PART THREE:
Elimu Mafunzo kwa Kutumia Teknolojia
Kwa masomo yanayohitaji vitendo mfano kilimo, ufugaji na uzalishaji, yafanyike kwa vitendo kwa yale yanayohitaji kuona, yafanywe kwa kuangalia na yale yanayohitaji ushirikishwaji yafanywe kwa kushiriki.
Kutokana na mfumo wa kujiendesha kwa kuzalisha na kuwekeza shule zitakuwa zinajihusisha na Kilimo, Ufugaji na uzalishaji mwingine kwenye viwanda n.k. hivyo kuna uwezekano wa baadhi ya sehemu za mashamba au uzalishaji ukawa mbali na mazingira ya shule, mfano kilimo cha Korosho kinaweza kupatikana Pwani, cha Kahawa Kagera na Michikichi Kigoma.
Hivyo sio ajabu makao makuu ya shule yakawa mkoa mmoja ila miradi mingine ikawa katika mikoa tofauti ambapo kwa zamu wanafunzi wakawa wanasafiri kwenda sehemu hizo kwa miezi kadhaa ili kupata elimu ya zao, na ufugaji husika.
Wanafunzi hao bado watahitaji kupata mafunzo yao mengine yaliyopo kwenye mitaala, kwa kutumia teknolojia.
Ni rahisi sana kwa mwalimu kutoa somo akiwa mkoa mwingine na mwanafunzi akapata somo hilo kama vile wapo kwenye chumba kimoja, hivyo kupelekea wanafunzi hao kutokupoteza au kuachwa nyuma.
Kuna masomo kama historia ni rahisi kwa mtu kuelewa na kutokusahau kwa kuona na kuangalia kuliko kusoma tu kwenye vitabu…, sio ajabu kwa kijana kukumbuka hata soksi alizokuwa amevaa mcheza sinema aliyoiangalia miaka kumi iliyopita ila asikumbuke wala kujua Kinjekitile alikuwa nani na alifanya nini, hivyo kwa kuelimisha kwa njia zote, kusikiliza, kuona, kufanya na kusoma kutasaidia sana kwa wanafunzi hawa kuelewa na sio kukariri.
Kuna masomo kama hesabu yanayohitaji misingi, yaani kama vile ambavyo huwezi kuezeka bati kabla ya kujenga msingi na kuta ndivyo hivyo huwezi kufanya hesabu za maumbo vizuri bila kujua magazijuto au algebra. Kwahio kwa masomo kama hesabu ni vema mtu akaendelea na topic/somo linalofuata pindi tu ikihakikishwa kwamba ameweza kuelewa na ku-master misingi. Jambo la kutokuwa na misingi bora limepelekea watu wengi kuchukia hesabu na kuona hesabu ni ngumu kumbe tatizo ni kuwa na misingi mibovu, hivyo hata wakipata waalimu bora huko mbeleni ni vigumu kufanikiwa sababu ya misingi mibovu…, huwezi kujenga Ghorofa kwenye msingi wa Banda la kuku!!!
Hivyo kwa kutumia videos/ conference na mitandao mwalimu mmoja ataweza kuwahudumia wanafunzi wengi iwezekanavyo na kwa wakati tofauti na muda mwingi utatumika kwa wanafunzi kufanya mazoezi ili kuhakikisha wameelewa na sio kukariri.
SEHEMU YA KWANZA; Shule zinazojiendesha kwa Faida kwa Kuzalisha bila Kutegemea Michango / Karo
Mpaka sasa shule ni sehemu za watu kupata elimu na mafunzo, mashule mengi yamekuwa yakitoa mafunzo ya kinadharia bila vitendo. Ni rahisi sana kubadilisha mfumo huu wa kinadharia na kuwa wa vitendo na kuhakikisha shule hizi zinajitegemea na katika kujitegemea huko inawafundisha wanafunzi kuzalisha na kujipatia mahitaji yao na ya jamii, hivyo kupelekea shule hizi sio tu kutoa mafunzo bali kutengeneza bidhaa zinazohitajiwa na jamii.
Baadhi ya vitu vitakavyofanyika ili kuhakikisha kujitegemea huku ni kuwekeza katika sekta zifuatazo
A. KILIMO NA UFUGAJI
Ili shule ziweze kujitegemea inabidi zikidhi mahitaji yao muhimu ya chakula kwa kuwa na kilimo na ufugaji. Kwa kutumia wingi wa wanafunzi na mashine na teknolojia kazi ya kilimo ambayo huwa mara nyingi ni ngumu na ya kuchosha inaweza ikafanyika kwa wepesi na kwa kusaidiana. Hivyo ni muhimu kwa shule hizi kuwa na wanafunzi wengi wa kutosha kuweza kupeana zamu katika masomo, uzalishaji na kilimo na ufugaji.
