SoC01 Kuleta maendeleo kwenye jamii ni jukumu la nani?

SoC01 Kuleta maendeleo kwenye jamii ni jukumu la nani?

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Sep 22, 2021
Posts
1
Reaction score
0
Nilipokuwa mdogo niliwaza na kufikiri kuwa, swala la kuleta maendeleo (mabadiliko) kwenye jamii ni jukumu la serikali na matajiri pekee. Nilihisi wao pekee ndio wenye nguvu ya kufanya hivyo. Mpaka leo mawazo haya yapo kwa baadhi ya watu ikiwemo vijana. Wengi wetu uhisi kuwa kuna kikundi fulani cha watu ndio wanaostahili kuleta maendeleo na kusukuma gurudumu la mabadiliko kwenye jamii, kutokana na nyadhifa au uwezo waliokuwa nao kiuchumi. Leo hii mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Twitter, Instagram na TikTok imejaa mashabiki na watumiaji ambao kazi yao kubwa ni kuleta masihara, mizaha, umbea na udaku. Vijana wengi wa leo tupo kwenye hili kundi tukipoteza muda mwingi pamoja na mali (bando la intaneti) tukiamini kuwa tunaenda na wakati.

Wengi wetu tumeridhika na kidogo tunachokipata na kuacha akili zetu zigande mitandaoni, kisha kuigiza yale yote yanayofanywa na watu maarufu (hata kama ni mabaya na ni kinyume na maadili). Leo hii maswala kama ushoga, usagaji, madawa ya kulevya, kucheza na kuigiza video za utupu, ukahaba na ulevi yamekuwa ni mambo ya kawaida kwenye jamii ili hali kuwa kinyume na maadili na utamaduni wa kitanzania na kiafrika. Kizazi cha leo kimekuwa cha ovyo, kisicho na maadili huku vitendo vya kigaidi, uharamia na tabia mbaya vikishamiri kwenye kila pembe ya dunia na hata kwenye taifa letu. Kwa mienendo hii, taifa haliwezi kupata mabadiliko chanya yenye kuleta maendeleo.

Hivi sasa nimejitambua, hata wigo wangu wa kufikiri umepanuka. Nimegundua yakua swala la kuleta mabadiliko na maendeleo kwenye jamii ni la kila mmoja wetu. Kwa kutambua hili, napaza sauti kumuhamasisha kila mmoja nikiweka mkazo hususani kwa kijana wa kitanzania na kiafrika. “KIJANA AMKA”, funga mkanda anza kupambana. Bila mimi na wewe hakuna maendeleo. Bila juhudi zako mimi na wewe hakutakuwa na maendeleo. Embu fikiria maisha yangekuaje leo kama kusingekuwa na maendeleo? Fikiri, ungekula nini leo kama trekta na jembe visingekuepo? Fikiri, ungeendaje nchi za nje kama ndege zisingekuepo? Fikiri, ungefanyaje kazi kwa urahisi kama tarakirishi (kompyuta) zisingekupo? Ni wazi kwamba maisha yangekua magumu sana. Sasa tufanyaje ili kuhakikisha kila mmoja wetu anashiriki kwenye kuleta mabadiliko chanya yenye kuleta maendeleo ya taifa? Yafuatayo, ni baadhi ya mapendekezo ya nini kifanyike kwenye kila sekta;

Sekta ya uchumi na biashara ya Tanzania inahitaji mawazo thabiti yenye kujenga na kuleta mabadiliko ili taifa lisimame kiuchumi. Tunahitaji sera makini za uchumi na biashara zinazosindikizwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ili Tanzania isimame kiuchumi na kibiashara ni lazima tuwe wabunifu na tufanye uvumbuzi. Ubunifu na uvumbuzi ni chachu ya mabadiliko chanya yanayoleta maendeleo kiuchumi. Biashara pia ziendeshwe kidijitali ili kuteka masoko ya mbali, kuongeza ufanisi na kujenga wigo mpana wa biashara

Katika sekta ya afya na maendeleo ya jamii, vijana na wananchi wote tunajukumu la kujilinda na kuwalinda wengine kiafya. Tunaweza jilinda kwa kuacha kufanya vitendo hatarishi kama ngono zembe, utumiaji wa dawa za kulevya na ulevi. Kwa kufanya hivi tutalinda afya zetu na za wale wa karibu yetu. Kwenye swala la usambazaji wa taarifa, sote tuepuke kusambaza taarifa au uvumi usio na uthibitisho wa kitaalamu ambao utaharibu imani ya watu kwenye swala fulani kiafya, mfano hai tulio nao ni swala la chanjo ya UVIKO 19. Kwa kufanya haya, tutaweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, kwenye sekta ya afya na kwa kila mtanzania.

