Ndio maana mtakatifu Paulo katika barua yake kwa Wafilipi 1:21 anatushawishi kuwa tujirudi na kuikubali maana sahihi ya kifo, kwamba kifo hakitutenganishi na wenzetu katika Kristu, wala na Kristu mwenyewe, na kwamba sisi tukifa tunakufa katika Kristu na tutaishi naye, kumbe baada ya ubatizo wetu hakuna kinachoweza kututenganisha katika umoja aliotuombea Kristu kwamba tuwe na ?umoja kama wao UTATU MTAKATIFU walivyo wamoja?.
Tunaalikwa kuona kuwa kifo si mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa maisha mapya katika Kristu, maisha ambayo sina shaka kila mwanadamu mwenye akili timamu anayatamani kuyarithi. Sala zetu na sadaka zetu zina thamani ya pekee mbele za Mungu na kwa ajili ya ndugu zetu waliotoharani. Hatuzungumzii kuyabadili mawazo ya Mungu au kumhonga Mungu kwa sadaka na sala zetu kama wengine wanavyotufikiria katika siku hii tunapowaombea ndugu zetu marehemu, kitu cha msingi na cha uhakika ni nia yetu njema katika sala, sadaka na maombezi kwa ajili ya ndugu zetu.
Ni ukweli usiopingika kwamba katika umoja wetu na ndugu zetu marehemu na watakatifu Mungu anakuwepo kati yetu, anazibariki na kuzikubali nia zetu. Kumbe kuwaombea marehemu ni tendo la kiimani, na tunapaswa kufanya kwa imani na kwa hakika itazaa matunda mema katika imani, tusonge mbele na nia yetu njema katika hili, bila aibu na hofu yoyote, sisi tunaamini na tunajua kwa nini tunafanya hivyo.
Tunapowakumbuka ndugu zetu marehemu, tukumbuke kwamba na sisi ni marehemu watarajiwa ili tufe katika hali ya neema inayotakiwa katika kuurithi uzima wa milele. Kama kuna jambo tunalopaswa kuwa na uhakika nalo ni kufa, kumbe tunapaswa daima kuwa tayari, kwa sababu hatujui siku wala saa atakapotuita Mungu toka maisha haya.
Ni bahati mbaya hatupendi kusika neno kufa katika maisha yetu licha ya kulizungumzia, lakini cha kushangaza ukimwuliza mtu kama anapenda kwenda kwa Mungu kila mmoja anapenda awe ya imani gani, tunasahau kuwa hatuwezi kurudi kwa Mungu bila kufa, na kufa ni mabadiliko ya ghafla ya maisha ya sasa na kuingia katika maisha ya milele tukifa katika neema ya Mungu.