Hii alama ina historia ndefu na ya kusisimua, hasa ukifuatilia historia za wanaohusishwa na alama yenyewe. Asili yake imetokana hasa kutokana na mungu wa Kigiriki anayeitwa Asclepius, lakini inahusishwa pia na hadithi ya Musa kwenye Biblia. Ipo hivi:
1. Fimbo ya Asclepius (Rod/staff of Asclepius)
Kwa mujibu wa hadithi na imani za wagiriki (Greek mythology), mungu Asclepius alikuwa anashika fimbo kama hiyo yenye nyoka. Mungu huyu ndiye anayehusika na uponyaji/dawa/udaktari. Ni alama ambayo imekuwa inatumika muda mrefu sana na inatambulika vizuri na yeyote aliyesomea udaktari/uuguzi. Alama hii ipo pia kwenye bendera ya World Health Organization (WHO).
Mwanzoni mwa miaka ya 1900, jeshi la Marekani likaanza kutumia alama nyingine yenye nyoka wawili, fimbo/fito na mbawa juu, ambayo imekuwa ikitumika kimakosa (Caduceus, angalia hapa chini). Caduceus ina maana tofauti kabisa na hii ya nyoka mmoja. Caduceus ni alama ambayo asili yake ni mungu Hermes (ugiriki), ambaye yeye alikuwa anahusishwa zaidi na uwakala wa miungu na muunganishi wa ulimwengu wa wafu/roho. Hermes anafahamika zaidi kwa huo uwezo wake wa kuingia na kutoka kwenye ulimwengu wa roho/wafu na kusaidia wale wanaokata roho au wanaotaka kufa waingie kwenye ulimwengu wa wafu/roho bila shida pamoja na mambo mengine mengi. Alikuwa anafahamika pia kwa mambo mengi, ikiwemo udanganyifu wa kujibadilisha ili kuwazuga miungu wenzie ilimradi tu afurahi mwenyewe. Baadae, Warumi walimuhusisha Hermes pamoja na hiyo alama yake na mungu Mercury, ambaye alikuwa ana tabia za kufanana. Kwa hiyo, popote utakapoona hii alama ya Caduceus inatumika na taasisi ya tiba, jua kuwa hawajasoma historia vizuri.
Alama zenyewe hizi hapa:
Sanamu ya mungu Ascelipus:
Sanamu ya Mungu Hermes:
2. Hadithi ya Musa kwenye Biblia, kitabu cha Hesabu, mlango 21, mstari wa 4 hadi wa 9:
4. Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. 5. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. 6. BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. 7. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. 8. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. 9. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Nadhani hiyo ya hadithi ya Musa kwenye Biblia inajieleza vya kutosha.