Kila mwananchi anaweza kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo kwenye utawala bora kwa kuwajibika. Kila mmoja akisimama kwenye nafasi yake na kutekeleza majukumu yake kuna nafasi kubwa ya kuleta maendeleo maana uzalishaji utaongezeka na viongozi wa nchi itawarahisishia kutekeleza miradi mikubwa ya nchi kwa ufanisi na ustadi. Wananchi tukishirikiana na serikali kufanya kazi na kuzalisha, tutajenga Tanzania yenye utawala bora wenye nguvu, mamlaka na utajiri zaidi ya mataifa mengine

Ili kujenga na kuleta mabadiliko chanya kwenye demokrasia, kila raia ana jukumu la kutenda kwa haki. Kutii bila shuruti kutaleta amani na utulivu. Kila mmoja wetu akizingatia usawa na kulinda haki za binadamu tutajenga demokrasia iliyo chachu ya maendeleo.

Kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na umwagiliaji mabadiliko chanya yatapatikana endapo tutatumia njia za kilimo zilizo rafiki na mazingira. Kila kilimo ni lazima kiendeshwe kwa njia za kisasa ili kukifanya kuwa endelevu. Kutumia sayansi ya kilimo na teknolojia imara kutasaidia kuboresha kilimo ikiwemo kuzalisha vyakula vyenye virutubisho sahihi kwa ajili ya ukuaji wa mwili. Uwekezaji kwenye kilimo uongezwe ili kuongeza ajira kwa vijana ambao wengi wetu tumekumbwa na wimbi la ukosefu wa ajira. Vijana tubadili mtazamo na fikra zetu juu ya swala la ajira na badala yake tuongeze nguvu kazi kwenye kilimo maana ndio uti wa mgongo wa taifa letu na ni ajira nzuri kwa mstakabali wa maisha yetu.

Matumizi mazuri ya mitandao. Ili kuleta maendeleo na mabadiliko chanya kwenye jamii, sote tuna jukumu la kufanya juu ya matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii. Mitandao ya kijamii isitumike kwa ajili ya burudani na udaku pekee. Kurasa za udaku na umbea zisiwe kipaumbele cha watu kutumia mitandao ya kijamii, badala yake mitandao hii itumike kuleta faida. Swali ni je, mitandao ya kijamii inawezaje kutumika kuleta faida za kimaendeleo? Mitandao ya kijamii huweza mletea mtu faida za kimaendeleo kwa sababu inasambaza taarifa kwa umati mkubwa kwa kutumia mda mchache. Unaweza tangaza biashara kwenye mitandao ya kijamii ikawafikia watu tofauti tofauti waliopo ndani na nje ya nchi. Tunaweza tumia mitandao hii kukuza biashara zetu na kuonyesha watu shughuli za maendeleo tunazofanya. Biashara za mitandaoni ni biashara zinazotembea, zisizokuwa na gharama kubwa sana ya kuendesha na huleta faida kubwa. Wengi wamekuza biashara zao kwa kuuza mitandaoni. Mitandao ya kijamii kama Youtube, itumike kujifunza ujuzi mbali mbali kama urembo wa mekapu, kutengeneza nywele, kushuti video, mapishi, ujenzi, upambaji pamoja na shughuli zingine za ujasiriamali kwa ajili ya kujiongezea kipato. Kwa kujifunza ujuzi mbalimbali mitandaoni, tutakuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe na kujijenga kiuchumi. Hivyo, vijana wenzangu tuamke, wakati wa kujenga Tanzania yetu ni sasa, tusikeshe mitandaoni kwa ajili ya udaku pekee, tuamke tufanye kazi na tuzalishe kupitia mitandao (WatsApp, Twitter, Instagram, Tiktok, Youtube).

