Unajua unajisi wa mbwa unakuja vipi, au ukoje? Unajua kama ni ruksa kufuga mbwa?
Mbwa mwenyewe hawezi kusemwa ni najisi kwa kutokuwa na dalili ya hilo, isipokuwa mate yake na majimaji ya puani mwake yanachukuliwa ni najisi ki-Shariy’ah ikiwa ni wa kufuga au vinginevyo kwa dalili iliyopatikana kutoka katika Hadiyth. Na kwa hivyo chombo chochote ambacho kitarambwa na mbwa kinapaswa kutwaharishwa kwa kuoshwa mara saba bila kutofautisha ni mbwa gani aliyekiramba, mojawapo kwa mchanga. Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kukitwahirisha chombo kilichorambwa na mbwa kunafanywa kwa kuosha mara saba, mojawapo kwa udongo” [Ahmad, Muslim, Abu Daawuwd na al-Bayhaqiy]
Na ikiwa ataramba chombo chenye chakula kikavu, kile chakula kilichoguswa na mdomo wa mbwa na kilicho pembezoni mwake kinatakiwa kitupwe, ama kilichobaki ni twahara kinaweza kubakishwa. Ama manyoya ya mbwa yakiwa makavu ni twahara. Sehemu iliyo najisi ya mbwa ni ule mdomo wake kwa ajili ya umandemande.
Hivyo, mtu kucheza na mbwa au kumpakata na kumfanya ni kichezeo, si jambo lenye kushauriwa kwa kupatikana uwezekano wa kunuswa au kurambwa nguo yake na maeneo ya kuswalia na sehemu mbalimbali za nyumba yake. Mbwa si kama paka, hivyo si jambo zuri watu kuiga tabia za wasio Waislamu na wao kuanza kufuga mbwa wa vichezeo na kuwafanya kama paka. Muislamu hata akibidi kuwa na mbwa wa ulinzi, anapaswa amweke nje ya nyumba; uani au sehemu ambayo si ndani ya nyumba ili kuepuka kutiliwa najisi vyombo, nguo na sehemu za kufanyia 'ibaadah.