Kutoka darasani hadi kwenye kilimo, ushirikiano wa China na Rwanda wakuza biashara ya kilimo ya uyoga ya Rwanda

Kutoka darasani hadi kwenye kilimo, ushirikiano wa China na Rwanda wakuza biashara ya kilimo ya uyoga ya Rwanda

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
VCG11426492268.jpg


Katika vilima vya kijani vya tarafa ya Bumbogo, wilaya ya Gasabo, nje kidogo ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali, kilimo cha uyoga na ujasiriamali vinazidi kustawi, vikibadilisha maisha na kuboresha mapato ya wananchi.

Katika kiini cha mabadiliko haya yupo mwanzilishi na mmiliki wa Triple S Company Ltd, Suzanne Nikuze, ambaye ni mfanyabiashara wa kilimo wa Rwanda aliyegeuza uyoga na kuwa ishara ya uvumbuzi, lishe na uwezeshaji.

Akiwa mwalimu anayetoa mafunzo na mjasiriamali wa kilimo mwenye shauku, safari ya Nikuze katika kilimo cha uyoga ilianza mwaka 2021, alipoanzisha Triple S.

Kampuni hiyo inajishughulisha na uzalishaji na utangazaji wa uyoga na bidhaa zinazotokana na uyoga. Inalenga kufanya kilimo cha uyoga sio tu chanzo cha lishe bali pia kichocheo cha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

"Nilipewa fursa ya kupata mafunzo katika Kituo cha Maonyesho ya Teknolojia (Kilimo) cha China na Rwanda katika uzalishaji wa uyoga. Pia nilipata fursa ya kutembelea China," Nikuze aliiambia Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni. "Kupitia uzoefu huu, nilielewa umuhimu wa uyoga na kutambua uwezo wake katika kuleta ajira na kuingiza kipato."

Wakati wa mafunzo hayo ndipo Nikuze alifahamu teknolojia ya Juncao, uvumbuzi kutoka China ambao unatumia nyasi badala ya kuni kama sehemu ya kilimo cha uyoga.

Tangu mwaka 2006, wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha China (FAFU) wamekuwa wakishirikiana na serikali ya Rwanda kwenye teknolojia ya Juncao, wakifundisha na kuitangaza sambamba na ubunifu mwingine wa kilimo kupitia Kituo cha Maonyesho ya Teknolojia ya Kilimo cha China na Rwanda, kilichoko katika tarafa ya Rubona, wilaya ya Huye, Mkoa wa Kusini.

Juncao, nyasi mseto iliyoanzishwa katika miaka ya 1980 na Profesa wa FAFU Lin Zhanxi, ni teknolojia ya kilimo inayofanya kazi nyingi. Inatumika zaidi kama sehemu ndogo ya kukuza uyoga wa chakula na dawa, lakini pia hutumika kama chakula cha mifugo na inasaidia katika kurejesha ikolojia. Teknolojia hiyo imepelekwa katika nchi zaidi ya 100, ikiwemo Rwanda.



Mradi wa teknolojia ya Juncao ulizinduliwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UM) mwaka 2017 na unaungwa mkono na Mfuko wa Amani na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa.

"Juncao ni teknolojia muhimu kwa sababu, mbali na kilimo cha uyoga, inaweza kutumika katika uzalishaji wa malisho ya mifugo na hata katika kuzuia mmomonyoko wa udongo," Nikuze alisema.

Kutokana na uzoefu huo, alianzisha kampuni ya Triple S akiwa na dhamira ya kukuza kilimo endelevu, kupambana na utapiamlo, na kuwawezesha wanawake na vijana kupitia kilimo cha biashara.

Leo, kampuni hii inazalisha mirija ya uyoga, inalima uyoga freshi, na kuongeza thamani kupitia bidhaa kama vile unga wa uyoga na vitafunio. Kampuni hiyo pia inatoa programu za mafunzo ya muda mfupi katika kilimo cha uyoga kwa vijana chini ya Mpango wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa Rwanda (TVET).

Ikiwa imeanza kama kampuni changa sasa imeajiri wafanyakazi wanne wa kudumu na wafanyakazi 30 wa muda, asilimia 80 kati yao wakiwa wanawake. “Lengo letu ni kuwawezesha wanawake na vijana kupitia ajira endelevu na kukuza ujuzi,” alisema Nikuze.

Manufaa ya kampuni hayapo tu kwenye utoaji ajira, bali kupitia bidhaa zake za bei nafuu za uyoga, Triple S inachangia katika vita dhidi ya utapiamlo katika jamii za wenyeji.

“Tunalenga kupunguza utapiamlo kupitia bidhaa za uyoga zinazopatikana huku tukitoa mafunzo kwa wanawake na vijana ili waweze kujiajiri,” Nikuze alibainisha.

Ndani ya miaka michache tu, kampuni hiyo imeshuhudia ukuaji mkubwa. Uzalishaji umeongezeka kutoka mirija 2,000 hadi 10,000 kwa mwezi, na mauzo ya kila mwezi yamepanda kutoka mirija 1,500 hadi 8,000, ikihudumia zaidi ya wateja 200, wakiwemo wanunuzi wa makampuni na watu binafsi.

Triple S pia imetoa mafunzo kwa vijana zaidi ya 400 katika uzalishaji wa uyoga na hivi karibuni iliidhinishwa na Bodi ya TVET ya Rwanda kuanzisha kituo cha mafunzo.

Hatua hizi muhimu zimeifanya Triple S kutambuliwa na kushirikiana na taasisi muhimu kama vile Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira ya Rwanda, Bodi ya Maendeleo ya Kilimo na Rasilimali ya Wanyama ya Rwanda, na EcoPlastic, kampuni ya Rwanda ya kuchakata upya plastiki.

Wakati Rwanda ikiendelea kuongoza uvumbuzi katika kilimo, hadithi ya Nikuze inasimama kama mfano angavu wa kile kinachoweza kufikiwa wakati elimu inapokutana na fursa na wakati wanawake wanapoongoza katika kuunda mustakabali wa kijani, wenye afya na usawa zaidi.
 
Back
Top Bottom