Dira ya kutuvusha na kutuongoza katika kusukuma gurudumu la maendeleo ni kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals- SDGs). Malengo haya yanatuhimiza sote kuwa chachu ya kuhakikisha tunatekeleza kutokomeza umaskini, kutokomeza njaa,kuleta afya bora na ustawi wa jamii, kutekeleza elimu bora, kujenga usawa wa jinsia, kutunza mazingira, kupunguza matabaka, kulinda uhai wa viumbe vingine na kuhakikisha maji yanakuwa safi na salama.

Kwa kutumia muongozo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu tunaweza kuleta mabadiliko chanya yenye kuleta maendeleo katika jamii kwenye sekta zote. Kila mmoja wetu analazimika kujua hatua za kuzingatia ili kupata maendeleo kulingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Maendeleo huja kwa hatua na hatua zifuatazo ni muhimu kufuatwa ili kuleta mabadiliko na maendeleo popote. Kwenye hatua ya kuleta maendeleo na mabadiliko kwenye jamii, ni lazima tutambue ya kwamba, maendeleo yoyote au mabadiliko chanya hupatikana endapo kutakuwa na kujitambua, kujiamini, kuthubutu, uthabiti na maarifa.

Hatua ya kujitambua. Kuna umuhimu wa kila mmoja wetu kutambua nguvu na madhaifu aliyokuwa nayo. Nguvu tulizonazo zikiwekezwa juhudi zitaleta mabadiliko chanya nyenye kuleta maendeleo. Unapotambua udhaifu wako inakuwa rahisi kuomba msaada kwa wengine ili kuushinda huo udhaifu ambao pengine ungechangia kukuangusha. Hivyo, maendeleo yoyote huja pindi mtu anapojitambua na kushinda madhaifu yake.

Ukishajitambua, hatua inayofata ni kujisimamia na kujiamini. Kujisimamia na kujiamini kuwa unaweza kufanya na usipofanya wewe hakuna mwingine wa kufanya. Unapojiamini unajenga uwezo wa kupata fursa mbali mbali, kuzichangamkia kisha kuzifanyia kazi ili zizae matunda.

Uthubutu ni hatua inayofata baada ya kujiamini na kujisimamia. Ni lazima kuthubutu na kuchukua hatua ya kuleta mabadiliko chanya ili kuleta maendeleo. Kutositasita, kufanya kwa vitendo, kutekeleza na kuthubutu kufanya ndio silaha ya kuleta mabadiliko yenye kuleta maendeleo

Uthabiti huja baada ya kuthubutu. Ukishathubutu kufanya vitendo hatua inayofata ni kusimama thabiti kwenye kutekeleza shughuli za mabadiliko ili kuleta maendeleo. Kama ni jambo linakutaka ulifanye basi kulifanya kila siku ili lilete mabadiliko chanya. Kuwa thabiti ni hatua ya kutokuyumbishwa na jambo au changamoto yoyote itakayojitokeza

Maarifa ni jambo lingine linalokamilisha gurudumu la maendeleo. Ili uweze leta mabadiliko kwenye jamii ni lazima kuwa na maarifa ya ziada. Maarifa ni hazina ya mafanikio maana hutengeneza njia ya maendeleo. Maarifa huja kwa kusikiliza ushauri, kusoma vitabu mbali mbali na kujifunza kutoka kwa wengine. Maarifa ni hazina ya maendeleo na mafanikio, hivyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa kila mmoja wetu kwenye jamii, kutafuta maarifa kwa gharama yoyote ile ili yatujenge na kupanua wigo wa kufikiri na kupambanua mambo

Baada ya kujua hatua za kufanya ili kuleta maendeleo, na kuelewa ni kwa namna gani sisi sote tunaweza kushiriki kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa, nitoe rai kwa kila mmoja wetu kutekeleza haya ili tujenge Tanzania yetu na Afrika kiujumla. Sote tutambue ya kwamba hakuna maendeleo yanayokuja kwa kusubiri wengine wafanye. Tuwe kama mchwa ambao hufanya kazi usiku na mchana wote wadogo kwa wakubwa, wakihangaika huku na kule, wakishirikiana kujenga makazi yao ambayo badae huwasitiri. Na sisi tuwe zaidi ya mchwa, tufanye kazi usiku na mchana, wadogo kwa wakubwa bila kujali cheo, madaraka, nafasi uliyonayo kwenye jamii au wadhifa. Tufanye kazi mithili ya mchwa ili tujijengee nyumba yetu Tanzania ambayo itatusitiri sisi na vizazi vyetu vijavyo.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom