Sehemu ya 14.
Nilianza kupiga hatua kuelekea nyumbani nikiwa na lengo la kumtafuta Vumilia. Ni kweli alikuwa amenisaidia katika wakati mgumu, lakini sikupendezwa na nguvu anayotumia kulazimisha mapenzi. Nilitembea hadi kijijini kwetu nikiwa na Lengo la kwenda nyumbani kabisa pale kwa bibi yake. Lakini nikiwa njiani nilipata wazo la tofauti, nikaona kwenda kwa bibi yake ingekuwa ni hatari kwangu. Nilifahamu ingekuwa ni hatari maana bibi yake ni mchawi aliyekubuhu. Nilighaili nikajisemea nitamsaka tofauti na pale kwenye mazingira ya nyumbani kwao.
Niliondoka nikaenda hadi nyumbani. Ilipofika jioni nikawa nimetoka na washkaji zangu kuelekea Centre. Bado nilikuwa na lengo la kumsaka Vumilia. Tulienda kukaa sehemu wanapocheza pool table tukawa tunapoteza poteza time. Tulikaa pale hadi mida ya saa moja kama na nusu hivi, usiku. Tukaanza kurudi nyumbani tulikuwa watu kama sita hivi kwa wakati huo. Sasa wakati tupo tunaendelea kutembea, wakati huo nilikuwa nimebanwa na mkojo. Tukafika sehemu ambapo kulikuwa na miti mingi na vichaka na hakuna nyumba za watu kwa mita kama Mia mbili hivi. Sehemu ambayo niliwahi kufuatwa na vishindo vya mtu bila kumuona (tukio nililolieleza huko nyuma). Niliona mahali pale ndio pazuri kuachia mkojo, nikaenda pembeni kidogo ya njia nikafungua suruali na kuanza kukojoa. Wakati huo washkaji walikuwa wanaendelea kutembea mbele. Ile namaliza kukojoa nageuka nyuma niwakimbilie washakji niliokuwa nao, nikashangaa kumuona Vumilia akiwa amesimama nyuma yangu.
"Vipi Vumilia umetokea wapi tena! "
Hakujibu kitu aliniangalia kama mtu aliyekuwa ananidadisi bila kusema chochote.
"Halafu ujue nilikuwa nakutafuta" nikamwambia
"Ulikuwa na shida gani" aliuliza
"kwa nini unatesa watu wasiohusika, kwenye issue yangu na wewe"
"Kivipi"
"Kwa nini ulimlaza Sara nje tena kwenye miiba. Kwani amekukosea nini?"
"Hujui alichonikosea? Labda nikuulize kwa nini unahisi mimi ndiye niliyemlaza nje na sio mtu mwingine"
Nilikaa kimya nikitafakari jibu la kumpa.
" Leo ndio nimethibitisha kwamba unampenda Sara kuliko mimi, Sikutaka kukufanyia ninachofikiria lakini kwa sasa sina jinsi"
Alivyoongea vile alinipiga kofi kidogo, baada ya pale sikuelewa vizuri kipi kilifuata. Ni kama nilipoteza fahamu kiasi, ila ninachokumbuka nikawa ninamfuata kwa nyuma. Njia tuliyopita wala sikuifahamu.
Fahamu zote zilikuja kurejea baadae, nikajiona nikiwa nimesimama kwenye mlango wa nyumba moja ya nyasi. Wakati huo Vumilia alikuwa mbele yangu anafungua mlango. Niliyafahamu vizuri yale mazingira, ilikuwa ni nyumbani kwa Yame, bibi yake Vumilia.
Nilichanganyikiwa nilijua sasa nimebonyeza wrong button. Niliwaza nikimbie lakini moyo ukawa mzito sana. Mlango ulifunguka halafu Vumilia akasimama pembeni ya mlango. Kwa ndani aliyetokea alikuwa ni bibi yake Yame, ambaye alinishika mkono na kunivuta kwa ndani. Niliingia ndani nikakuta kulikuwa na mwanamke mwingine wa makamo ambaye nilimfahamu pia. Baadaye Vumilia nae aliingia ndani. Nikawa nimekalishwa chini.
