SoC03 Kizungumkuti Wizara Michezo na utengaji bajeti ya ukarabati wa viwanja vya Michezo vinavyomilikiwa na chama

SoC03 Kizungumkuti Wizara Michezo na utengaji bajeti ya ukarabati wa viwanja vya Michezo vinavyomilikiwa na chama

Stories of Change - 2023 Competition
Joined
May 5, 2023
Posts
7
Reaction score
5
KIZUNGUMKUTI SEKTA YA MICHEZO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA BAJETI YA WIZARA YA MICHEZO, SANAA NA UTAMADUNI

Kwa miaka kadhaa sekta ya michezo imekuwa ikizidi kukua siku hadi siku na kujiongezea wafuasi ambapo katika mpira wa miguu ni eneo ambalo kwa sasa lina mashabiki wengi, pamoja na kuwa na mashabiki wengi wa ndani nje pia ligi yetu imezidi kupaa katika medani za kimataifa na kuwa miongoni mwa ligi bora Barani Africa.
Mbali na hivyo vilabu vyetu vikubwa hapa Nchini navyo vimezidi kuimarika na kuleta ushindani wa kweli baina ya vilabu vikubwa Barani Africa ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita ambapo matokeo ya mechi za nje kwa vilabu vyetu yalikuwa yanatia aibu. PONGEZI KWA WAWEKEZAJI KATIKA VILABU HIVI.

Hoja yangu kubwa;
Sambamba na hayo yote lakini hoja yangu kubwa ni kuwa; kiujumla bado miundombinu ya sekta ya michezo ya mpira wa miguu kwa ujumla wake ni mbaya ukilinganisha na bajeti za Wizara husika ambazo zimekuwa zikitajwa kuwekwa kila mwaka kwa miongo kadhaa. Je, fedha za bajeti hizi zimekuwa zikifanya kazi gani? Na uwasilishwaji wa matumizi ya fedha hizi kuwa zimefanya kazi gani katika sekta ya michezo kwa ujumla wake umekuwa hakuna, jambo linalopelekea kuwa na ombwe la mawazo kuwa huenda tumekuwa tukichezewa “mazingaombwe” kuambiwa kuna bajeti kumbe hakuna au ni kweli kuna bajeti lakini kumbe inatumika kunufaisha wachache au Taasisi zisizohusiana na michezo.

Lakini jambo jinginge ni kuwa; ikiwa tunatambua kuwa karibu asilimia kubwa viwanja vyetu vya michezo vinavyotumika katika Ligi yetu hasa vya Mikoa mbalimbali vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM). Japo umiliki wake mpaka leo bado najiuliza ulikuwaje (Kwa sababu zilikuwa ni zama za ujima wacha tuendelee) hii ni kutokana na kuwa nimejaribu kufuatilia historia ya ujenzi wa baadhi ya viwanja na wahusika waliokuwako/kuhusika kujenga siku hizo kusema ya kuwa, kipindi hicho kulikuwa na kodi (ambayo ilikuwa inatozwa na Serikali na siyo chama) sasa kwa Raia ambao hawakuwa na kiasi hicho walibebwa kwenye karandinga (gari) na kulazimishwa kufanya kazi ya kujitolea kujenga viwanja hivyo ili kufidia kodi hiyo. Mfano; uwanja wa Allly Hassan Mwinyi Tabora. Sasa bado sijajua ni nini kilitokea baada ya viwanja kukamilika vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi hatimaye kukabidhiwa kwa Chama?

Swali langu ni kuwa, ikiwa viwanja hivi vinamilikiwa na chama imekuwaje Serikali kutenga bajeti ya ukarabati wa viwanja hivi? Mfano: mwaka jana/juzi tumeona Serikali walitenga bajeti ya Bilioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa viwanja 7 vya mpira wa miguu katika maeneo tofauti ya Nchi. Lakini miongoni mwa viwanja hivyo ni viwanja VIWILI TU ambayo tuliambiwa na Wizara kuwa vinamilikiwa na Serikali, ambavyo ni uwanja wa Benjamin Mkapa na uwanja wa Uhuru vyote vya Dar es Salaam. Hoja inakuja kuwa wamiliki wa viwanja hivi wamekuwa wakilipwa ushuru/kodi na vilabu kila mechi inapochezwa na kila muhusika anapata gawio lake ikiwa ni pamoja na Serikali wenyewe kupitia Shirikisho lake la Soka la Tanzania.

Sasa kwanini wamiliki wa viwanja wasitumie fedha zao za kodi kukarabati viwanja ikiwa wanapata kodi? na Serikali kujenga au kuwekeza kwenye miundombinu ya Serikali? Kwa sababu inawezekanaje Serikali kutenga bajeti kwa miradi ya Taasisi binafsi, na je, ikiwa jambo hilo liko Kikanuni/Sheria inawezekana pia Serikali ikatenga bajeti kwa miradi inayomilkiwa au kuendeshwa na Vyama vingine vya upinzani?.

Nini kifanyike
Serikali ije na majibu na hoja hizi lakini pia uwazi wa matumizi ya bajeti ya Wizara ya Michezo Sanaa na Utamaduni iwekwe wazi na kama kuna fedha zinazotumika kulipa wasanii kuimba/kushiriki katika makongamano ya Kiserikali na Chama matumizi yajulikane kwa maslahi mapana ya Taifa. Kwasababu uhalisia wa bajeti tajwa kwa kila mwaka na matokeo ya kile kinachoonekana haviendani kwa kiasi kikubwa.

Vilevile Serikali ibainishe Kanuni/Sheria ipi iliyopelekea umilikishwaji wa viwanja vya michezo kwa CCM ambavyo kimsingi historia yake vimejengwa kwa nguvu za wananchi, pia ni kifungu cha Kanuni/Sheria gani kinachoruhusu wao kama Wizara kutoa fedha za ukarabati au uendeshaji wa miradi ya Taasisi binafsi ambazo zinafanya biashara na kupata mapato yake yatokanayo na Vilabu vinavyotumia viwanja hivyo.

Ikiwa hakuna kifungu cha Sheria/Kanuni ambayo ipo Sheria inayoruhusu utoaji wa fedha/bajeti kwa ajili ya miradi ya Taasisi binafsi, basi rai yangu ni kuwa viwanja vyote vinavyomilikiwa na Chama virudishwe mikononi mwa Serikali kwani fedha wanazotumia Serikali kutenga bajeti ya ukarabati wa miundombinu hizi ni fedha za walipa kodi (Wananchi) ambao walilipa kodi pia kwa kutumia nguvu zao wakati wa ujenzi wa miundombinu hizo. Kwa kufanya hivyo tutaliokoa Taifa lijalo na ombwe hili ambalo litapelekea siku za usoni vizazi vijavyo kuambiwa vitega uchumi vyote vikubwa Nchini ni mali ya chama au Taasisi flani kwa sababu hakuna kumbukumbu/taarifa zozote zinazotunzwa juu ya umilikishwaji wa mali za umma kwa Taasisi au watu binafsi kwa muktadha wa vizazi vijavyo.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom