Vita vya makundi ndani ya chama dola kongwe tawala Zanu PF : Polisi wanamsaka mzee Geza; wanasema anakabiliwa na wizi, uchochezi wa vurugu za umma, kumtukana Rais mashtaka
Februari 12, 2025
Na Costa Nkomo
Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Zimbabwe (ZRP) limesema linataka kumhoji mzee Blessed Runesu Geza, mkongwe wa vita anayepinga "ajenda ya 2030" ambaye anakabiliwa na mashtaka manne ya makosa ya jinai.
Picha : Mzee Blessed Runesu Geza
Mashtaka hayo ni pamoja na wizi wa magari, kumdhalilisha Rais Emmerson Mnangagwa, na kuchochea ghasia za umma.
Mzee Geza, anayejulikana kwa jina la Bombshell, amekuwa mwiba kwa Rais.
Hatua hii inafuatia mfululizo wa mikutano ya waandishi wa habari iliyofanywa na mzee Geza na kundi la maveterani wa vita vya Zanu PF, ambapo walitoa wito wa kujiuzulu kwa Mnangagwa.
Wazee maveterani Wanamshutumu kiongozi wa Zanu-PF kwa kusimamia kukithiri kwa ufisadi na upendeleo, na kupanga njama ya kuongeza muda wake zaidi ya ukomo uliowekwa na katiba.
Mzee Geza pia alimgeukia Mke wa Rais, Auxilia Mnangagwa, akimshutumu kwa ufujaji wa rasilimali za serikali kwa kile anachokiona kuwa ziara zisizo za lazima nchini kote.
Wataalamu wa kikatiba kama vile Profesa Lovemore Madhuku wameshikilia kwa muda mrefu kwamba kuongezwa kwa muda kama huo haiwezekani kisheria.
Wakati Mnangagwa mwenyewe ameahidi hadharani kuachia ngazi mwishoni mwa muhula wake mwaka 2028, wakosoaji wanaonya kuwa hii ni janja na hadaa zake tu za kutuliza mambo - inayotoa hisia ya kuelekea upande mmoja huku akiegemea upande mwingine.
Wanasema kuwa aliendelea kukaa kimya juu ya suala hilo, na kushindwa kuwafuta wale wanaotetea kuongezwa kwa muda kama ushahidi zaidi.
Muhula wa Mnangagwa unakamilika mwaka 2028, lakini baadhi ya washirika wake machawa na wanachama wa chama wanaendelea kumtaka abaki madarakani hadi 2030.
Mzee Geza msema kweli daima, mjumbe wa Kamati Kuu ya Zanu-PF, alitoa kauli katika mkutano wake wa hivi majuzi na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, akiwataka Wazimbabwe kujiandaa kwa kusitishwa kwa shughuli za kitaifa huku wito wa kujiuzulu kwa Mnangagwa ukiongezeka, na hali inazidi kubadilika kwa umma.
“Tunakusihi ujiuzulu kwa amani. Usipojiuzulu kwa amani, watu watatumia katiba kutekeleza haki yao kukuondoa madarakani,” Geza alisema.
Geza pia aliwaonya polisi kwamba ikiwa watathubutu kuwapiga au kuwapiga risasi waandamanaji wanaoandamana dhidi ya Mnangagwa, umma utawawajibisha katika vitongoji vyao.
Kujibu, msemaji wa polisi Kamishna Paul Nyathi alitoa taarifa Jumatano, akisisitiza kwamba mzee Geza anakabiliwa na mashtaka ya kumtusi Mnangagwa na kuchochea ghasia za umma.
"Tuhuma za wizi kama inavyofafanuliwa katika Kifungu cha 113 cha Sheria ya Uainishaji na Marekebisho ya Sheria ya Jinai, Sura ya 9:23. Mshukiwa aliiba na kutupa magari matatu ya mlalamikaji bila ridhaa yake."
"Pia anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuvunja Kifungu cha 33 (2) (a) (ii) cha Sheria ya Makosa ya Jinai na Marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 9:23, 'Kudhoofisha Mamlaka au kumtukana Rais'" Taarifa ya Nyathi ilisema.
Kamishna Nyathi aliendelea kusema kuwa Geza alichochea wananchi kufanya vurugu, na kukiuka Sheria ya Makosa ya Jinai na Sheria ya Marekebisho.
"Kesi moja ya kukiuka Kifungu cha 187 cha Sheria ya Kuratibu na Marekebisho ya Sheria ya Jinai, Sura ya 9:23, 'Uchochezi wa kufanya vurugu za umma," Nyathi alisema.
Nyathi pia alionya kuwa yeyote atakayepatikana akimhifadhi Geza au kumsaidia kukwepa kuhojiwa na polisi atawajibika sawa kwa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.