Inaendelea sehemu ya sita.
Tulikuwa tumeshafika kwenye mlango wa kuingia kwa mganga. Unajua familia nyingi za usukumani zinakuwa na wigo au tuseme uzio ambao mara nyingi unakuwa wa miti fulani inaitwa minyaa au "manara" kwa kisukuma, lakini pia wigo mwingine ulikuwa wa mkonge "katani" kwa kisukuma. Na kwenye wigo huu huwa kuna sehemu ya kutokea ambao ndio kama geti la kuingilia. Sasa tulikuwa tumesimama kwenye hiyo sehemu ya kuingilia, lakini tulivyopita tu kuingia Sasa kwa mganga tukawa hatuoni chochote. Nyumba tulizokuwa tunaziona za mganga pindi tukiwa nje ya ule wigo tukawa hatuzioni, ni miti na vichaka tu ndio tukawa tunaona.
"Oooh! nini hiki" alisema Vumilia kwa sauti iliyoashiria kufadhaika na hali ile.
Nilimuangalia kwa sababu nilikosa sababu hata nimjibu nini, kwangu kila kitu kilionekana kama mazingaombwe. Baadaye aliniambia unajua mganga huyu ameweka madawa ya kuzindika eneo lake kwa hiyo sitaweza kupita, hadi nivue nguvu za kichawi nije kawaida ndio nitapita.
"Utavuaje?" Nilimuuliza
"Inabidi tuende kwa bibi"
Tulianza kutembea kwenda kwa bibi yake ambapo ilikuwa ni palepale kijijini kwetu. Sio muda mrefu tulikuwa tumeshafika. Aliingia ndani kwenye moja ya nyumba za pale kwao, akakaa kidogo halafu akarejea.
Safari hii alikuwa amevaa nguo za kawaida . Alikuwa amejifunga kitenge kiunoni na kitenge kingine amekizungusha kwa juu kifuani. Alinyoosha mkono na kunionyesha kopo, akaniambia nichote na kujipaka usoni. Nilichota kitu ambacho ni kama yalikuwa mafuta yakiwa yamechanganywa dawa, ambayo yalifanya kuwa kama mchanganyiko wa mafuta na unga unga. Yalikuwa ni mafuta yenye harufu kali ya kama kitu kilichooza lakini sikujali nilijipaka bila kujiuliza mara mbili. Aliniambia yalikuwa ni mafuta ya aina fulani ya mjusi ambaye kwa kiswahili sijui jina lake yamechanganywa na unga wa mizizi ya miti minne ambayo hakunitajia wala hakunambia matumizi yake.
"Inabidi tutembee haraka, nahisi tuko hatarini" aliongea huku uoga ukiwa dhahiri machoni mwake.
"kwa nini"
" Nahisi wanakutafuta kukuchukua na sasa wako njiani wanakuja, inabidi tufanye haraka tufike kwa mganga. Wakitukuta njiani kabla hatujafika utakuwa hatarini"
"Wamejuaje tumekuja huku" niliuliza nikionyesha mshangao kidogo.
"Wewe huyajui haya mambo, tafadhali tuwahi tuondoke"
Safari hii hatukutembea kama mwanzo isipokuwa tulikuwa tunakimbia ili tuwahi kufika. Na miongoni kati ya vitu vilivyonishangaza mwanzoni tulikuwa tunatumia muda kidogo sana kutembea umbali mrefu, lakini safari hii tulitumia muda mrefu. Haikuchukua muda mrefu toka tuanze ile safari, akaniambia wako nyuma yetu wanatufata. Wakitupata tu umekwisha. Niliogopa sana nikawa natamani hadi kupaa. Niliwaza pia vipi tukifika tena kwa mganga halafu tusipaone halafu huku nyuma tunafukuziwa.
It was probably the most terrifying moment in my life.
