"Tulikokuwa tunaenda siko, tumeamua kugeuka" - Mhe. Anne Kilango Malecela
...mambo ambayo anayazungumzia ni pamoja na ... kwanini wabunge wa CCM walikuwa wanaitetea serikali yao hata ilipokuwa inaharibu
... kwanini anaamini Kikwete ni kweli anataka mabadiliko
...Mimi niko impressed na watu mara chache sana.. this is one of those times.
Anna Kilango Malecela (Mb.) ni shujaa kweli kweli. Ni wachache ndani ya CCM, kama wapo, ambao wanamshinda kwa uwazi, juhudi na ari mpya ya kuleta mabadiliko. Hata hivyo, japo ana nia ya dhati ya kufanya kazi za Wananchi, uchambuzi na uelewa wake wa masuala ya Kisiasa una mushkeli nyingi. Aidha anaogopa kusema anachotaka au anashindwa kuwasilisha anachotaka kukisema. Na inawezekana hajui kinachoendelea.
Kuhusu ufisadi, anasema tatizo kubwa lililotufikisha hapa tulipo ni kwamba mali za nchi hazilindwi na viongozi. Ukisema viongozi hawalindi mali za Umma unatenganisha wezi na walinzi. Huu uchambuzi aidha ni wa asiye jua picha halisi ya Ufisadi au wa anae ogopa kusema Viongozi ni wezi wa mali za Umma. Hakuongelea matatizo ya kutokuwepo kwa ufuatiliaji wa Sheria au kutokuwepo kwa Sheria za kuwakamata Mafisadi.
Anasema suluhisho la matatizo yetu ni kubadilisha mfumo wa kiuchumi ambao unaruhusu wachache kumiliki mabilioni ya pesa huku walio wengi hawana kitu. Halafu hapo hapo anasema hayo mapesa yanayomilikiwa na wachache sio yao, bali, ni ya Serikali. Tatizo la kutoelewa au labda kushindwa kujieleza linajitokeza hapa. Kama wachache wanamiliki pesa zisizo kuwa zao basi hilo ni tatizo la ufisadi, tatizo la wizi, na sio tatizo la mfumo wa Uchumi. Utabadilisha mfumo, na hata ukafufua Azimio la Arusha, lakini kama kujapigana na ufisadi, mfumo wako mpya labda ndio utakuongezea matatizo maana utazidi kujichanganya. Sasa hivi Watanzania tumechanganyikwa juu ya mfumo wa Siasa na Uchumi tunaofuata, kati ya Ujamaa na Kujitegemea au Ubepari unaoruhusu njia kuu za uchumi kumilikiwa na wachache. Kubadili mfumo wa Kiuchumi peke yake hakuwezi kutatua ufisadi.
Akitetea jinsi Bunge la CCM lilivyo kuwa limelala usingizi, anasema hata South Africa walitawaliwa na Makaburu mpaka siku moja wakaamua kugeuka, wakaona hawawezi kuongozwa na makaburu wachache. Huu mfano hauhusiki, kwa sababu hakuna siku wa South Africa walikuwa wanaona ni sawa kutawaliwa na Makaburu. Vita vya kwanza dhidi ya Wadachi vilianza siku maharamia wa kampuni ya Dutch East India Co. walipotia mguu kwenye ardhi za wa KhoiKhoi karne ya 17. Tofauti na wapigania Uhuru wa South Africa, hili Bunge la CCM ya Mama Malecela lilikuwa limelala likiota njozi za Alinacha. Ni pale wakina Zitto, Slaa na wengine wawili watatu walipoonekana ndio peke yao wanafanya kazi kati ya mamia ya Wabunge wa Jamhuri ndipo wakina Mama Malecela walipoona soni na kuzinduka kutoka katika usingizi wa
Rip Van Winkle!
