Kodi ya Majengo Kwenye Luku ni ya Mwenye Nyumba Sio Mpangaji
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu kodi ya majengo ambayo imeanza kulipwa jana Agosti 20, 2021 kupitia makato wakati wa ununuzi wa LUKU za umeme baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria hiyo hivi karibuni.
Katika mkutano uliofanyika leo Jumamosi, Agosti 21, 2021 katika mtandao wa ZOOM ukiongozwa na Taasisi ya Watch Tanzania, mkutano huo umewashirikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndio wakusanyaji wa mapato, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Pamoja na Bunge ambalo ndilo lilitunga sheria hiyo.
MWAKILISHI WA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA (TRA)
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo
Kodi ya majengo sio kitu kipya, imekuwa ikitozwa kwa namna tiofauti, mwanzoni ilikuwa kwa asilimia ya thamani ya jengo baadae tukaja na flat rate. Changamoto ilikuwa kila mwaka mtu afuate control number kisha alipe kwa wakala au simu yake.
Serikali inatakiwa ipate pesa yake, mwananchi wengine walikuwa akipata penati kutokana na madeni haya.
Kodi hii inatozwa kwa majengo ambayo yamefanyiwa uendelezaji wa ardhi, iwe imepimwa au haijapimwa. Na hii itafanyika katika majiji na manispaa Tsh 12,000 (kwa mwaka) yaani Tsh 1,000 kila mwezi kwa nyumba za kawaida, tutakusanya kupitia manunuzi ya umeme.
Jengo la ghorofa moja litachajiwa chini atalipa Tsh 60,000 na juu Tsh 60,000 jumla Tsh 120,000. Itakuwa tsh 5000 kwa kila sakafu hivyo 10,000 kwa mwezi. Majengo yaliyo makao makuu ya wilaya, ghorofa itatozwa jumla ya Tsh 60,000 tu bila kujali ni ghorofa moja au Zaidi.
Jengo la kawaida haijalishi lipo wapi kwenye jiji au manispaa, itakuwa 12,000 maeneo yote. Kwa nyumba ambazo hazitumii luku lakini zinatumia umeme wataendelea kulipa kupitia Ankara zao za kawaida (bill) lakini ambao hawana umeme au wanatumia sola wataendelea kulipa kwa sababu ni wajibu wao kisheria kulipa.
Nyumba za vijijini hazihusiki, hazitozwi. Nyumba ambazo zimejengwa kwa vifaa ambazo hazidumu hazitozwi, za udongo na nyasi pia hazitozwi.
Wanaohusika wakitozwa wafike TRA kutoa taarifa, maofisa wetu wameshapewa maelekezo wasiohusika (waliosamehewa) na nyumba ambazo hazina vigezo vya kutozwa wasitozwe, wakiwemo wazee ambao wana msamaha.
Kwa mwenye nyumba kama ana luku mbili kwenye nyumba moja, kwa sasa luku zote zinatozwa, lakini anaweza kuja Tanesco na kueleza nil uku ipi itatumika kulipa kodi.
Kodi hii inatakiwa kulipwa na mwenye nyumba na si mpangaji, hivyo anaweza kufanya mawili… mwenye nyumba anaweza kupunguza kwenye kodi yako ya nyumba Tsh 12,000 au kumnunulia mpangaji wake umeme wa Tsh 12,000 kwa mwaka, lakini kama watashindwa kuelewana mwenye nyumba na mpangaji wake hiyo ni juu yao.
Kwa ambao walikuwa wameshalipa kwenye mfumo wa zamani basi wafike ofisi ya TRA iliyo karibu nae tuone namna ya kufanya. Kama alikuwa anadaiwa hilo deni lipo kwa mujibu wa sheria atalazimika kulipa, kubadilisha mfumo haimanishi deni limeisha.
Tozo hiyo atakatwa kila mwezi, mara moja tu kwa mwezi, hatutozi ya mwaka mzima kwa pamoja, ila kama umelimbikiza madeni utalazimika kuyalipa kwanza pale tu utakaponunua umeme.
Kama una nyumba na kibabda cha kuchajisha simu utalipa kama kawaida. Nyumba za serikali zinazotoa huduma kama shule za umma, hospitali za umma, majengo ya halmashauri, huduma za TRA hayo hayalipiwi, lakini kama unaishi nyumba ya serikali utalipa.
Nyumba zinazotoa huduma kama shule binafsi nna hospitali binafsi zitalipishwa sababu zinafanya biashara. Utaratibu watu hawajauzoea, ilitakiwa ianze Julai mosi, ndio maana walionunua jana, wamekatwa tozo ya Julai na mwezi Agosti.
Kwa wazee, waje na uthibitisho wa nyumba moja anayoishi ikionyesha umri wake, isiwe nyuba ya biashara iwe ya kuishi, kama imepangishwa itakosa sifa na badala yake atalipa sababu inaingiza kipato. Kama anazo nyumba mbili au tatu na ana wake wawili watatu kila mmoja kwenye nyumba yake, nyumba moja haitalipiwa nyingine zote zitatozwa.
Makanisa na nyumba ya ibada yatasamehewa, ila nyumba nyingine kama zipo eneo la kanisa ambazo hazitoi huduma ya ibada, labda ni ofisi ama nyumba za kuishi watumishi wa Mungu, zitatozwa.
Kodi hii itasaidia mengi, kwanza kwa TRA hakuna paper work, itarahisisha makato na kuondoa ulimbikazi wa madeni, Serikali itapata kodi yake kwa wakati.
MWAKILISHI WA BUNGE
Mbunge wa Busega Simiyu, Mhe. Simon Songwe
Mapendekezo ya sheria hii yamepitishwaa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu June 22, mwaka huu ililetwa na Waziri ikaenda kamati ya bunge. Concern za Waziri zilikuwa nyingi na kuhitaji serikali kubadili mfumo.
Kumsaidia mwananchi kusahau na kuondokana na penati, Serikali ilikuwa haikusanyi mapato ya kutosha kupitia kodi hii ya majengo.
Hii itasaidia sasa kupunguza gharama kwa mwananchi badala ya kusaifiri kwenda TRA kutafuta control number na kulipa, itapunguza gharama za ufuatiliaji kwa serikali, itasaidia kukusanya fedha hizi kwa wakati
Ni sehemu ya jukumu letu kama wabunge kuendelea kuwaelimisha wananchi, sisi tutaendelea kuwaelimisha wananchi lakini pia TRA waendelee kutoa elimu. Sisi sote ni Watanzania na nchi yetu itajengwa na Watanzania wote. Kodi ni jukumu la mwenye nyumba, wasiwanyanyase wapangaji.
MWAKILISHI WA TANESCO
Meneja Mkuu Huduma kwa Umma, Martine Mwambene
Kodi hii hakuna fungu linalokuja TANESCO bali tunashirikiana na Serikali kukusanya pesa hizo, lakini kuna asilimia flani inakwenda TAMISEMI.
Nyumba moja yenye luku 2, kwa kuanzia kwa sasa mita zote ziwekewe, kisha baadae wenye nyumba watasema luku ipi itumike kulipia kodi hii.