KUTOKA "NIKIPATA NAULI" HADI "NIKIPATA MAUA": SASA MJOMBA AMENUNUA VIATU?

KUTOKA "NIKIPATA NAULI" HADI "NIKIPATA MAUA": SASA MJOMBA AMENUNUA VIATU?

Kijana wa Ifoza

JF-Expert Member
Joined
Oct 31, 2025
Posts
1,180
Reaction score
2,302
Zamani za kale, miguu ya Mrisho Mpoto ilikuwa haina viatu, na sauti yake ilikuwa kilio cha wanyonge mitaani. Tulimzoea akisaka nauli ya kwenda mjini kumwambia Mjomba kuhusu shida za wananchi, na baadaye akatutengenezea hadithi ya Sizonje kutuaminisha kuwa yeye ndiye kiranja wa wanyonge anayejua hadi rangi ya ukuta wa chumba cha mateso ya kiuchumi. Lakini zama zimebadilika kwa kasi ya 5G. Leo hii, miguu hiyo hiyo iliyokuwa na sugu za mitaani imepata lami safi na maridadi kuelekea milango ya wakubwa, na safari hii haijabeba barua ya machozi—imebeba mashada ya maua safi yenye marashi ya gharama kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwenye ujumbe wake wa hivi karibuni uliowasha moto mitaani, Mpoto ameamua kuleta mapinduzi mapya: diplomasia ya mimea. Amemwagia sifa kedekede Rais kwa kuboresha sekta ya afya na kutoa pongezi nzito kwa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road kwa mapambano dhidi ya saratani ya matiti. Ni ujumbe mzuri, wa kiutu, na unaoelimisha kuhusu kuwahi matibabu—hilo halina ubishi. Lakini wabongo, kwa tabia yao ya kukosa shukrani na kutafuta chawa kila mahali, wameanza kukunja ndita na kuuliza: Huyu ni yule yule aliyekuwa analia njaa na wanyonge akitafuta nauli, au nauli ilizidi kiwango akajikuta amenunua hisa za ukada?
Mtaani gumzo limebadilika kutoka kwenye ugonjwa wa saratani hadi kwenye ugonjwa mpya wa kijamii: Uchawa wa Kidijitali wenye Shahada ya Uzamivu (PhD).

Wakati chawa wa kiwango cha chini kama Mwijaku na Baba Levo wakipiga kelele za kujiabisha mitandaoni, wakitokwa na povu kusaka Uteuzi na vyeo vya haraka haraka, Mpoto ameamua kuonyesha utofauti wa kisanii na kielimu. Yeye hatumii kelele za kijiweni wala matusi; anatumia mionzi ya Ocean Road na mashada ya maua kama chambo cha kupimia upepo wa teuzi. Ni uchawa ulienda shule ukagundua kuwa badala ya kupiga kelele kama daladala inayotafuta abiria, unaweza tu kubeba maua na kuonekana mstaarabu mbele ya kamera.

1792236417240.png


Wakitazama mtanange huo wa kisomi, hata kule kwenye korido za jukwaa la JamiiForums, ambako magwiji wa kupandisha nyuzi za kusifia mifumo usiku na mchana wanakesha, wamebaki midomo wazi wakijilaumu kwa nini walisoma masomo ya kompyuta badala ya kilimo cha maua. Wale wataalamu wa humu ndani wanaofahamika kwa ID zao mahususi za kupambania kila teuzi—kama vile Lucas Mwashambwa (kiranja mkuu wa mapambio ya CCM Intelijensia), Hance Mtanashati, na magwiji wengine wa kukata na shoka kama Joni na Bia Yetu—wamegundua kuwa wameachwa nyuma kwa mionzi mikali ya mabadiliko. Wale wanaotumia masaa 24 kutetea kila mradi kwa keyboard sasa wanajikuna vichwa wakiona Mjomba amekuja na uchawa wa kiwango cha juu kabisa; haandiki aya ndefu jukwaani kujaza server, yeye anapeleka maua ya live moja kwa moja getini!

Inasikitisha na kufurahisha kwa wakati mmoja. Kipindi kile Mpoto anatafuta nauli, sauti yake ilikuwa inaliza hadi mawe. Sasa hivi inaonekana sio tu kwamba alipata nauli, bali alishafika mjini, akanunua viatu vya ngozi ya mamba, na lile gari la Sizonje sasa hivi ndilo analotumia kwenda kununulia maua ya bei mbaya. Huenda hata yale maajabu ya nyumba ya Sizonje aliyokuwa anaimba kwa hofu, sasa hivi ndiyo sebule yake rasmi ya kupumzikia baada ya uchovu wa kubeba mashada.

Kupongeza juhudi za afya ni jambo jema sana na kila mwananchi anapaswa kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari. Lakini pale msanii wa wanyonge anapoanza kubeba maua mbele ya kamera huku mtaani wananchi wakigombania daladala na kukataliwa bima za afya huku wameshika makaratasi ya michango ya matibabu, lazima akina Mwijaku, Baba Levo, na wale magwiji wa keyboard wa kule JamiiForums wajisikie wanyonge na walioachwa nyuma. Wataona Mjomba anataka kuwanyang'anya tonge mdomoni kwa kutumia mbinu ya kisomi ya kukata raba peku, kuvaa suti, na kugeuza matatizo ya afya kuwa jukwaa la kupandisha wasifu wake wa kisiasa!








 
Back
Top Bottom