe kule Singida alikuwa akizoa hizo mbegu nilizoeleza hapo juu, wanazoa zoa mashambani tu, matokeo yake nikaanza kuona vinajitokeza vitunguu vyeupe na vyekundu, baadae shamba zima lilichanua utadhani nimelima vitunguu vya mbegu!!
Kuwa mwangalifu utakapokuwa unatafuta mbegu!
Niwie radhi jamani maelezo yangu marefu saa zingine namimi nae mweeee!