Tanzania ni nchi iliyobalikiwa kuwa na maeneo makubwa ya ardhi. Hivyo kuliko mashule kubabana mijini mengine hata hayana viwanja vya michezo vya wanafunzi, ni heri kuwe na shule chache ila kubwa za kuweza kuchukua wanafunzi wengi iwezekanavyo na ziwe kwenye maeneo makubwa ambayo yataweza kuwekeza kwenye mashamba ya kisasa na ufugaji ambayo zaidi ya kuzalisha chakula cha kujilisha watapata kingine cha kuuza. Ufanyaji kazi huu na kuongezea thamani bidhaa zitakazouzwa itakuwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa vijana.
Ingekuwa ni enzi zile za kilimo cha jembe la mkono ingewanuia vigumu sana wanafunzi kuweza kufanya kazi hizo ngumu na za suluba na kupata muda wa kusoma kwa umakini, ila kwa dunia ya sasa ya kilimo cha matreka na uvunaji wa mashine (harvester), kazi sio ngumu na wingi wa wanafunzi utasaidia kwa wanafunzi hawa kupata muda wa shift hata kama ni mara moja au mbili kwa wiki kuweza kupata elimu mashambani na wakati huohuo kuzalisha. Na kwa matumizi ya gesi asilia shule hizi zitahakikisha hazina gharama za nishati na wakati huo huo kutunza mazingira.
Kwa kuwa na maeneo makubwa shule moja inaweza ikashiriki katika kilimo na ufugaji wa mazao na mifugo mbalimbali ili kijana akimaliza elimu yake ya sekondari atakuwa na ujuzi wa kilimo cha aina zote. Pili shule hizi badala ya kupanda na kuvuna mazao kwa mbegu zilezile itakuwa ni fursa nzuri ya kufanya uchunguzi wa mbegu imara na jinsi ya kuzidisha mavuno.
Hii itakuwa fursa kwa shule kuwafundisha taifa la kesho kilimo cha kisasa, kilimo cha umwagiliziaji na kilimo endelevu ambacho hakina athari kwa mazingira.
Umwagiliziaji huo unaweza kwenda sambamba na uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya maji kwa kutumia baadhi ya maji ya kufulia na kuogea katika umwagiliziaji.
Kilimo hiki kitahakikisha mazao ya chakula kwa kuhakikisha wanafunzi na waalimu wanajilisha na kuuza ziada, pia mazao ya biashara ili kujipatia kipato. Mbinu za kilimo zinaweza kuwa intensive farming (ili kuhakikisha mazao mengi yanapatikana katika sehemu ndogo iwezekanavyo) na uchafuzi wa mzingira ambao ungeweza kutokea kutokana na na aina hii ya kilimo, mabaki na uchafu wa kilimo hiki na ufugaji yatatumika katika kutengeneza gesi asilia na mbolea.
Ufugaji mbali ya kuwa wa wanayama unaweza kuhusisha mpaka ufugaji wa Samaki mpaka nyuki wadogo, hii ni kuhakikisha mwanafunzi anapata mafunzo ya vitendo kwenye kila aina ya kilimo.
Kwa kujitegemea kwa chakula na kuuza ziada kutaleta faida ya kupunguza gharama za chakula, kupata faida kwa kuuza ziada na kutoa mafunzo ya kilimo kwa wanafunzi ambao mwisho wa siku wakihitimu watayatumia katika maisha yao ya ukubwani.
B. MATUMIZI BORA YA NISHATI NA UVUNAJI WA NISHAJI
Nishati ni muhimu sana katika uzalishaji wowote katika jamii, kwa nchi ya tropiki kama Tanzania yenye jua la kutosha inasikitisha sana kuona nishati hio haitumiki ipasavyo, kwahio pamoja na kutumia solar katika matumizi ya taa, ili kupunguza gharama za nishati, pia nishati ya jua inaweza kutumika kwenye pump za kusaidia kupump maji wakati jua linawaka ili yaje yatumike katika umwagiliziaji, hii itasaidia sana kurahisisha nguvu kazi.
Pia kwa kuhakikisha uchafu wote wa chooni, mabaki ya chakula na mifugo yanatumika katika kutengeneza gesi asilia kutapunguza gharama ya kupika kwa kutumia nishati mbadala kama kuni. Kwa kufanya haya shule hizi sio tu zitapunguza gharama za kujiendesha bali vilevile zitakuwa, zinaonyesha njia ya kutunza na kujali mazingira. Na sababu utamaduni huo utakuwa unafundishwa kwa watoto ambao ni taifa la kesho hii itahakikisha na kujenga utamaduni kwa taifa hili la kesho kujali mazingira.
C. VIWANDA VYA BIDHAA NA USINDIKAJI
Ili kuongeza thamani na kuweza kuuza bidhaa kwa wahitaji ni muhimu kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinawekwa katika utayari wa kuingia sokoni. Yaani zinakuwa na viwango vinavyohitajika na kukubalika na soko.
Tukichukulia mfano wa viwanda vya china ambavyo vipo (adaptive) vinaweza kubadilika kutengeneza mambo tofauti kulingana na mahitaji. Kwa kuwa na viwanda vya "assembling and packing" itakuwa rahisi kwa bidhaa nyingi kuweza kupakiwa na kuwa tayari kwa matumizi ya wateja.