Muda sio mrefu nikaanza kusikia vishindo vya watu vinatufuata kwa nyuma. Wakati akili haijakaa sawa nikasikia kishindo kwa mbele yetu ni kama kitu fulani kilikuwa kimerushwa. Tokea pale tukawa tunapata ugumu sana wa kukimbia, miguu ilikuwa mizito sana au niseme ni kama kuna nguvu fulani unakuvuta kwa hiyo unapiga hatua kwa tabu sana. Tulijikongongoja hadi tulipovuka pale ambapo kile kitu kilikuwa kimedondokea. Tulipokivuka tu tukaanza kukimbia tena kwa kasi. Kufupisha story zoezi hili likawa endelevu ikawa kila tukivuka muda sio mrefu, kile kitu (ambacho kwa wakati huo bado sikukijua ni kitu gani) kinarushwa tena, tukivuka baada ya dakika chache kinarushwa tena. Lakini tukikivuka kasi yetu ya kukimbia inaongezeka, kikirushwa kasi inapungua inakuwa kama tunavutwa. Tulihangaika hivyo hadi tulipofika kwenye geti la kuingilia kwa mganga.
"rudini sasa watoto wangu mmewashindwa"
Ilikuwa ni sauti ya kiume ambaye nilikuja kumugundua ni mzee Nkelebe. Alikuwa akiwaamuru wale wachawi warudi walikotoka. Alitupokea na kutupeleka hadi kwenye mojawapo ya kijumba kilichopo pale kwake kilichojengwa kwa nyasi mwanzo mwisho.
Aliingia kwenye nyumba na kuja na viti vidogo aina ya vigoda viwili akatupatia na kutuamuru tukae.
"Unajua mwanzoni niliwaona mlivyokuja mkarudi. Wewe Vumilia ni mwenyeji hapa nilijua umekuja kwa nia njema Na lazima kuna shida hivyo nilijua lazima utarudi tu, hivyo nilikaa kukusubiri"
"Na huyu msabato umemtoa wapi, hadi akawa anakimbizana na wajanja usiku huu" aliendelea kusema huku akiniangalia Kwa unafiki fulani
Ni kama alikuwa ananikumbusha mwaka mmoja uliopita tu, nikiwa na brother mmoja mwinjilisti wa kanisani kwetu muuza vitabu vya dini ambapo nikiwa naye tuliwahi kumtembelea huyo mganga kumhubiri neno la Mungu. Nilikumbuka mwinjilisti yule aliyekuwa hamung'unyi maneno akimwambia mganga wewe unafanya kazi ya shetani utachomwa moto. Na sisi tunaofanya kazi ya Mungu tutaenda mbinguni. Sasa ilikuwaje mtoto wa Mungu anayesubiri mbingu, kwenda kutafuta msaada kwa wachomwa moto.
Ukistaajabu ya Musa, utayaona ya firauni.
"Tuachane na hayo baba huyu kijana anahitaji msaada" alisema Vumilia
"Sawa"
Mzee alisogeza maji kwenye karai dogo akaweka dawa fulani. Akamaliza akachukua kitu kama mkia wa mnyama wenye rangi nyeusi. Kama unaujua mkia wa ng'ombe kule chini huwa unakuwa kama una manyoya manyoya marefu, alichukua mkia wa hivyo sasa. Akamaliza akaanza kupiga manyanga huku akiimba nyimbo na kuongea ongea kama aliyepandwa na wazimu. Baada ya dakika kadhaa akanipa kakipande ka mti wa mnyaa na kuniambia nizungumze shida zangu bila kutoa sauti. Ni kama mtu anavyonuia kitu fulani.
Baada ya kumaliza zoezi lile alikichukua kile kipande akakiloweka kwenye yale maji. Akamaliza akakitoa kisha akaanza kukiangalia.
Akaanza kuniambia.
