Kijiji hicho ambacho ni nadra sana kutembelewa na kila binadamu anaetamani kuendelea kuishi hata wanaotaka kujiua hawasogei, kimepata umaaurufu mkubwa ndani na nje ya nchi kikielezwa kuwa ni kitovu cha uchawi na wachawi wanaoweza kufanya miujuza.
Inaelezwa kuwa, ikifika usiku, Gamboshi hubadilika, inaonekana kama mmoja wa miji mikubwa Duniani, nyumba nyingi zenye ghorofa zaidi ya 50.
Kabla sija funga Safari ya kuelekea kijiji cha gamboshi nilimuuliza Rafiki yangu Mkazi wa Lamadi, wilayani Magu, Anthony alidai: “Gamboshi ni jiji la ‘masupastaa’ wa uchawi hawatakuachia ufike huko.
Nika mwambia acha imani potofu kesho naenda ili nika shuhudie mi mwenyewe tulipo kua njiani nikaanza kuona mauza mauza ya kwanza Kutoka Bariadi mjini ni lazima upitie kijiji cha Ngulyati kiasi cha kilometa 30 Mashariki ya Bariadi katika barabara itokayo Bariadi kwenda Magu. Hakuna kibao kinachotambulisha Kijiji cha Gamboshi mwanzoni mwa barabara inayoelekea Gamboshi kuanzia Ngulyati. Watu walikuwa wengi katika kilometa 5 za awali kuelekea Gamboshi, lakini idadi ikazidi kupungua kwa namna tulivyozidi kukikaribia kijiji hicho. Barabara ilikuwa tupu hadi kilometa tano kukufikia Gamboshi hali ambayo ilianzisha hofu mpya kwangu. Nyumba nzuri mfano wa shule za kisasa za ‘English Medium’ ilionekana kuvutia macho kilometa chache kabla ya kukifikia Kijiji cha Gamboshi. “Ile ni shule ya Serikali au ya mtu binafsi,” aliuliza mmoja wa watu tuliokuwa nao katika safari hiyo baada ya macho yake kuishuhudia kwa mbali. Lakini kwa mshango dereva alisema: “Hakuna shule yoyote ule ni mlima tu wa mawe mengi.” Ilioneka dhahiri kuwa ni nyumba, lakini hata tulipopiga picha kwa kamera niliyokuwa nayo, picha ilionesha kuwa hakuna nyumba yeyote. Baada ya mwendo, Kijiji cha Gamboshi kikaanza kuonekana kikipambwa na miti ya Jakaranda yenye maua mekundu, kiliioenekana ni kijiji kizuri, chenye nyumba chache na hali ya hewa nzuri.
Wakati tukiingia Gambosi, kunakuwa na hisia tofauti, baadhi wanasisimka mwili kufika kijiji ambacho kina simulizi za kukanganya na wengine wanaingiwa na hofu ya kukutana na miujiza waliyokuwa wakisikia.
Tukiwa bado tumegubikwa na mchanganyiko wa mawazo ya huko tuendako, ghafla dereva anasimamisha gari kujizuia kugonga mti mkubwa ulio mbele unaoashiria mwisho wa barabara tulishtuka.
Mmoja wa askari watano tuliokuwa nao ni mwenyeji wa kijiji hiki ingawa si mzawa. Anaelezwa kuwa ni mwenyeji kutokana na kuongoza misafara mingi ya viongozi au wageni wanaokwenda Gambosi.
“Unajua si kila askari hufurahia safari za kuja Gambosi,” anasema askari huyo na kuongeza;
“Huku, wanatakiwa watu wenye mioyo na nia safi. Watu kama mimi wasiojihusisha na mambo ya ushirikina. Hiyo ndiyo maana kila safari huwa nateuliwa.”
Baadaye tunasikia sauti na baada ya kugeuka tunamuona kijana mrefu na mwembamba anayeonekana kama mwenye matatizo ya akili, jambo linalotufanya tuanze kuwa makini kushuhudia maajabu. Baadhi yetu wanapandisha vioo.