Kwa kufanya hivi pamoja na kuzipatia vipato shule, kukidhi mahitaji ya jamii, itakuwa pia ni elimu tosha kwa wanafunzi ambao watakuwa wanajifunza kwa vitendo kila kinachofanyika uraiani na ambacho watakuwa wanakifanya au watakuja kukiboresha siku wakiingia mtaani.
Mafunzo haya ya uzalishaji katika viwanda hivi yatategemea na uhitaji wa jamii, iwapo bidhaa za ushonaji, furniture n.k. zinahitajika katika jamii basi shule husika zitakuwa na karakana zinazofanya uzalishaji huo pamoja na kutoa mafunzo.
Wanasema hakuna mwalimu bora kama uzoefu, na kwa kupata vijana ambao kuanzia wadogo mpaka wanapokuwa vijana watakuwa wanafanya kila kinachotakiwa, wanachokipenda na watakachokifanya baadae ni ukweli usiopingika kwamba watakuwa na uzoefu na uelewa wa kila tatizo na changamoto za mnyororo mzima hivyo kuwa na ufahamu wa jinsi ya kuboresha mfumo mzima.
D. MAFUNZO YA SANAA, MICHEZO NA KUKUZA VIPAJI
Michezo na Sanaa ni Sekta yenye faida na yenye kuzalisha pesa nyingi duniani, watoto wengi wanavipaji ambavyo havitambuliwi na kama vingeweza kuendelezwa vingeleta faida kwa jamii.
Kwa kufundisha Sanaa, michezo na kukuza vipaji shule hizi zitakuwa na fursa ya kuweza kutambua wenye vipaji na kuvikuza na mwisho wa siku wachezaji hao wakichukuliwa na timu nyingine (kuuzwa) au wakishinda kwenye matamasha shule hizi zitapata fursa ya kupata kipato na faida. Ni kweli katika kufundisha watoto wengi huenda usipate hata mmoja ambaye ataweza kuuzwa na kuleta faida ila ukizingatia nia itakuwa sio kutengeneza pesa pekee, bali kukuza vipaji, hivyo hata asipopatikana mchezaji wa kuuzwa na kupata faida itakuwa sio hasara.
Kwa wanamichezo hawa kushiriki katika mashindano na ligi za mpira itakuwa rahisi kwa wahisani na watu wenye matangazo kuwapa ufadhili.
Pia inashauriwa shule ziwe na timu ambazo zitaingia katika mashindano ya ligi ya nchi husika kwa kufanya hivyo wanafunzi wenye vipaji wataweza kuonekana, shule zitatoa burudani ya mashindano na watu kuweza kuangalia na kulipia hivyo kupata kipato, kwahio shule zitashauriwa zitengeneze timu ambazo zitakuwa na uwezo wa kupambana kwenye mashindano tofauti, na masomo mengine yataendelea sambamba na mafunzo ya michezo, ukizingatia teknolojia ya sasa sio vigumu kwa wanafunzi hao kupata elimu wakiwa sehemu yoyote au muda wowote.
Kazi za Sanaa pia zinapendwa sana, mfano tamthiliya nyimbo n.k., kwa kuwahusisha wanafunzi kuanzia wadogo katika utunzi na kuigiza itakuwa ni kukuza vipaji vya wanafunzi hao. Vilevile kwa kutoa na kuuza kazi hizo kwenye studios, television na kwa jamii ili iweze kutazama na kununua itakuwa pia ni njia ya shule hizi kujipatia kipato.
E. SHULE KAMA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII INAYOTOA KIANZIO KWA
WAHITIMU
Ingawa tumeeleza kwamba elimu itakuwa ni ya gharama ndogo kwa mzazi kuhakikisha kwamba anamudu na wasio na uwezo pia wanasoma, ila michango kutoka kwa wazazi italeta uwajibikaji kwa wazazi kuhakikisha wanaweza kuhudumia familia na wanafuata uzazi wa mpango.
Michango hii ya wazazi kila mwezi na mwaka badala ya kutumika kuendeshea shughuli za kila siku za shule na kulipa mishahara itatumiwa na shule kama mifuko ya wanafunzi na kuwekezwa ili ipate faida na kila mwanafunzi akihitimu sekondari atapewa kama kianzio cha kuweza kuwekeza na kumsaidia katika maisha yake ya uraiani.
F. SHULE KAMA CHANZO CHA AJIRA
Kwa shule kuwa na miradi mingi sehemu tofauti na vilevile kuwa na uwezo wa kuzalisha watu wenye ujuzi na vipaji tofauti, watakuwa katika nafasi nzuri ya kujua na kushauri muhitimu fulani afanye nini, kama ajiajiri au apachikwe sehemu fulani kusimamia au kufanya uzalishaji wa aina fulani.
Kwa ufupi shule hizi zitakuwa katika nafasi nzuri ya kushauri na kusaidia nguvu kazi hizi ni wapi zitumike kwa manufaa ya kijana mwenyewe na jamii kwa ujumla.
Itaendelea na Sehemu ya Pili ; Utatuzi wa Changamoto