SoC02 Kuufumua Msukosuko

SoC02 Kuufumua Msukosuko

Stories of Change - 2022 Competition

Yohana Mayenga

New Member
Joined
Aug 8, 2022
Posts
1
Reaction score
0
“Wanameremeta, wanameremeta”, sauti za akina mama zilisikika na vigelegele vilisikika hapa na pale. ‘’Shosti yetu kashauaga umaskini’’ Nyemo aliwaambia wasichana wenzake aliosimama nao huku akimuonyeshea Sapora na Dakute ambao walipanda gari kuelekea fungate. ‘’Cheki gari lile! Kuna usafiri na magari lile sasa ni gari”, alidakia Chakuye huku akiwa anaonyeshea gari aina ya Range Rover Sport jeusi. “Ila jamani baada ya dhiki faraja’’ Salome naye alitia neno. Salome alisema hivyo akirejelea yaliyotokea. Basi ndugu msomaji yaliyojiri niruhusu nikujuze. Sapora ni binti aliyetoka kwenye familia ya watoto watatu ya hali ya chini. Baba na mama Sapora waliishi kwa amani ama kwa lugha nyingine mama Sapora alijitahidi kutunza amani. Baba Sapora alikuwa ni mlevi na asiyejishughulisha na majukumu ya familia, zaidi sana alijijali yeye na pombe zake na alikuwa anapenda kubeti ila kama suala la bahati liko Dar es Salaam yeye alikuwa visiwa vya Comoro. Kila siku alikuwa analiwa kichwa tu na hakusita kukopa sehemu mbalimbali na wadai wake wakajua namna ya kuzipata hela zao nayo ni kumbana Mama Sapora ambaye bila hiyana akikumbuka mafunzo ya unyagoni kuwa ndoa ni uvumilivu akavumilia kwa pesa zake.

Pesa kichele matumizi bahari ndio yalikuwa maisha ya mama Sapora naye akaona kuwa VICOBA ndiyo kimbilio la kutoka kimaisha. Alichukua mkopo wa laki tatu kwa ajili ya kuongeza mtaji wa biashara yake ya kuchoma chapati. La kuvunda halina ubani na ingekuwa heri asingaliuchukua mkopo maana aliziweka fedha chumbani kwake na baba Sapora akazitumia kubeti na kama kawaida bahati haikuwa upande wake. Mama Sapora alivurugwa na yaliyotokea maana aliwaza kuhusu marejesho ya mkopo. Rafiki yake Mama Seso alimwambia, ‘’Shoga njia ya kipato si moja, nakuambiaga unajikuta mtakatifu sana mpenda ndoa kwa mume yupi unayemtunzia heshima? We danga tu! Yakikushinda kaokote makopo’’. Basi siku moja isiyo na jina baada ya kutoka kwenye meza yake ya chapati mama Sapora akaupara mwenyewe akatoka mlangoni kumfuata Boni muuza unga maana aliweka miadi naye ila akahisi miguu mizito pembeni akaona kiroba. Akajisemea, ‘’Kwani wanaookota makopo na wenyewe si watu tu?”, akakisogelea na akakinyanyua kisha akaelekea mtaani kusaka makopo ili aongeze pesa maana asingeweza kumudu maisha kwa kipato alichokuwa nacho wakati ule na neno marejesho lilikuwa kama mwangwi unaongezeka sauti kila uchwao. Akaenda mtaani huku na huku akitafuta bila mafanikio shikika, akatazama upande wa pili wa barabara akaona kama chupa tano hivi akakanyaga lami ili kuvuka na ghafla akagongwa na lori na umauti ukamfika pale pale.

Mazishi yalifanyika na matanga hayakuchukua muda mrefu kwani fedha za kuendesha msiba zilikuwa ni tia maji tia maji na kama Mzee Siteswa asingeingilia kati hali ingekuwa kwenye tete. Siku tatu baada ya matanga kuanuliwa Mzee Siteswa alimtuma dereva wake kwa baba Sapora na kumualika nyumbani kwake, alipofika alimueleza kuwa kijana wake, Dakute alitaka kumuoa Sapora. ‘’Mhh’’ baba Sapora alishusha pumzi. Mzee Siteswa akamuuliza “Yaani huna shukrani baada ya yote niliyokutendea?’’. ‘’Hapana mkuu mimi sina tatizo kabisaa mapenzi yako ni amri kwangu lakini naogopa jela umesahau Sapora ni mwanafunzi tena ana miaka kumi na sita tu?’’ baba Sapora akajibu. Mzee Siteswa akainua simu yake na kumpigia Wakili wake na akamuelezea ili kujua kama kuna hatari yoyote kisheria. “Mzee moshi mweupe kama wa uchaguzi wa papa hata ingekuwa kuna kashikashi tungepenyeza rupia na udhia ungekimbia,” Wakili Msomi Jasore alimhakikishia kuwa hakuna tatizo lolote kisheria ili mradi tu mzazi awe ameruhusu maana sheria ya ndoa ya mwaka 1971 haijabadilishwa bado licha ya ushindi wa Wakili Msomi Rebecca Gyumi mwaka 2016 katika kesi yake dhidi ya serikali akipinga ndoa za utotoni. “Ukiona kama inasumbua tajiri kijana amtunuku tu ujauzito’’ akamalizia Wakili Jasore. Basi ndugu msomaji hayo ndiyo yaliyokuwa nyuma ya pazia kabla ya watu kuimba hayawi hayawi.