Mle ndani kulikuwa na moto unawaka ndio uliokuwa unatoa mwanga. Wote sasa tukiwa wanne tukawa tumekaa tumetengeneza ka mduara fulani. Yaani mimi, Vumilia, Yame na yule mwanamke mwingine.
Muda wote nilikuwa kama nimepigwa bumbuwazi sikuweza kuzungumza chochote Zaidi ya kutumbua macho, nilikuwa kama kondoo akiwa machinjioni. Sikujitetea!
Baadaye Yame nilimsikia akisema
"Dashi! Unasubiri nini sasa!, Wakati tunakusubiri hapa. Fanya haraka!" Aliongea kwa sauti ya kufoka
Baadae niliona ngazi imeshuka kutoka kwenye dari. Nilimuona mtu mmoja akiwa na nywele ndefu sana na mchafu kupita maelezo, akishuka na ngazi hiyo kutoka kwenye dari akiwa ameshika sahani. Sahani hiyo aliyoishika ilikuwa ni kibuyu kilichokatwa kiustadi kutengeza umbo la sahani. Aliishusha hadi chini hiyo sahani akaiweka katikati yetu. Nilikaza macho kwa umakini ili nione kwenye ile sahani kulikuwa na kitu gani. Aisee! Ilikuwa ni sahani iliyojaa nyama zilizonona sana!
"Kula sasa"
Nilifikiria kugoma nisile. Nikakumbuka maneno ambayo niliwahi kuambiwa na mtu fulani. Alisema katika uchawi wote duniani, hakuna uchawi mbaya kama ule utakaopewa kwa njia ya chakula. Huo uchawi huwa ni mgumu sana kuaguliwa na kupona, maana dawa zinakuwa zimewekwa ndani ya mwili sio nje!
Niliona hapa nikijichanganya kula tu. Nimekwisha!
"Kula basi usiogope"
Bado niligoma, sikuwa tayari kunyoosha mkono wangu kula ile nyama. Japo machoni ilionekana kuwa tamu sana! Ghafla bin vuuu nilishangaa nakabwa na lile jamaa lenye manywele marefu huku yule mama mwingine aliyekuwemo, akinifungua mdomo kwa lazima kwa kuutanua kwa kutumia mikono yake. Wakati huo mimi nilipambana niweze kujinasua mikononi mwao. Ikawa ni mapigano mle ndani, nilikabwa na wote mle ndani na kulazimishwa kutanuliwa mdomo ili nile. Juhudi zangu za kujaribu kujinasua ziligonga mwamba kwani walifanikiwa kuniwekea zile nyama nikazila zote.
Kiukweli zile nyama zilishabihiana na mwonekano wake. Zilikuwa ni nyama tamu sana. Katika nyama zote nilizowahi kula hadi leo hii, bado sijaona nyama yenye ladha tamu kama ile. Labda siku nikija kula vipande vya kuku KFC nitaleta mrejesho!
Nililishwa hadi nikamaliza nyama yote iliyokuwa kwenye bakuli. Na mpaka leo sijui ile nyama ilikuwa ni ya nini!
Baada ya tukio hilo, nilinyanyuliwa nikatolewa nje. Halafu nikaamriwa kwenda nyumbani. Niliondoka kwenda nyumbani, huku nikiwa nimejaa mawazo mengi kichwani. Nilikumbuka maneno ya mzee Masele aliponambia Yame ana dawa ambazo yeye mwenyewe Masele pamoja na ugwiji wake (ambao nilikuwa nimeushuhudia) lakini pale kwa Yame alikuwa ananyoosha mikono. Niliwaza sasa nilikuwa nimeyakanyaga rasmi. Bado sikujua nia yao ilikuwa ni nini lakini niliamini walikuwa na sababu ya kufanya vile. Na niliamini hawakuwa na lengo zuri!
Huwa nina tabia fulani ya kupenda kuwa msiri sana! Hasa kwa wazazi wangu! Na mara nyingi huwa sipendi kuwapa hofu wazazi wangu kwa sababu ya matatizo ninayoyapitia.
Hivyo pamoja na tukio hilo lililotokea kuwa lilikuwa la kuogofya, lakini sikutamani kumwambia mtu yeyote nililiacha iendelee kuwa siri.
Itaendelea!
I'm here to stay...