Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Historia imeandikwa mkoani Tabora na mikoa jirani ambapo kwa mara ya kwanza watoto wawili wenye vichwa vikubwa wamefanyiwa upasuaji kupitia kambi maalum ya matibabu ya kibigwa na bobezi inayoendesha na Madaktari bingwa, Wauguzi, Mtaalam wa usingizi kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) kwa kushirikiana na Wataalam wa hospitali ya Rufaa Nkinga, Tabora.
Daktari bingwa mbobezi wa Ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka MOI Dkt. Alpha King`omela amesema lengo la kambi hiyo ni kuendelea kuwajengea uzoefu Madaktari, Wauguzi na Wataalam waliopo katika hospitali ya Rufaa Nkinga, Tabora.
Kwa upande wake Daktari wa upasuaji wa hospitali ya Rufaa ya Nkinga Dkt. Richard John amewashukuru wataalam wa MOI kwa kuwajengea uwezo huo.
“kwa mara ya kwanza nimeshiriki kuwafanyia upasuaji watoto wawili wenye vichwa vikubwa katika hospitali yetu, awali watoto hawa tulikuwa tunawapa Rufaa ya kwenda kutibiwa Bugando na MOI lakini sasa tumejengewa uwezo na upasuaji huu utakuwa unafanyika hapa kwetu” amesema Dkt. John
Naye, Mkazi wa Tabora Mzazi wa mtoto Nathan amesema amenufaika kupitia kambi hiyo kwani afya ya mtoto wake inazidi kuimarika kwani awali alikuwa ana changamoto nyingi lakini sasa anaendelea vizuri baada ya upasuaji.
Taasisi ya MOI inazidi kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuzidi kuongeza wigo mpana wa tiba za kibingwa na bobezi katika hospitali za Rufaa na Mikoa.