Mapenzi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine! Ili uwe bora katika uhusiano wako wa kimapenzi, ni lazima uzijue lugha tano za mapenzi na maana yake na namna ya kuzitumia.
Lugha zinazozungumzwa hapa siyo Kiingereza, Kiswahili au Kifaransa, bali ni zile lugha ambazo moyo ndiyo huzielewa zaidi kuliko akili. Ni lugha ambazo hazitoki mdomoni bali moyoni na ukizitumia vizuri unayo nafasi kubwa ya kum-win umpendaye.
Twende pamoja katika mada hii ili kuzijua lugha hizo na kuelewa ni kwa namna gani unaweza kuzitumia kuboresha uhusiano wako wa kimapenzi.
1. MANENO YA KUMSIFIA
Maneno mazuri unayomwambia mwenzi wako, ukimsifia na kuonesha ni kwa namna gani ameyabadilisha maisha yako tangu mkutane, au ni kwa namna gani unajivunia kuwa naye, ni lugha ambayo hueleweka zaidi na yule umpendaye. Maneno haya haya yanatakiwa kuwa machache lakini yaliyobeba ujumbe mzito na unapaswa kuwa unayatoa kwa mwenzi wako mara kwa mara.
Msifie akipendeza, mshukuru akikufanyia jambo zuri, mweleze jinsi unavyofurahi unapokuwa karibu naye lakini pia mweleze jinsi unavyompenda kila siku.
2. KUMSAIDIA MAJUKUMU YAKE
Waswahili wanao msemo wao kwamba vitendo vina nguvu kuliko maneno! Yawezekana ukawa na ratiba ngumu ambayo inakufanya usikae nyumbani na mwenzi wako mara kwa mara, lakini pale unapopata nafasi ya kuwa naye nyumbani, msaidie majukumu yake ya kila siku.
Kama wewe ni mwanaume, unaweza kumsaidia kazi ndogondogo za nyumbani, unaweza kumsaidia kuwahudumia watoto kama mmejaliwa watoto na kadhalika. Lakini kama wewe ni mwanamke, mbali na kufanya majukumu yako yote ya kila siku, unatakiwa kujifunza kuhusu shughuli anazofanya mumeo na uwe mwepesi kumsaidia mambo madogomadogo hata pale ambapo hajakuomba msaada.
3. KUMPA ZAWADI
Wapo baadhi ya watu ambao unapowaambia kwamba unapaswa kumpa mwenzi wako zawadi, wanawaza mambo makubwa ndani ya vichwa vyao na mwisho wanajiona kama hawawezi. Zawadi hata ndogo kabisa, ya Ice Cream, pipi au Chocolate, ina maana kubwa sana kwa mwenzi wako. Unapombebea zawadi, maana yake ni kwamba ulikuwa unamfikiria.
Jenga utaratibu wa kuwa unampelekea zawadi mara kwa mara, na hiyo itamfanya azidi kukupenda.
4. TENGA MUDA WA KUWA NAYE
Hii kwa Kiingereza inaitwa Quality Time, muda ambao mambo yote mengine yanawekwa pembeni, inakuwa ni wewe na yeye tu! Huu ni muda ambao hupaswi kuwa bize na simu yako wala hutakiwi kuwa bize kutazama runinga, ni wewe na yeye tu. Hata kama una ratiba ngumu, jiwekee utaratibu wa kutenga hata siku moja kwa wiki ambapo wewe na mwenzi wako mtapata ‘Quality Time’ kwani ni lugha ambayo moyo huifurahia sana.
5. KUGUSANA
Sawasawa mbaba
Hii kwa Kiingereza inatwa Physical Touch, yaani wewe na mwenzi wako mnagusana. Inaweza kuwa ni kwa kushikana mikono, kwa kukumbatiana, kubusiana na kadhalika. Hata hivyo, kutokana na janga la ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na Virusi vya Corona linaloisumbua dunia kwa sasa, washauri wa masuala ya kimapenzi wanawashauri wapendanao kuacha kugusana mpaka hapo ugonjwa huu utakapodhibitiwa.
https://www.youtube.com/watch?v=MCTpBt6Onps&feature=youtu.be