Kitabu cha 1 Wafalme 8:29-30 kinatuambia kwamba Mfalme Sulemani aliomba huku akilielekea hekalu lililokuwa Yerusalemu. Sasa swali ni hili: kwa nini Wakristo hawafanyi sala kama Sulemani? Mbona hawana mwelekeo maalum wanaposali? Usiumize kichwa kutafuta majibu. Majibu haya hapa:
Kwanza ni muhimu kukumbuka kwamba, Yesu Kristo alipokuja duniani, Mungu hakuendelea kukaa katika hekalu lililotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Yesu Kristo alizaliwa na kuishi pamoja nasi. Yesu ni Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi (Mathayo 1:23). Hii inamaanisha kwamba hatuhitaji kugeukia upande fulani ili kumfikia Mungu, maana Mungu yupo nasi kila mahali na upande wowote.
Na sisi wenyewe sasa ni Hekalu la Mungu. Biblia inasema: “Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu?” (1 Wakorintho 6:19). Hivyo Hekalu haliko tena Yerusalemu peke yake. Popote alipo Mkristo, ndipo hekalu la Mungu lilipo. Kwa sababu hiyo hatufungwi kusali kwa kuelekea upande fulani.
Katika mahubiri yake, Yesu alimwambia mwanamke Msamaria:
“Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.” (Yohana 4:23).
Hapo tunaona Yesu akionyesha kuwa ibada na sala hazifungwi tena na uelekeo wa mahali hekalu lilipo. Tunachotakiwa tu ni kusali kwa roho na kweli, mahali popote.
Yesu mwenyewe aliomba bila kuelekea upande maalum. Yesu aliomba jangwani, mlimani, katika bustani, na msalabani, bila kuashiria mwelekeo maalum.
Hicho ni kielelezo kwamba sala ni mawasiliano ya moja kwa moja na Mungu. Mungu yupo kila mahali na katika kona zote za dunia.
Paulo na Sila waliomba wakiwa gerezani, na milango ya gereza ikafunguka (Matendo 16:25–26). Wakati wanaomba, hawakugeukia Yerusalemu.
Labda unajiuliza tena: kwanini basi Sulemani aliomba huku akielekea Yerusalemu? Huyo alikuwa anafuata maagizo ya Kum 12:5 kwamba mahali atakapochagua BWANA Mungu, apaweke jina lake, ni makao yake, hivyo waelekeze nyuso zao hapo. Yerusalemu ilichaguliwa iwe makao ya Mungu. Ndio sababu Sulemani alijenga hekalu Yerusalemu. Lakini sasa Mungu hafanyi makao katika majengo, bali ndani ya waaminio kama tunavyosoma katika Yohana 14:23
Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
Kwahiyo kama tulivyoona, baada ya kuja kwa Yesu Kristo, ufunuo ulitimia: Mungu yupo pamoja nasi kila mahali, amefanya makao ndani yetu; na sisi wenyewe tumekuwa hekalu lake. Hivyo Wakristo tunaposali, hatuna haja ya kuhangaika kujua Yerusalemu iko wapi. Tunaomba kwa kuelekea upande wowote, na Mungu anasikia na kutupatia haja zetu (Mathayo 7:7).