Home
*BAADHI WAGOMEA WASTAAFU, WADAI MAELEZO
Waandishi Wetu
UAMUZI wa kumwondoa Zitto Kabwe kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya mwenyekiti wa Chadema, umeanza kukitikisa chama hicho baada ya wazee waliokutana jana jijini Dar es Salaam kugawanyika katika makundi mawili.
Zitto, 33, alikitingisha chama hicho alipoamua kupambana na mwenyekiti Freeman Mbowe kuwania nafasi hiyo ya juu kwenye chama hicho, lakini akatangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kuheshimu ushauri wa wazee kuwa uamuzi wake ungesababisha chama kuvunjika.
Lakini habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa baadhi ya wazee wanaomuunga mkono mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini wamepinga uamuzi wa kumshauri Zitto ajiondoe kugombea uenyekiti kwa madai kuwa halitambui kikao kinachoitwa cha wazee wastaafu, wakati kundi jingine linaunga mkono uamuzi huo.
Wazee hao jana walikutana jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine, kumchagua mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa.
"Mimi na wenzangu hatutambui baraza lililomwengua Zitto kugombee nafasi ya mwenyekiti. Katiba yetu iko hovyohovyo sana kwa kuruhusu suala hilo," alisema mmoja wa wazee wanaopinga uamuzi huo ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
"Baraza linalotambuliwa kikatiba ni hili linalokutana leo (Baraza la Wazee la Taifa) na sio waasisi na wazee wastaafu wa chama," alieleza.
Taarifa kutoka kwenye mkutano huo zilieleza kuwa kutokana na kutoridhishwa kwao, baadhi ya wazee wakiwamo wa kutoka Ruvuma wameandaa barua kwenda kwa mwenyekiti wa chama hicho siku ya mkutano mkuu baada ya kukosa fursa kutoa dukuduku lao jana.
Kwa mujibu wa habari hizo, wazee hao wanadai kuwa Zitto aliondolewa kimizengwe kwa sababu ya maslahi ya watu wachache wa chama. Wanadai kuwa muundo mzima wa chama kuanzia kwa Mtei hadi kwa Mbowe umefinyanga demokrasia.
Wakati kundi hilo likipinga uamuzi huo, lingine limebariki likisema ni sahihi Zitto kuondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa kuwa uamuzi wake kugombea nafasi hiyo ulianza kukigawa chama.
"Ule uamuzi ni sahihi kwani tulishafikia mahali tukagawanyika, lakini sasa tumerudi kuwa wamoja," alisema mzee mwingine anayeunga mkono uamuzi huo.
Hata hivyo, katiba ya Chadema toleo la mwaka 2006, kipengele cha mabaraza haikuwataja wazee wastaafu na waasisi wa chama kuwa sehemu ya jumuiya za chama hicho.
Lakini katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kuwa kitendo cha baraza la wazee kukaa na kuamua mvutano kati ya Mbowe na Zitto ni kwa mujibu wa katiba hiyo, kifungu cha 5(1)5.
Kwa mujibu wa kifungu hicho wazee wana haki ya kukaa na kuamua maamuzi ya nani agombee uenyekiti kwa maslahi ya chama.
Alisema kuwa kikao kiliongozwa na mwenyekiti wa kwanza wa Chadema, Edwin Mtei, Balozi Christopher Ngaiza, Profesa Mwesiga Baregu, Bob Makani na mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo akisaidiana na ofisi ya katibu mkuu.
Alisema baada ya kukaa katika kikao hicho walimshauri Zitto asigombee kwa ajili ya maslahi ya chama, lakini pia kwa ajili ya kudumisha mshikamano ndani ya chama.
Alisema kwa kuheshimu demokrasia kikao hicho kilifanyika kwa wazi bila mizengwe yoyote na baada ya kikao Zitto aliandika barua kwa katibu mkuu akieleza kuwa ameamua asigombee ili nafasi hiyo ibaki kwa mgombea mmoja ambaye ni Mbowe.
Kwa mujibu wa kikundi kinachounga mkono kuondolewa kwa Zitto, kitendo hicho hakina mkono wowote wa watu kutumiwa bali kimefikiwa kulinda maslahi ya chama.
Wakati wazee hao wakivutana mmoja wa waasisi wa Chadema aliyeshiriki kikao cha kumwondoa Zitto kwenye kinyang'anyiro cha uenyekiti, Bob Makani amekiri kwamba wazee walifinyanga demokrasia katika kufikia uamuzi huo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Makani ambaye alikuwa mwenyekiti wa pili wa Chadema, alisema demokrasia ina ukomo wake kwani inaweza kudhibitiwa pale inapoonekana kwamba itasababisha mtafaruku.
"Demokrasia ina ‘limit' (ukomo), huwezi kuiachia pale 'interests' (maslahi) za chama zinaposababisha athari," alieleza Makani ambaye aling'atuka madarakani na kumpisha Mbowe.
Kwa mujibu wa Makani kwa mazingira ilipofikia hoja ya Zitto, ilikuwa lazima wazee kuingilia kati ili kuokoa chama n athari ambazo zingeweza kutokea baadaye.
Alisema jambo lililofanywa na Chadema si la ajabu kwani hata katika tawala za mataifa, serikali haziwezi kuachia mambo yaende kiholela eti kwa sababu ya demokrasia.
Wakati Makani akisema hayo mhadhiri mwandamizi wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma (PSPA) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema Zitto alikurupuka kugombea uenyekiti.
Dk Bana alisema Zitto alitaka kutengeneza joto na presha ya kisiasa kuuhadaa umma kwamba kuna demokrasia ndani ya Chadema.
Naye Profesa Abdallah Safari alisema kitendo cha Zitto kujiondoa kimedhihirisha wazi kuwa sera na utamaduni wa chama hicho ni kuachiana madaraka.
Pia alisema hoja aliyotoa Zitto ya kukinusuru chama ili kisigawanyike ni kudumaza ukuaji wa misingi bora ya demokrasia ya kweli nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Profesa Safari alisema wazee wa chama hicho wameonyesha udhaifu mkubwa katika kukuza demokrasia hiyo.
"Wazee wa Chadema wamekosea, hivyo ni wazi sasa watangaze kuwa sera na utamaduni wa chama chao ni kuachiana madaraka na si vinginevyo," alisema Prof Safari ambaye aliangushwa na Prof Ibrahim Lipumba kuwania uenyekiti wa CUF. Habari hii imeandaliwa na Musa Mkama, Leon Bahati, Salim Said na Sadick Mtulya.
Contact Us DISCLAMEREmail:webmaster@mwananchi.co.tz© Mwananchi Communications Ltd 2006- 2009