Kisa cha Dola 10 Zilizotupwa Mtoni jasho la mtu haliliwi

Kisa cha Dola 10 Zilizotupwa Mtoni jasho la mtu haliliwi

bless on

JF-Expert Member
Joined
May 22, 2026
Posts
1,213
Reaction score
2,938
Salamu sio lazima twende moja kwa moja kwenye kisa Cha kweli chenye hekima kubwa👇
Zamani kidogo, kulikuwa na mzee mmoja tajiri na mchapa kazi aliyekuwa anamiliki mali na biashara nyingi. Alikuwa na mtoto mmoja wa kiume aliyekuwa mvivu sana, asiyetaka kufanya kazi yoyote na aliyekuwa anasubiri tu mzee afe ili arithi mali zote.

Kila mara kijana alimfuata baba yake na kumwambia: "Mzee, lini utanikabidhi urithi wangu wa mali?"

Siku moja, baba yake alimwangalia na kumwambia: "Mwanangu, kama unataka kurithi mali zangu zote, nenda mtaani ukatafute Dola 10 (ama Shilingi Elfu 25 za Kitanzania) kwa jasho lako mwenyewe, uje unipe. Ukifanya hivyo, mali zote zitakuwa zako."

Yule kijana aliondoka akicheka. Badala ya kwenda kufanya kazi, alikwenda kwa mama yake mzazi, akamlilia shida na kumwambia: "Mama, nipe Dola 10 nimpelekee mzee ili anikabidhi urithi." Mama yake kwa huruma alimpa ile Dola 10.

Kijana alirudi kwa baba yake na kumkabidhi ile pesa. Yule mzee bila kusema neno lolote, alichukua ile Dola 10, akaenda nayo dirishani na kuitupa katikati ya mto uliokuwa unapita nyuma ya nyumba yao!

Kijana alitazama tu akitabasamu, hakujali wala kushtuka. Baba yake alimwangalia na kumwambia: "Nenda tena mtaani, pesa hii hukuitolea jasho!"

Kijana aliondoka tena. Safari hii alikwenda kwa dada yake, akamuomba Dola 10 nyingine. Dada yake akampa. Alipompelekea baba yake, mzee alichukua tena ile Dola 10 na kuitupa tena mtoni! Kijana alishika tu mabega akacheka, maana kwake haikuwa kitu. Baba akamwambia tena: "Hii nayo hukuitolea jasho!"

Safari hii, mama yake na dada yake walikataa kabisa kumpa pesa nyingine na kumwambia: "Nenda ukafanye kazi!"

Yule kijana akiwa hana ujanja, alilazimika kuingia mtaani. Alikwenda kwenye eneo la ujenzi (site), akabeba mifuko mizito ya simenti, akapasua mawe, na kuvuja jasho jingi chini ya juakali kwa siku tatu mfululizo. Mikono yake ilijaa madoa ya damu na miguu ilimuma vibaya sana. Mwisho wa siku ya tatu, alilipwa Dola 10 za jasho lake!

Alirudi nyumbani akiwa amechoka mahututi, akaingia ndani na kumkabidhi baba yake ile Dola 10 akiwa anatetemeka kwa uchovu.

Yule mzee alichukua ile Dola 10, akasimama na kuelekea tena dirishani ili kuitupa mtoni!

Safari hii, kabla mzee hajaitupa, yule kijana aliruka kwa kasi kama simba,😁 akamshika baba yake mkono kwa nguvu zote, akapiga magoti na kupiga kelele kwa uchungu na machozi:

"Baba Hapana! Tafadhali usitupe hiyo pesa! Unajua jinsi nilivyovuja jasho siku tatu mfululizo? Mikono yangu inavuja damu na mgongo unaniuma vibaya sana kisa hii Dola 10! Usitupe jasho langu mtoni!"

Yule mzee alitabasamu kwa furaha kubwa, akamwekea mwanaye mkono kichwani na kumwambia:

"Mwanangu, sasa hivi upo tayari kurithi mali zangu zote! Nilipotupa zile pesa za kwanza mtoni, hukujali kwa sababu huzikutolea jasho. Lakini hii uliyoipigania kwa jasho lako, uko tayari kuipigania kwa maisha yako. Sasa unajua thamani ya pesa na mali zangu zitakuwa salama mikononi mwako!"

Angalizo👇

Pesa Ya Bure Haina Nidhamu Wala Heshima Mtu anayepata pesa za dezo, za wizi, au za kurithi bila kuzitolea jasho, huwa hazithamini. Ndio maana watu wengi wanaoshinda bahati nasibu au kurithi mali nyingi bila kufanya kazi, wanazitawanya na kurudi kwenye umaskini ndani ya muda mfupi.

Jasho Lako Ndio Mwalimu Wa Nidhamu Ya Fedha Pesa unayoipata kwa maumivu ya mgongo wako, kwa kuamka asubuhi na mapema na kuvuja jasho mtaani, ndiyo inayokufundisha nidhamu ya matumizi. Huwezi kuitumia pesa ya jasho lako kwenye ujinga kwa sababu unajua gharama ya kuipata.

Gharama Ya Mafanikio Ni Pamba Na Jasho Usitamani maisha au mali za mtu mwingine kabla hujawa tayari kubeba maumivu na juhudi alizopitia kuzipata. Hakuna njia ya mkato ya mafanikio ya kudumu lazima ukubali kuingia ulingoni na kuvuja jasho lako mwenyewe.

Acha kulalamika au kusubiri msaada wa bure mtaani. Pambania Dola 10 yako ya jasho leo hiyo ndiyo itakayokupa nidhamu, heshima, na uwezo wa kulinda mamilioni ya kesho!
 
Back
Top Bottom