Nyemo, Salome na Chakuye waliondoka pamoja na kutembea kurudi majumbani mwao. Njiani walimwona mama Nyemo aliyetoka hospitali alikokwenda kwa ajili ya matibabu. ‘’Shikamoo mama’’, walisema kwa pamoja na kisha aliitikia na Nyemo akaanza hapo hapo kumsimulia yaliyojiri. ‘’Mama yaani Sapora alipendeza kwelikweli ni ndoa ya kimila lakini lile gauni la kizungu’’. Wenzake walicheka na mama mtu naye akaachia tabasamu tatanishi kama alifurahi kama hakufurahi vile. Akamwambia ‘’Mwanangu Nyemo kuna gauni natamani uvae, lile dera la kisomi ‘’. ‘’Haliitwi hivyo mama”, alidakia Chakuye “linaitwa joho”. “Hilo hilo wanangu magauni mengine yote utajinunulia ama utanunuliwa lakini lile ni la tofauti. Binti zangu mimi sikupata nafasi ya kusoma kama nyinyi lakini niliposikia kuwa kuna MEMKWA niliamua mwenyewe kujiunga na hivi sasa naweza kusoma na kuandika. Nyinyi hamjachelewa kufikia ndoto zenu msikubali kuvaa shela kabla ya joho. Sapora ameolewa na Dakute katika umri mdogo sana mnadhani ataweza kuzifikia ndoto zake? Maskini! tena katoto kale ndo kalikuwa kakiranja ka taaluma na kiingereza chake kilikuwa kizuri yaani kama mzungu”. “Mzungu wapi?” anadakia Nyemo. ‘’Wivu tu umekujaa” alisema mama Nyemo na wenzake Nyemo wakacheka. ‘’Mama sisi tunaendelea”, Chakuye aliaga maana walikuwa wamefika kwa akina Nyemo na alikuwa akiendelea mbele zaidi na Salome. Waliagana vizuri na mama Nyemo akaendelea kuongea na bintiye.

‘’Mimi sikubali kabisa uolewe sasa hivi hata aje mtu na utajiri gani mwanangu. Nimeamua kutokuyarudia makosa ya walionitangulia na kuwa mfano. Sisubiri serikali inihamasishe kwani faida ya maamuzi yangu nitaila mwenyewe na hasara yake sitagawana na serikali. Serikali ipo kunisaidia ila hainiondolei wajibu binafsi kama nahodha wa maisha yangu’’, mama Nyemo aliongea kwa hisia. Nyemo akamuuliza, ‘’Hivi mama kwa nini hujagombea uongozi? Maana sio kwa hekima hizi”. Mama Nyemo alicheka kisha akajibu ‘’Siku moja tu itakuwa ila sasa acha niuze mihogo yangu tu’’. ‘’ Ila mama kiuhalisia shoga angu Sapora kayakanyanga kajisemea Mandonga ndo nini kuolewa na teja?”, Nyemo aliongea kwa masikitiko. ‘’ Kumbe saa zingine zimo mwanangu, hapo umenena muathirika wa madawa ya kulevya anahitaji matibabu hahitaji mke. Ila ndo hivyo sasa malezi mabovu ya wazazi kuwalea watoto kama mayai yanachangia. Vijana hawana budi kujifunza kuwa heri kutokuanza kabisa madawa na vilevi maana kuna mstari mwembamba sana kati ya uraibu na matumizi. Starehe ya muda mfupi isikufanye ufanye maamuzi yenye athari za muda mrefu.’’ alisema Mama Nyemo huku akijilaza mkekani chini ya mti.