"Kijana una matatizo makubwa sana. Umefanya vizuri kuja hapa leo la sivyo leo ulikuwa mwisho wako. Kwanza ninaona watu wameandaa sherehe sehemu fulani kufurahia kukukaribisha huko kwenye makazi ya misukule"
"Na ninawaona hadi sasa wamekaa pale nje ya wigo wangu wanakusubiri utoke hapa"
Alisema na kuniangalia, nilikaa kimya sikuwa na la kuongea bado.
Alichukua kopo fulani akalisogeza kwenye mdomo wake, akaongea maneno fulani halafu akachukua dawa nyeusi na kunipaka usoni kisha akaniambia nitoke nje na kuangalia angani. Huku akinielekeza maneno fulani ya kutamka hadi mara tatu. Nilitoka nje huku nikiogopa nikafika nikatazama hewani na kutamka maneno aliyoniambia mara tatu. Yalikuwa maneno sio ya kiswahili wala kisukuma.
Ghafla kilijitokeza kitu cha ajabu angani, ambacho sikukitarajia. Ni kama ilitokea luninga iliyokuwa inaonyesha matukio mbali mbali. Kwa ufupi niliwaona wachawi kuanzia siku ile walivyonichukua wakanipeleka makaburini na kunichanja chale na kila kitu walichokifanya. Kilichonisikitisha zaidi niliwaona bibi yangu na mama yangu mdogo wakiwa na mwanamke mwingine ambaye naye alikuwa wa palepale kijijini. Bibi huyu alikuwa ni mmojawapo wa wake za babu yangu mzaa mama ambaye kwa wakati huo alikuwa marehemu na mama mdogo ni mtoto wa kuzaliwa na huyo bibi. Nilivyoona tu nilijua sababu ya yale yote ni nini.
Kulikuwa na mgogoro baina ya watoto wa mke wa kwanza wa babu yangu ambao ni mjomba wangu, mama mkubwa na mama yangu mzazi ambaye alikuwa ni kitinda mimba. Huyu bibi niliyemuona kwenye luninga ya mzee Nkelebe alikuwa ni mke wa pili kuolewa. Sababu ilikuwa ni mgogoro wa ardhi ambapo mke huyu alidai kuna sehemu ambayo mama yangu na mama mkubwa walichukua, ambayo ilinunuliwa yeye akiwa ndio ameolewa hivyo yeye ndiye haki nayo.
Kumbe nalogwa kisa mgogoro wa ardhi niliwaza!
Baada ya muda luninga ile ilikata matangazo nikarudi kwenye kijumba cha mganga. Kufika tu Vumilia alifungua mdomo wake na kuniambia.
"Nafikiri sasa umeanza kuniamini, mwanzoni nilipokuambia ndugu zako wanakutafuta labda hukunielewa"
Mzee Nkelebe alimtuliza Vumilia kisha akaanza kuniambia.
"Una matatizo mawili ambayo nimeyaona kwako yanayotakiwa kushughulikiwa. Tunaanza na tatizo la kwanza"
Mganga aliniangalia kisha akanambia nikunje suruali yangu. Aliliona kovu ambalo nililipata miaka mingi, siku ile nimeona wachawi nikiwa darasa la tatu. Aliniambia
"Kuna kitu uliwekewa kwenye mwili wako muda mrefu sana nimekiona unacho, tatizo lenu wafiadini hamtembeagi hadi mambo yawafike shingoni, ulitakiwa uwe umeshakiondoa muda mrefu sana" alisema mganga huku akiniangalia kwa umakini pale kwenye kovu.
"Labda nikuulize swali" alisema mganga akatulia kidogo kisha akaendelea
"hivi unadhani kwa nini siku ile unaona wachawi wakati ukiwa bado mdogo, kwa nini wewe peke yako ndio ulizisikia zile kelele za wachawi?. Na unadhani kwa nini ulipotoka nje ulifanikiwa kuwaona wachawi pasipo kutumia dawa yoyote, wakati kikawaida huwezi kuwaona wachawi bila Dawa?"
