ASANTE KWA USHAURI WAKO NA MUHIMU WASOME HAPA
Uhusiano na Uratibu wa Mambo ya Muungano (Ibara za 127 – 128)
Katiba Inayopendekezwa inaimarisha Muungano wetu kwa kuanzisha Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo ya Muungano. Chombo hiki, pamoja na mambo mengine, kitakuwa na jukumu la kukuza na kuratibu ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mojawapo ya malengo ya uratibu huu ni kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya Serikali hizi mbili na kukuza kiwango cha utoaji huduma kwa wananchi wote.
Kwa utaratibu wa sasa ipo Kamati inayoshughulikia masuala ya Muungano ambayo inaongozwana Makamu wa Rais. Kwa Katiba Inayopendekezwa chombo hiki sasa kitakuwa na nguvu ya kisheria na hivyo kuweka mfumo madhubuti zaidi wa kushughulikia changamoto za Muungano na pia kuratibu masuala mengine yanayohusiana na ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa ujumla wake.