Nimesikia matamko toka kwa viongozi wakidai kwamba ni aibu kwetu kuomba vyombo vya nje kuja kutusaidia kutafuta wahalifu waliotaka kumuua Lissu na mauaji mengine kama ya Kibiti, maiti zinazopatikana baharini, kupotea kwa kina Ben Saanane nk. Ni kama tunasema hao wasiojulikana ni afadhali waendelee kutojulikana kuliko aibu ya wao kujulikana kwa kusaidiwa na mataifa toka nje.
Lakini wakati huo huo, Tanzania tumekuwa mstari wa mbele tunapotembelewa na viongozi wa nje, na hata nchi ndogo kama Morocco, tunaomba msaada wa vitu kama kujengewa misikiti na viwanja vya michezo.
Sasa nashindwa kuelewa, hivi ni lipi kati ya haya mawili linatia aibu zaidi kwa taifa letu? Kama tunaweza bila aibu, tena kwa nchi ndogo kama Morocco, kuomba msaada wa kujengewa msikiti na uwanja, iweje tuone aibu kuomba mataifa makubwa kuja kutusaidia matatizo ya uhalifu ambayo yana harufu kali ya kigaidi?
Je, ni aibu tunayohofia ikiwa tutaomba msaada wa kuwatafuta hao wasiojulikana, wahalifu wa mauaji, au ni kutaka ukweli fulani usijulikane?