Kisa cha Kweli: Sitasahau nilivyopendwa na mchawi nikaishia kurogwa

Inaendelea sehemu ya tisa.

Nilikuwa nimelala usiku, nikiwa na amani kidogo kwa kufahamu angalau waliokuwa wananitafuta wamekwama. Kichwani mwangu nilikuwa na mambo matatu yaliyokuwa yananiumiza kichwa na kunifikirisha.

Jambo la kwanza nilijiuliza kuhusu kurudi shule kuendelea na masomo, hili lilikuwa la kawaida halikuniumiza kichwa sana.

Jambo la pili nilijiuliza kama na mimi ningehusika tena kwenye mkakati wa kwenda kuwamaliza hao wabaya wangu. Nisiwe mnafiki tokea nilivyofahamu waliyonifanyia niliwachukia sana, hivyo nilifurahi niliposikia wanaenda kuuawa na sikuwa na shaka nilikuwa nishajua mizizi ya mzee Masele ni mirefu. Hili liliniumiza akili kwa sababu sikupenda kuhusika kwenye hayo mambo tena nilikuwa nimeshayachoka...

Jambo la tatu ambalo ndio liliniumiza kichwa kuliko yote, ilikuwa ni ukweli kwamba sikuwa na uwezo wa kumkatalia Vumilia kuhusu jambo la kuwa kwenye mahusiano na yeye. Nisingeweza kwa sababu kuu mbili, kwanza yeye ndiye aliyenisanua mimi boya mmoja kwamba kuna wajanja wananitafuta kwenye kumi na nane hivyo niliona napaswa kulipa fadhila. Mbili nimeshuhudia mwenyewe kwa macho yangu Vumilia ni mchawi, hivyo kumkataa na kama kweli ananipenda ingekuwa hatari kwangu. Ilikuwa ni lazima niwe naye, niliona hakukuwa na uamuzi mwingine wa kuamua tofauti.

Asubuhi kulikucha na makucha yake, tukaamka tukawa tunaendelea na ratiba za kawaida. Nakumbuka nilifagia asubuhi uwanja baada ya kumaliza nikawa nimekaa pale, Baadaye mzee Masele aliniambia kwamba mchana saa nane jua kali tutaongozana kwenda kumalizia ile kazi. Sikupenda lakini nisingeweza kusema hapana ilikuwa ni mwendo wa ndio mzee.

Mchana muda wa saa sita aliniita ndani ya kijumba chake cha nyasi, nikaingia nikakaa. Alikuwa amewasha moto na kuna mizizi na magome ya miti akawa anayachoma, pembeni ya ule moto mkono wa kulia kulikuwa na mkuki na mkono wa kushoto kulikuwa na chungu kilichokuwa na maji. Akawa anaongea ongea mara azungushie lile eneo na dawa mara aongee kwenye chungu, mara atoke nje azungukie eneo lote la pale kwake, hakuwa na utulivu kabisa. Akamaliza alinivalisha shingoni kidude ambacho ni kipande cha mti kidogo kilichochongwa kwa ustadi mkubwa na kimefungwa kamba nzuri ambayo ndio niliitumia kuvaa kile ki mti. Ni miaka ya mbele sana ndio nilikuja kujua ile inaitwa hirizi, sikuwahi kukiona kitu kinachoitwa hirizi kabla japo ni kitu nilichokuwa nakisikia mara kwa mara watu wakikizungumzia.

Baadaye mida ya saa saba aliniambia twende tukamalizie kazi yetu. Tulianza kutembea kwa miguu kuelekea kijiji chetu tena. Njiani watu tulikuwa tunakutana nao lakini huwezi amini hakuna aliyekuwa anatuona. Sikuamini

This is a daylight witchcraft!

Ndio nilichowaza kichwani. Wakati wote mimi nilikuwa naamini uchawi hufanyikaga usiku tu , kumbe hadi mchana. Maajabu haya!

Tulitembea hadi tulipofika hapo alipokuwa anakaa bibi yangu, tukafika hadi kwenye njia ya kuelekea pale kwake. Yaani sehemu ambayo ndio kama geti la kuingilia. Tulivuka na tulitembea hadi katikati ya uwanja wa nyumba yake, alikuwepo lakini hakuweza kutuona kabisa. Mzee Masele aliniacha pale katikati ya uwanja halafu yeye akawa anazunguka maeneo yale. Nilimuona kama anaenda maeneo tofauti tofauti anachimbia dawa na kwenda eneo jingine. Alivyomaliza alikuja akachimba kishimo kidogo kwa kutumia kisu ambacho tulikuwa tumebeba akaweka dawa na kufukia. Alifanya mambo mengi sana ambayo mengine nayaacha kwa sababu ya muda..

Baada ya pale aliniambia "tuondoke sasa ili twende nikakufanyie dawa, Baadaye leo leo jioni utarudi hapa, utamkuta bibi yako pale amekaa peke yake" alisema huku akinionyesha kwenye mti wa size ya kati wa mhare akimaanisha ndiyo sehemu ambayo ningemkuta bibi yangu mchawi amekaa.

