*Ni wa nafasi ya mwenyekiti wa chama Mkoa Mara
*Ukumbi wageuka uwanja wa mapambano, viti vyarushwa
*Msimamizi avunja mkutano, aahirisha uchaguzi
Na Raphael Okello, Bunda
UCHAGUZI Mkuu wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mara jana ulivunjika baada ya wagombea kuchapana makonde ukumbini mbele ya wasimamizi wa uchaguzi baada ya kutokea kutofautiana katika kipengele cha katiba ya uchaguzi.
Wagombea hao wa nafasi ya Mwenyekiti Mkoa wa Mara, Bw. Machage Machage ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Tarime na Bw. Mwita Mikwabe ambaye ni Mkurugenzi wa Sera na Uenezi CHADEMA, walitofautiana msimamo katika moja ya kipengele cha katiba ya uchaguzi ambacho kinamtaka mshindi kufikisha nusu ya idadi ya kura za wajumbe halali baada ya kutakiwa zirudiwe kati yao ili mshindi halali apatikane.
Vurugu hizo zilianza baada ya kipindi cha awali cha kuhesabu kura kumalizika ambapo msimamizi wa uchaguzi huo, Bw. Charles Mwera ambaye ni Mbunge wa Tarime na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kutangaza kuwa katika nafasi zote zilizogombewa, isipokuwa Ukatibu, hakuna mgombea aliyefikisha nusu ya kura ya wajumbe.
Kwa mujibu wa katiba ya uchaguzi wa chama hicho, wagombea wawili wa kwanza walioongoza kwa idadi kubwa ya kura, walilazimika kurudia ili kupata mshindi halali.
Msimamo huo wa Bw. Mwera kusimamia katiba ulionekana kuwakera baadhi ya wagombea na wapambe wao hususan wale walioongoza kwa idadi ya kura katika awamu ya kwanza ambapo Bw. Machage aliongoza kwa kura 26 huku Bw. Mwikwabe akiwa na kura 24 na Bw. John Koyi akikusanya kura 14 kati ya 64 za wajumbe halali.
Baada ya malumbano marefu, mkutano ulifikia muafaka na upigaji kura kurudiwa kwa nafasi zote ambapo wakati shughuli ya kuhesabu kura awamu ya pili ikinaendelea, Bw. Machage na wapambe wake walionekana kumsonga songa Bw.
Mwikwabe kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono katiba iliyosababisha kura hizo zirudiwe.
Akionekana kupandwa jazba, Bw. Machage alimfuata Bw. Mwikwabe aliyekaa upande wa pili wa ukumbi na kumrushia makonde na kumshambulia kwa viti ambapo alikwepa kwa kusaidiwa na baadhi ya wajumbe.
Kutokana na vurugu hizo, kabla ya kusoma matokeo ya awamu ya pili, Bw. Mwera alisimama na kuahirisha uchaguzi huo hadi utakapotangazwa tena ambapo aliwaeleza wajumbe kuwa yeye hawezi kuendelea kusimamia uchaguzi ambao unakiuka katiba ya chama kwa maslahi ya watu binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhairisha uchaguzi huo, Bw. Mwera ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la CHADEMA, alisema alitumwa na uongozi wa chama hicho ili asimamie uchaguzi kwa kuilinda katiba.
Alinukuu kanuni ya uchaguzi wa CHADEMA ibara ya 6:3:1(C) kinachomtaka mgombea atangazwe mshindi kwa kufikisha nusu ya idadi ya kura za wajumbe halali waliopiga kura.
Nimesikitika sana kuona viongozi wanaotakiwa kuongoza watu wanakuwa na utovu wa nidhamu kwa kuvunja katiba ya chama kwa sababu hiyo imenilazimu kuahirisha uchaguzi huu wa viongozi hadi itakapotangazwa tena na chama,alisema Bw. Mwera.
Kuhusu malalamiko ya baadhi ya wagombea na wajumbe kwamba chaguzi zingine za viongozi
wa chama hicho ngazi ya matawi, kata na wilaya zilikiuka kanuni, Bw. Mwera alisema hana ushahidi huo na kudai kuwa hata kama zilikiuka katiba si kigezo cha kukubali kuvunja katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sababu ya kutotaka kipengele hicho cha katiba kutumika katika uchaguzi huo, Bw. Machage alidai kuwa katika chaguzi zote za kuwapata viongozi wa ngazi ya tawi, kata na wilaya mkoani humo walishindi walitangazwa kwa kufuata wingi wa kura na kwamba haikuwa lazima kufikisha nusu ya kura za wajumbe wote na kudai kuwa wasimamizi hao, walilenga kumhujumu.
Kama wasimamizi wa uchaguzi huu wa leo hawawezi kuwatangaza washindi walioongoza kwa idadi kubwa ya kura hadi wafikishe nusu za kura za wajumbe wote basi hata chaguzi zingine za ngazi ya chini zilivunja katiba nazo ni batili zirudiwe ! Alilalamika Bw. Machage.
Naye Bw. Mwikwabe ambaye awali aliwahi kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga aliyejiunga na CHADEMA wakati wa kampeni ya uchaguzi mdogo Jimbo la Tarime kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, marehemu Chacha Wangwe, alisema suala muhimu ni kuzingatia katiba.
Alieleza kusikitishwa na baadhi ya wajumbe na wagombea kushabikia kile alichosema uvunjaji katiba katika chaguzi ndani ya chama hicho.
Kutokana na sakata hilo baadhi ya wajumbe waliohudhuria uchaguzi huo walieleza kusikitishwa na vitendo hivyo na kueleza kuwa kimechafua chama kwa kuzingatia kuwa kila siku CHADEMA kimekuwa makini na kusisitiza maadili mema.
Waliitaka Kamati ya Maadili kuchunguza chanzo cha vurugu hizo na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watakaobainika kuhusika.
SOURCE: Majira