And Another!
Katika harakati za kutafuta Ugali nilijikuta nimeomba kujiunga na jeshi la JKT. Nikatupiwa Kigoma, kule Bulombora 821KJ.
Nikapigishwa jaramba na kulishwa vumbi la kutosha huku nikitazama ziwa Tanganyika kwa ukaribu kabisa lililozungukwa na mawese ya kushato. Ruka Juu, Kanyaga Chini kwa nguvu mpaka mguu utoke nje ya kiatu.
Mikesha ilivyozidi nikaona hapa nitakufa. Nikaanza harakati za kutafuta nafasi ya kulala vizuri maana zile Dakika 5 unazopewa za kulala hazitoshi kabisa. Nikaanza kutafuta machimbo. Wenzangu wakienda mkesha, mimi najipeleka porini. Siku nyingine nakutana na ma afande na wao wamedoji kwenda lindo wananitimua najikuta nimerudi kulala uvunguni.
Tabia yangu ya kujizoesha kulala ikaanza kunigharimu. Ikafika mahali nikawa siwezi kabisa kwenda kukesha hata siku moja. Nikaanza kuona hadi uvivu wa kwenda kulala mbali na anga letu. Nakumbuka nilikua Eagle Coy.
Siku hiyo nimelala uvunguni nakoroma kabisa, saa ngapi afande asiingie ndani kutafuta watoro. Si akaniskia navyokoroma kule chini ya kitanda. Dah sitasahau hiyo kipigo niliyopewa. Nakumbuka al manusura nipoteze jicho. Maana vile vitanda vimechomelewa kwaiyo kuna kama vichuma flani hivi kama nondo vimejitokeza kwa juu, alinibamiza kichwa kwenye kile kitanda ile nondo ikachubua kidogo pembeni ya jicho.
Sijui nilipata wapi ujasiri nikamsukuma pembeni nikasogeza kioo cha dirisha nikarukia nje nikaanza kukimbia huku nachechemea machozi yananitoka ya kutosha. Jamaa nadhani aliniangalia navyokimbia kwa tabu akanionea huruma akaamua kuachana na mimi huku akisema "Nitakuua Mbwa Wewe".
Nilivyofika walipo wenzangu kwenye mkesha nikapokelewa tena na adhabu za kubiringita na kukwepa ndege za kivita. Dah.. nilihisi mwisho wangu umefika, nikasema kwa sauti "Nakufa" huku machozi yanatoka ili hata jamaa anionee huruma lakini wapi. Yeye kakazana kunioshea na kunifanya mfano kwa wengine. Saiyo pumzi imekata, maumivu kila mahali, machozi yameshatoka mpaka yamekauka, siwezi kuongea tena. Ni kwa Neema za Allah pekee nilifanikiwa kuona tena Jua siku iliyofuata maana nilikua nahisi kabisa nakufa. Hali yangu ilikua mbaya sana!
Sikuwahi kujuta kwenye maisha yangu kama hiyo siku. Nililaani uamuzi wangu wa kwenda huko. Kile kitu kilinikaa sana moyoni kwa muda mrefu. Niliona kabisa huku sio kwangu. Course ilivyoisha, wakati wengine wanasikilizia kwenda JWTZ na Polisi, mimi nikaandaa nauli yangu, nikavizia ule muda tunaotumwa kwenda town...nikatorokea huko mazima na nikaapa sitarudi tena. Ikawa imeisha hiyo!
Kwa kweli mambo ya Jeshi yana watu wake. I was not one of them!