Ninathubutu kusema kuwa baadhi yetu humu hatukumwelewa Prof. Shivji. Na kama tulimwelewa, tunapindisha alichokisema kutokana na kuathiriwa na mambo tunayoyaamini.
Pamoja na kutoa mawazo yake kuhusu muundo wa muungano, la msingi alilolisema Shivji ni makosa kuzungumzia muungano kwa jicho la idadi ya serikali. Alisema, muungano ni suala la demokrasia. Si suala la idadi ya serikali peke yake. Watu wa pande mbili wanakubali kuungana na kufanya mambo yao kwa utaratibu wanaouchagua.
Shivji pia alieleza kwa ufasaha kuwa rasimu ya katiba ilivyo sasa itadhoofisha muungano. Hii ni kutokana na ukweli kuwa katiba itakayotokana na rasimu hii itakosa ukuu (Supremacy of the Law ). Yaani katiba ya muungano inashauri badala ya kushurutisha nchi washirika. Hivyo, washirika wana hiari na si wajibu kufanya mambo yaliyopo kwenye katiba ya muungano. Sasa, kama Katiba ya Muungano haibani nchi washirika, ni dhahiri kuwa muungano utadhoofishwa. Na ili kueleweka vema, hapa Prof Shivji alitumia mifano ya Mashirikisho mengine duniani kama Marekani na Australia (mchangiaji mmoja hapa anasema kwa makosa hii ni kufananisha chungwa na apple). Shivji pia alieleza kuwa mambo kama vyombo vya usalama, benki kuu, mipaka ya nchi washirika yalivyo kwenye rasimu ya katiba yanaweza kudhoofisha muungano.
Shivji pia alieleza kuwa rasimu ya katiba kwenye suala la muungano ni matokeo ya compromise na si consensus baina ya wajumbe wa tume. Hivyo, bado kuna manung'uniko katika kila upande: ule unaotaka muungano wa mkataba na ule unaotaka muungano wa serikali moja. Manung'uniko hupelekea migogoro.
Mhadhara wa Prof Shivji upo online sasa. Ninashauri Bw. Maggid na wengine tuusome tena tukiwa sober. Shivji is making strong arguments.