Nyemo alimuaga mama yake na kisha akaenda kuchota maji kisimani. Njiani aliwaza, “Hivi kuna hasara gani nikipambana kuzipigania ndoto zangu? Mama husema juhudi haijawahi kuua mtu. Kuzaliwa binti sio hasara na sio mkosi kuna mengi naweza kufanya kupambania ndoto zangu. Kama mama yangu anaogopa kugombea uongozi mimi nitagombea ubunge na nitashinda tu siku moja. Weweee kama najiona na skokonko zangu bungeni sijui niwe spika kabisa au niwe raisi? Au basi! Hivi nitaongea nini na wananchi?’’ aliendelea kujiuliza. Akaweka ndoo chini akakohoa kidogo kisha akaanza kuwahutubia wananchi wake hewa, “Ndugu wananchi njia pekee ya kutoka katika msukosuko ni kuufumua kwa kuwa wakala wa mabadiliko. Serikali inajitahidi kufanya kwa sehemu yake na nyinyi mjitahidi kwa sehemu zenu kufanya maamuzi yenye tija na kuyatekeleza. Yatupasa tujenge utamaduni wa uwajibikaji na tabia ya kusimamia kwenye ukweli na haki. Vita dhidi ya umaskini ni yetu sote lakini kabla ya kupambana nao tujitathimini umaskini umetufikiaje na tushughulikie viambajengo vyake kama uvivu, ulalamishi, ujinga na mengineyo mfano wa hayo ili tusiwe tunapiga ngumi hewani. Vijana hamna budi kujibidiisha katika kazi na si makundi rika yasiyo na tija au kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu vyenye kutia aibu familia zenu na jamii kwa ujumla. Elimu, elimu, elimu nimeitaja mara tatu iko haja ya kuwekeza katika elimu ambayo mizizi yake huwa michungu lakini matunda yake ni matamu. Ndugu wananchi, mila potofu hatuna budi kuachana nazo pia kwa maana zinatutendea ubaya kuliko wema. Ukiamua wewe kama mwananchi mmoja unaweza ukaleta badiliko lakini ukinyamaza na kuyaacha mambo yaendelee tutauendeleza mzunguko wa matatizo katika jamii yetu. Mwisho kabisa nipende kuwashukuru kwa kunisikiliza mbunge wenu na niwatakie kila la kheri katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku”.

‘’Wacha weee! Una hatari we mtsotso,’’ Bobi Madusko alidakia na kuiacha bodaboda yake aliyokuwa ameipaki pembeni na kumfuata Nyemo. Bobi Madusko alikuwa akimsumbua Nyemo kwa muda akimtaka awe mpenzi wake. “Unajua nini? Wewe ndiye mbunge wa moyo wangu yaani kura zote nishakupa mama. Umeona harusi ya mwenzio ilivokuwa? Ya kwetu itabamba zaidi mimi ndiye Bobi Madusko baba lao”, akaendelea kujinadi. Nyemo akamjibu “Kwa hela ipi uliyokuwa nayo? Mimi ni binti mwenye malengo na kwa taarifa yako mimi sihitaji kuyumbishwa na mpita njia yeyote katika safari ya kuzifikia ndoto zangu. Hivi huoni aibu kunifuatilia na umri wako huo. Tafuta wakubwa wenzio”. Bobi alijibu kwa hasira “Yaani huna maadili kabisa’’. “Wewe mwenyewe huna dili” Nyemo naye alirudisha maneno na kisha akajisemea kimoyomoyo ‘’Leo nimemuweza”. Nyemo akachota maji na kuanza safari ya kurudi nyumbani.

Njiani alikutana na Chakuye na Salome wamejitanda khanga. Anawauliza “Kulikoni? Mbona na maguo mmejitanda kimetokea kipi?’’. Chakuye alijibu huku chozi likimdondoka jicho la kushoto, “Sapora hatunaye tena. Yeye, Dakute pamoja na mtoto wake aliyekuwa tumboni wametangulia mbele ya haki. Dakute aliwasha msokoto ndani ya gari wakielekea fungate na Sapora akabanwa na pumu. Dakute alipoona vile akajua anajifanyisha kupandwa na mashetani akaanza kumpiga mpaka akatokwa na damu nyingi na kupoteza fahamu. Dakute alipoona damu akajua ameua akashuka huku gari inakimbia hakuangalia kuwa kuna pikipiki inayokuja kwa kasi ikamgonga na akafa. Dereva alimkimbiza Sapora zahanati lakini alifariki muda mchache baada ya kufika zahanati”. “Kazi ya Mola haina makosa”, Salome alisema. “Hapana shosti hii ni kazi ya mtu”, Nyemo alisema na ukimya mkuu ukatanda kati yao.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom