Mag3,
Mwandishi akizungumza na Mwalimu Maunda Plantan mjukuu wa
Affande Plantan kuhusu historia ya ukoo wake
Nimelijibu mara nyingi hili suala la kama Wazulu walioingia Tanganyika
kama mamluki wa Wajerumani walikuwa Waislam au la kutokana na
majina yao.
Ushahidi upo kuwa waliingia Tanganyika kama Waislam na walikuwapo
ambao walikuwa na majina ya Kiislam lakini hili si muhimu kwa sasa
inabakia ni historia.
Katika waliokuja Tanganyika wakiwa Waislam ni
Ali Katini mdogo wake
Sykes Mbuwane.
Huyu alikuwa kipofu na aliingia pamoja na ndugu yake wakiwa chini ya
uongozi wa
Herman von Wissman Kamanda wa Majeshi ya Ujerumani
Tanganyika.
Kulikuwa na
Ramadhani Mashado Plantan mtoto wa Afande Plantan
huyu aliingia Tanganyika mwaka wa 1905 akiwa na umri wa miaka mitano
na alikuwa Muislam.
Huyu
Mashado Plantan ndiye alikuja kuwa na gazeti Zuhra gazeti la pili
kuendeshwa na Mwafrika gazeti la kwanza likiwa ni Kwetu la
Erika Fiah.
Kulikuwa na
Thomas Saudtz Plantan pia mtoto wa
Afande Plantan na
yeye aliingia Tanganyika akiwa Muislam.
Sasa tuje kwa
Kleist Sykes ambae ni kizazi cha kwanza Mzulu kuzaliwa
Tanganyika.
Yeye alizaliwa Pangani mwaka wa 1894 na kwa kuwa alizaliwa chini ya
himaya ya Wajerumani baba yake akiwa katika Germany Constabulary ni
Wajerumani ndiyo wakitoa majina na kusajili.
Ndipo
Kleist alipopewa hilo jina la Kijerumani lakini jina ambalo alipewa
na baba yake mlezi
Affande Plantan ni
Abdallah na hili jina lipo katika
kaburi lake pale makaburi ya Kisutu.
Kaburi la Kleist Abdallah Sykes
Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa na huu ndiyo ukoloni ulivyokuwa ukifanya
mambo yao katika nchi walizokuwa wakizitawala.
Babu yangu kama alivyokuwa
Kleist alizaliwa Tanganyika kutoka baba
aliyeingia nchini kutoka Belgian Congo na kama
Kleist walisimama dhidi
ya ukoloni na kuongoza mapambano ya kupigania uhuru wa Tanganyika.
Babu yangu
Salum Abdallah alikuwa Mmnanyema kizazi cha kwanza
katika ukoo wetu kuzaliwa Tanganyika, Shirati huko Musoma lilipokuwa
Boma la Wajerumani.
Lakini kabla ya hawa askari wa Kimanyema kuingia Tanganyika tayari kwa
miaka mingi kulikuwa na Wamanyema ambao walikuwa wamehamia kwa
miaka mingi na wakiishi Kigoma na Ujiji.
Nimeweka hapa mchango wa babu yangu wote muuone na nitaurejesha
tena In Shaa Allah kwa yule ambae ulimpita ausome.
Babu zetu hawakuwa Makaburu lau kama baba zao waliingia Tanganyika
kuja kuwasaidia Wajerumani katika vita dhidi ya
Chifu Mkwawa na
Abushiri bin Harith wa Pangani.
Nadhani nitawashangaza wengi nikiwaambia kuwa
Mkwawa jina lake lingine
ni
Abdallah.
Babu zetu wakapigana WWI upande wa Wajerumani dhidi ya Waingereza
lakini baba zetu wakapigana upande wa Waingereza dhidi ya Wajerumani
katika WWII.
Haya yote ni matatizo ya ukoloni na sasa imebaki ni historia.
Naona mnahangaishwa sana na kuwa
Cecil Matola ndiye muasisi wa African
Asociation akiwa rais.
Matola aifariki mwaka wa 1933 na Kleist 1949 miaka 16 baada ya kifo cha
Matola.
Kleist kaeleza mwenyewe katika mswada alioacha kabla ya kufariki dunia vipi
aliunda African Association akiwa Katibu muasisi.
Mimi nisingependa kulikuza hili jambo lakini ningependa kusema kuwa katika
Waafrika wa wakati wake
Kleist alikuwa mwingine kabisa na ukitaka kumjua
msome
Daisy Sykes Buruku, ‘'The Townsman: Kleist Sykes,'’ katika
Iliffe
(ed)
Modern Tanzanians, Nairobi, 1973, uk. 95-114.
Daisy ni mtoto wa
Abdul Sykes.
Mwandishi na
Daisy Sykes
Ukipenda unaweza pia kumsoma katika Dictionary of African Biography,
Oxford University Press, New York 2011 au
Kleist Sykes: Man of Ideas katika,
''The Life and Times of
Abdulwahid Sykes (1924 - 1968) The Untold Story
of Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,'' Minerva Press,
London 1998.
Mwisho ningependa kusema kuwa historia hii niliyoandika ndiyo historia ya
Tanganyika katika kupigania uhuru wa Tanganyika na kwa sehemu kubwa
Waislam walikuwa mstari wa mbele.
Sidhani kuandika historia hii ambayo ilipuuzwa ni kupanda chuki.
Mohamed Said: KUTOKA JF: BABU YANGU SALUM ABDALLAH