TAJIRI MKUU WA MATAJIRI
JF-Expert Member
- Dec 1, 2010
- 11,999
- 24,328
Mwaka 1902, mji wa Hanoi nchini Vietnam ulishuhudia moja kati ya mipango ya kijinga, ya kuchekesha, na iliyoacha kovu la aibu katika historia ya ukoloni wa Ufaransa—jaribio la kutokomeza panya kwa kuwalipa wananchi kwa kila mkia wa panya walioleta! 🐀💥🇫🇷🇻🇳
Kisa hiki kilianza wakati wakoloni wa Kifaransa walipovamia Hanoi. Ili kuonyesha ukubwa na ustarabu wao, walijenga miundombinu ya kisasa, ikiwemo mfumo mkubwa wa maji taka chini ya ardhi. Lakini bila wao kujua, walikuwa wamejenga hoteli ya nyota tano na paradiso ya panya chini ya mji huo.
Mamilioni ya panya wakaanza kuzaliana kwa kasi ya ajabu. Mfumo wa maji taka ukawa barabara kuu ya panya hao kuvamia mitaa ya wazungu, majumba yao, na kuanza kueneza magonjwa ya kutisha kama tauni.
Wafaransa walipopatwa na hofu, walianza kwa kuajiri timu maalum ya wakamata panya. Timu hiyo iliuwa maelfu ya panya kila siku, lakini idadi ya panya haikupungua hata kidogo. Ndipo maafisa wa Kifaransa walipokuja na wazo walilodhani ni la "kitalaamu mno": Kwanini tusiwalipe wananchi wenyewe ili watufanyie kazi hii?
Serikali ya Kifaransa ilitangaza zawadi ya fedha kwa kila panya atakayeuawa na mwananchi. Lakini ili kuzuia adha ya kuletewa mizoga ya panya waliooza na kunuka kwenye maofisi ya serikali, waliweka sheria moja fupi: "Leta mkia wa panya tu kama ushahidi, na utalipwa fedha zako."
Maafisa wa Kifaransa walifurahia sana wazo hili, wakiamini wananchi wangeingia msituni na kwenye mifumo ya maji taka kusafisha mji. Lakini walisahau kanuni moja kuu ya saikolojia ya mwanadamu.
Wananchi wa Vietnam waligundua kitu kimoja cha dhahabu: Ukimuua panya, unakuwa umeua chanzo chako cha mapato!
Badala ya kuua panya, wananchi wakaanza kutumia akili ya ziada:
Walikuwa wakimkamata panya, wanamkata mkia kwa kisu, kisha wanamwachia arudi kwenye mfumo wa maji taka akiwa hai! Lengo lilikuwa ni panya huyo asife, bali aendelee kuzaliana na kutengeneza panya wengine wengi wenye mikia mipya ya kuja kukatwa baadaye!
Baadhi ya wananchi wenye akili za kibiashara walianzisha mashamba maalum ya kufuga panya kwenye maeneo ya vijijini nje ya mji. Walikuwa wakifuga panya wengi tu kama kuku, kisha wanawakata mikia na kwenda kuwauzia Wafaransa!
Wengine walianza kuagiza na kusafirisha panya kutoka mikoa ya jirani kuja Hanoi ili tu kupata mikia ya kuuza.
Baada ya miezi kadhaa, Wafaransa walishangaa kuona wanalipa mamilioni ya dola kwa ajili ya mamia ya maelfu ya mikia inayomiminika kila siku, lakini idadi ya panya mjini Hanoi ilikuwa ikiongezeka badala ya kupungua!
Siku ambayo maafisa wa Kifaransa walitembea mitaani na kuona makundi ya panya wasio na mikia wakiruka na kucheza kwa furaha kwenye mifumo ya maji taka, ndipo walipogundua kuwa wamechezewa mchezo wa akili wa hatari mno. Walisitisha mpango huo mara moja kwa aibu kubwa.