Aliniuliza lakini niliona dhahiri sikuwa na jibu kamili. Hivyo nikamwambia sijui chochote.
Akaniambia ulipokuwa mtoto ulikuwa na nguvu za asili na ukoo wenu una mizimu mikali sana. Hizo nguvu ndio zilikusaidia kuwaona na kusikia zile kelele, japo sasa hivi zimepungua na ni kawaida kupungua kadri unavyozidi kukua.
"Sasa wachawi hawakufurahishwa na wewe kuwaona, ilibidi wakufate baadae ulipokuwa umelala wakuchane mguu na kukuwekea dawa fulani iliyo kwenye kakipande kadogo ka mti"
"Kazi ya dawa hizo ni kukuzuia wewe ushindwe kusema chochote kila unaposhuhudia tukio la kichawi. Hebu niambie tokea ulivyoona tukio lile ulishawahi kumsimulia mtu kama ulitokewa na jambo kama lile"
"hapana" nilijbu kwa mshangao huku nikikumbuka jinsi moyo ulivyokuwa unakuwa mzito na kuogopa sana kila nilipotaka kumwambia mtu yeyote kuhusu tukio lile.
"Kumbe dawa zile zilikuwa zinafanya kazi" niliwaza
"Amini hata hili tukio la kuchanjwa usingeweza kumwambia yeyote. Na hautaweza kuja kumwambia yeyote kuhusu tukio la kishirikina utakalolishuhudia hadi siku unaingia kaburini, kama tusipoitoa hiyo dawa mwilini mwako" alisema mganga
"Hata baba yako najua usingemwambia, najua ungepata nia ya kumwambia lakini usingethubutu, hivyo watu wasingejua shida yako na usingepata msaada"
Baada ya kumaliza alichukua wembe na kunichana kidogo kwenye kovu.Alipaka dawa kisha akachomoa kipande cha mti kidogo kama vimisumari vile vidogo.
" Sasa uko huru kuongea. Tunaenda kwenye tatizo la pili".alisema kisha akaendelea
"Hili nadhani umejionea mwenyewe, wachawi tayari wana mamlaka juu ya mwili wako maana wameshamaliza maagano na mizimu ya kwenu, kwa tambiko lililofanyika makaburini. Kazi iliyobaki ni kukuchukua. Sasa ili tukurudishe kuna damu yako waliichukua wakati wanafanya tambiko inabidi tuirudishe kwanza" alitulia kidogo kisha akaendelea
"damu hiyo mwanzoni ilikuwa imefichwa kwenye dari la nyumba ya kwa bibi yako. Ila baada ya kujua umeshaanza kutembea kwa waganga kuna sehemu imepelekwa kufichwa pa siri zaidi ambayo mimi kwa uwezo wangu siwezi kuichukua huko. Inabidi nikupeleke kwa mganga ambaye naamini yeye anaweza kukusaidia. Ila ni mpaka nimtaarifu kwanza baba yako kwanza ajue kila kitu. Maana kuna vitu vitahitajika"
Nilikubali kwa sababu sikuwa na ujanja. Hata hivyo nilijua kama mama yangu angejua ndio angeleta kipingamizi lakini baba yangu hakuwa na shida, hakuwa mtu wa dini sana. Nilimshauri wasimshirikishe mama kwenye hilo, kwa sababu nilijua kwanza ni lazima angepinga kwenda kwa mganga. Pili sikutaka kumuona akiyajua matatizo yangu yangemfanya asononeke sana.
Mganga aliniambia nisiondoke pale kwake maana ndio ilikuwa sehemu salama kwangu. Hadi ile damu yangu irudishwe, lakini akamwambia Vumilia aondoke kesho asubuhi ila asipite kwenye njia ya kutokea kwa mganga wakati anatoka. Yaani apite sehemu pasipo na njia rasmi, mganga alihofia kuna mitego imeachwa ni mpaka aitegue kwanza.
Itaendelea