"ukifika msalimie kwa adabu, halafu muombe maji ya kunywa. Akikubali tu kufata maji jua kazi yetu imeisha"

"Hivyo akikuletea hayo maji wewe
, Yapokee halafu yamwage chini bila kusema lolote"

Tuliondoka tukarudi hadi nyumbani kwake. Kweli alinifanyia dawa. Siku hii mzee alitumia muda mwingi akifanya mambo yake ya ajabu ajabu ambayo sikuelewa yalikuwa na maana gani.

Mida ya jioni kweli tuliondoka maeneo yale, safari hii tuliondoka na baiskeli. Mimi ndiye niliyekuwa naendesha...

Tulienda hadi nyumbani kwetu tukaiacha ile baiskeli. Halafu tukatembea kwenda kwa huyo bibi. Tulipofika mganga aliniambia simama kidogo halafu utaenda baada ya dakika kama tano. Aliondoka hadi kwenye shamba lililokuwa pembeni na maeneo yale. Au niseme shamba ambalo lilikuwa la babu yangu ambalo mwanamke huyo alipewa kama mali yake baada ya kifo cha babu.

Nilikadiria muda baada ya kuona dakika tano zinaweza kuwa zimetimia niliondoka na kwenda pale nyumbani. Huwezi amini nilimkuta kweli yuko peke yake, nilienda moja kwa moja hadi alipokuwa amekaa pale kwenye mti.

Nilitamani nisimsalimie kwa hasira niliyokuwa nayo. Lakini nikakumbuka mzee Masele aliniambia nikifika nimsalimie kwanza tena kwa adabu.

"Bibi umeshindaje" kisukuma hakina shikamoo.

"Salama tu babu yangu" alijibu lakini alionekana dhahiri alishtuka ni kama hakutegemea kuniona pale kwa wakati ule.

Nilivyomaliza sikutaka kupoteza muda, nilimuomba maji ya kunywa.

"Nilimuona akisimama na kufata maji ndani"

Jambo hili lilinifanya niwaze na kuona kwamba kweli dawa zina nguvu zinaweza zikakufanya ukafanya maamuzi bila wewe kujua. Niliwaza hivyo kwa sababu kwanza mimi haikuwa mara ya kwanza kwenda pale, nilikuwa mwenyeji na niseme ni kama nimekulia pale. Kwa sababu toka enzi za marehemu babu yangu tulikuwa tunaenda pale kucheza nikiwa mtoto bado, hivyo nilijua vizuri sehemu ambayo maji yalikuwa yanatunzwa. Na siku zingine za nyuma kabla ya uhasama ulioletwa na kugombania ardhi nilikuwa naenda pale, nikisikia kiu naingia ndani nachota maji mwenyewe bila hata kuomba. Hivyo siku hiyo mimi kuomba pale maji yalikuwa ni maajabu! Bibi kunifatia maji yalikuwa ni maajabu zaidi, kwani kikawaida angeniambia niende tu nikachote maana sikuwa mgeni pale.

La pili nilikuwa ninaamini anajua nimeenda kwa mganga, kutokana na yeye mwenyewe kunifukuzia usiku nikiwa na Vumilia wakati tunaenda kwa mganga. Sasa kitendo cha kufika na kuomba maji moja kwa moja yeye kama mshirika wa haya mambo ya ushirikina nilidhani labda angeshtuka! Nilitegemea angegundua kuna mchezo mchafu anataka kufanyiwa.

Lakini haikuwa hivyo aliniletea maji, nikayamwaga chini. Nilipomaliza tu lile zoezi la kumwaga maji chini,nilisikia anatoa sauti ya maumivu kama amejiumiza sana sehemu fulani au amechomwa na kitu fulani kinachomletea maumivu.

"Ishiiiiiii! Nakufa" alijisemea mwenyewe

Palepale nikajua kazi imeanza!

Itaendelea

NB: huu uzi nimeuandika nikiwa na usingizi sana ila naamini unaeleweka! Usipoeleweka mnisamehe nitaelezea vizuri zaidi kwenye miendelezo inayofata.

Itaendelea. Usiku mwema.
 
Dah
Shukrani sana kwa kutukumbuka leo

Naona mambo yanazidi kuwa moto
Tuko pamoja
 
Ahsante mkuu,
Tunasubiri kwa hamu episode zinazofuata,

Mm siamin uchawi, but I am here to enjoy the story πŸ˜ŠπŸ™
 
Kuna picha imenijia nikakumbuka siku moja nikiwa zamu kazini alikuja binti akilalama kwamba anahisi kuna vitu kama vijiti mwilini mwake kama njiti za uzazi wa mpango mikononi na sehemu za mapajani nikamdadisi huenda alichomwa na vitu lakini alikataa kata kata baada ya kufanya examination nilivibaini lakini hakukuwa na port of entry nilistaajabu nilitoa sindano nyeusi 5 mapajani 3 na mikononi 2 nikiri haikuwa rahisi leo nimeanza kuelewa sasa nini kilifanyika
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…