Ndani ya sekunde chache wanajitokeza watu wengine wawili. Mmoja mzee wa makamo anayefika na kusimama pembeni mwa gari bila kutusemesha na mwingine kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30.
Kijana huyu anafanya ishara ya kututaka tufungue vioo. Meneja Ngassa aliyekuwa akiendesha gari letu ambaye anatoka jamii ya Wasukuma kama walivyo wenyeji wa Gambosi anapata ujasiri na kuteremsha kidogo kioo, ndipo kijana yule anapomwelekeza arudishe gari nyuma kidogo na kuonyesha njia inayochepuka.
Kijana huyo anayeonekana aliandaliwa maalumu kwa ajili ya kutupokea anatuelekeza hadi Shule ya Msingi Gambosi ambako ndiko ugeni wetu ulipangiwa kufika.
Tambiko kabla ya mahojiano
Kazi ya kutambika inafanywa na ntemi (si mtemi kama wengi wanavyotamka), Malosha Kufungile, kiongozi wa kimila na mganga wa tiba za asili anayeheshimika kijijini hapo.
Sote tunatakiwa kuweka mezani vifaa vyetu vyote vya kazi kuanzia kamera, vinasa sauti, kalamu na notibuku (note book) ili vitambikiwe.
Kwa ustadi, Ntemi Kufungile anazunguka meza yenye vifaa vyetu vya kazi akiimba na kunyunyiza dawa ya majimaji kama ishara ya kuvitakasa na kuvibariki.
Hata sisi hatukusalimika. Pia, tulitambikiwa kwa kunyunyuziwa dawa mwilini na kwenye viganja vya mikono. Yote haya yanayafanywa hadharani na aliyetambulishwa kwa jina la Ntemi Kufungile, ambaye alisema yeye ndiye mwenyekiti wa waganga wa tiba asili Afrika Mashariki.
“Sasa mko salama. Mnaweza kuendelea na kazi zenu bila wasiwasi,” anatamka Ntemi Kufungile.
Uchawi na Gambosi
Swali kwamba uchawi upo katika kijiji hiki, ndilo lilikuwa la kwanza kwangu tunapozungumza na Ntemi Kufungile.
“Sisi si wachawi? Hayo ni maneno ya watu wasiofahamu historia yetu. Sisi ni watu tunaoheshimu, kulinda, kudumisha na kufuata mila na desturi,” anajibu kwa upole, huku wananchi waliotuzunguka wakitikisa kichwa kuashiria kukubaliana naye.
Hata hivyo, kiongozi huyo kijana mwenye umri wa miaka 34 mwenye wake watatu na watoto wanane, anasema wanatumia zaidi tiba ya miti shamba.
“Dawa zetu ni kwa ajili ya kujitibu. Ni dawa za kuokoa maisha ya watu,” anasema kabla ya kuongeza neno la kuchanganya.
“Pia, tunazo (dawa) za kutulinda dhidi ya adui.”
Anatamba kuwa yeyote anayefika Gambosi kwa hila na nia ovu, hukiona cha mtema kuni kwa ama kupotea njia na kurandaranda hadi kujikuta amerejea alipotoka au kupita kijiji hicho bila kuona nyumba wala wenyeji.
“Anayefika kwa heri kama mlivyokuja tunampokea kwa heri vilevile na wala hatapata shida yoyote. Ila ukija kwa nia ovu utakayokutana nayo utayasimulia.
WENYEJI WANASEMA?
“Sisi ni wakulima wakarimu wa pamba, mahindi na mpunga. Yote mnayoyasikia kwamba sisi ni magwiji wa uchawi ni uvumi uliotiwa chumvi nyingi. Tunamwomba Rais wetu kwa kushirikiana na Mbunge wetu, Andrew Chenge watusaidie kulisafisha jina letu,”alisihi Zephaniah Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gamboshi.