Uchambuzi wa Siasa za Uchaguzi wa Anne Malecela nao una matatizo makubwa ya kurahisisha rahisisha mambo. Anasema Kikwete alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa CCM na baadaye kwa 80% kwenye uchaguzi mkuu. Kwa mtaji huo, anadai, si yeyote bali ni wananchi waliomchagua Kikwete. Sasa hili ni jaribio la wazi wazi la kuficha madhambi ya CCM wakati wa Uchaguzi. Kwamba chaguzi za CCM zimejaa mizengwe na shutuma za rushwa. Ndo maana kabla ya Mkutano Mkuu mgombea tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, ilibidi atoe onyo rasmi kwamba safari hii akifanyiwa mizengwe katika kuchagua jina la tiketi basi hatokubali; Ndo maana kuna vikundi vya "Mtandao" na "wasio Mtandao" ndani ya CCM; Ndo maana mpaka leo Zanzibar kunafukuta moto kufuatia chaguzi za CCM zilizo jaa mushkeli, dhulma, na zahma za mateso dhidi ya wapinzani, na wakati mwingine hata umwagaji damu. Ndo maana waasisi wa CCM, wakina Butiku wamekuwa wakisema wameshuhudia rushwa zikitembea mchana mchana kwenye chaguzi za CCM; Ndo maana Mahakama Kuu ilifutilia mbali ufisadi wa wazi wazi wa uchaguzi uliobatizwa jina la kuficha ficha, takrima. Kwa hiyo, Malecela hawezi kusema eti matokeo ya kura yanaonyesha matakwa ya wananchi. Hawezi kujifanya hajui kwamba wapo wachache fulani wazito waliohusika katika kumchagua Kikwete, zaidi ya kura za Wananchi. Malecela, mbunge wa ngwe ya pili, si mgeni wa Siasa na atakubaliana na mwandishi wa Kimarekani aliyewahi kusema "ukweli haujulikani kwa kura ya wengi."
Mama Malecela pia aliharibu vibaya vibaya aliposema Kikwete ana nia ya kuleta mabadiliko eti kwa sababu katika hotuba yake ya kwanza Bungeni aliahidi kupitia upya mikataba. Malecela pia anamsifu Kikwete kwa kuliambia Bunge kwamba hana ubia na kiongozi na kwamba aliliambia Baraza lake la Mawaziri la kwanza kwamba wasilaumiane mbele ya safari kama wakilega lega kwenye kazi. Tatizo ni kwamba amempasisha Rais kwa maneno ya hotuba aliyo yatoa alipopata Madaraka. Kikwete amemaliza nusu ya Utawala wake sasa hivi, utawezaje kumtathmini kwa kuangalia alichosema siku anachukua madaraka?
Huwezi kutuambia Kikwete ana nia ya kuleta mabadiliko bila kutueleza inakuwaje kuwaje anateua mafisadi kutwa kucha, akidharau nasihi za wananchi kuhusu sifa chafu za teuzi zake. Rais anaefukuza Gavana wa Benki halafu anamrithisha kazi msaidizi wa aliyemfukuza. Rais anaewaambia viongozi wasiogope kuitwa mafisadi, akidharau msingi muhimu wa maadili ya uongozi unaosema Kiongozi yabidi aepuka, sio tu ufisadi dhahiri, bali hata taswira ya ufisadi. Rais anaekalia ripoti za uchunguzi wa ufisadi bila kujali vilio vya wananchi vikiomba azitoe hadharani. Rais anae waambia wananchi kwamba viongozi wastaafu wanaoshutumiwa na Ufisadi kushoto na kulia "waachwe wapumzike." Rais anaevumilia kuona kilindi cha kiza kinagubika mazingira ya kutoweka kwa mashahidi na washutumiwa wa ufisadi wa mabilioni ya fedha za jasho la masikini wa kutupwa!
Ukitetea Rais kama huyo, tunaweza kusema aidha huelewi elewi kinacho endelea au na wewe juhudi zako inawezekana ni changa la macho. Kinacho fadhaisha zaidi na zaidi ni kwamba watu kama Mbunge Anne Malecela ndio tegemeo la nchi, ndio
crème de la crème ya uongozi wa nchi yetu, halafu nao hawajui kinachoendelea!