Mwenyeji wetu pamoja na wanakijiji wenzake walidai kuwa, hofu iliyoenezwa ndani na nje ya nchi kuhusu uchawi uliovuka mipaka wa Kijiji cha Gamboshi umesababisha madhara makubwa kwa kijiji chao kiasi chakutengwa na jamii yote ya Watanzania.
“Hakuna aliyetembelea kijiji hiki kwa miaka mingi sana. Hata sisi tunapotoka nje ya kijiji, wengi hawataki kutusogelea wakiamini tutawadhuru, ” alisema Musa mmoja wa wakulima walionufaika kilimo cha mkataba kijijini Gamboshi.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, tangu Uhuru mwaka 1961, hakuna kiongozi yoyote wakitaifa aliyewahi kukanyaga kijijini hapo.
Anaongeza kuwa mtu wa pekee aliyewahi kuzuru kijijini hapo ni mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, aliyefika kijijini hapo mwaka 2010 na 2015, wakati akifanya kampeni za ubunge.
“Tume ya Katiba ilitupita, mwenge wa Uhuru nao haujawahi kupita hapa.Tuko kisiwani mbali na Watanzania wengine,” anasema Mwenyeji.
Kijiji Kikiwa mafichoni kabisa, kiasi cha kilometa 44 kutoka mjini Bariadi, Kijiji cha Gamboshi si rafiki wa watu wa Kanda ya Ziwa kama ambavyo watu wanafahamu.
Mijini na vijijini, kumekwepo na ubishani mkali kuhusu ni mkoa gani unaokimiliki kijiji hicho, ambacho baadhi ya wakazi wake wanadai kuwa miongoni mwa vioja vyake ni mauzauza yanayoweza kuifanya Gamboshi ionekane kama Jiji la New York, Marekani au London, Uingereza wakati wa usiku.
Pamoja na umaarufu wake, bado uwepo wa Gamboshi umekuwa ni kitendawili kikubwa kwa jamii ya Wasukuma kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu.
Mbali na ubishani mkali kuhusu mahali hasa kilipo kijiji hicho cha miujiza, wengi wamekuwa wakidai wakazi wake siyo jamii ya Kisukuma.
Wakazi wa Shinyanga wanadai kuwa Gamboshi iko wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wakati wale Mwanza wakidai kuwa iko mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa Mwenyeji, Gamboshi iko katika Wilaya Bariadi, karibu na mpaka unaotenganisha na Wilaya ya Magu
Kwa mujibu wa mwenyeji ni maofisa wa bodi ya pamba tu ndiyo wanaofika kijijini hapo na kwamba siyo wananchi tu wanaogopa , bali hata baadhi ya kampuni za ununuzi wa pamba.
“Kampuni ya Billlchard, moja ya mawakala wa kilimo cha mkatabaka alishindwa kutuletea mbolea hapa, badala yake akaenda kuibwaga katika Kituo cha Polisi Bariadi kwa kile ambacho wafanyakazi wake walidai ni kuhofia usalama wao.
Chanzo cha hofu
Akifafanua kiini cha chuki na hofu hiyo, Mwenyeji anadai kuwa hapo zamani ilitokea kijana mmoja kutoka kijiji jirani cha Ngasamwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na msichana mzaliwa wa Gamboshi.
“Siku moja kijana huyo alikuja kijijini hapa akimsindikiza mpenzi wake, kisha kushindwa kurudi kijijini mwake,” “Juhudi za kumsaka kijina huyo hazikiweza kuzaa matunda, hadi alipoonekana kichakani baada ya siku saba, huku ngozi yake imebadilika na kuwa nyeupe.” Anaeleza kuwa alipouliza alifikaje kichakani hapo, kijana huyo alijibu kuwa ameteremshwa na ndege kutoka Ulaya na baada ya hapo kijana huyo alirukwa na akili na kushindwa kuongea. “Ilibidi achukuliwe na kupelekwa kutibiwa na waganga wa jadi na akapona baada ya matibabu ya zaidi ya mwezi mmoja,”
Siku subiri usiku uingie niliondoka nikarudi mwanza siku hiyohiyo