Tulipendana sana, tukapanga mipango kedekede ya maisha yetu ya baadae na kuahidiana kila aina ya ahadi tamu tamu lakini yote hayo hakuyajali na kwa kuwa moyo wa mtu ni kichaka sikuweza kung'amua lolote mpaka siku ile ambayo sitakaa niisahau maishani mwangu!
Kama ilivyoada aliniaga kwa mabusu moto moto, nilijua ni moja kati ya safari zake za kibiashara, nilimwombea kila la heri huko aendako. Na safari ikaanza na kuniacha mwenye majonzi kwani nilijua nitamkosa kwa muda usiopungua wiki moja, kilichoniumiza zaidi ni kujua fika kuwa baada ya masaa yapatayo 12 nisingeweza kuwasiliana naye hata kwa simu maana aliniambia kuwa huko aendako ni maporini kusiko na network. Nilimwamini pasipo shaka. Naam baada ya masaa 12 sikuweza tena kumpata kwenye simu zake zote ila haikunipa shida kwani nililijua hilo.
Siku tatu baada ya kuondoka kwake, mida ya jioni nilishtushwa sana baada ya kupigiwa simu na rafiki yangu mmoja na kunipa pole kabla ya kuniuliza imekuwaje? Badala ya kumjibu nilimwuliza kwa wasiwasi mwingi, ananipa pole ya nini? Na imekuwaje nini? Jibu lake ndilo lilinifanya mpaka leo nisiisahau hiyo siku! Alicheka kwa kejeli kisha akanijibu ina maana hujui kama fulani(alitajajina la mpenzi wangu aliyesafiri siku 3 zilizopita) kanilipia mahali leo na kesho tunaenda kuandikisha ndoa kanisani? Sikusikia kingine alichokiongea bali nakumbuka mwangwi wa maneno yale yaliendelea kujirudia masikioni mwangu kwa masaa kadhaa kabla ya kulala (sina uhakika kama nililala au nilizimia)
Nilipoamka nilikuta simu ikiwa chini huku kioo cha simu kikiwa kimevunjika na betri ya simu imedondokea upande wake, nikajua kuwa baada ya taarifa zile nilidondosha simu pasipo kujijua.
Baada ya wiki moja mpenzi wangu alirudi kama alivyoniahidi akiwa na zawadi lukuki, nilizipokea na nilijaribu kuficha hali niliyokuwa nayo lakini aligundua kuwa sikuwa sawa akaniuliza nina tatizo gani nikamwambia ninaumwa na nimeshauriwa na daktari kupumzika muda mwingi. Alinionea huruma akataka alale kwangu ila nikamkatalia, nikamwambia nahitaji kuwa mwenyewe ili niweze kutumia muda mwingi kwa kulala. Alinielewa na akaondoka.
Sikuonana naye tena kwani kesho yake asubuhi na mapema nilisafiri kwenda mkoa mwingine na nilibadilisha namba ya simu. Tulionana tena siku ya harusi yake na rafiki yangu kipenzi, ilinibidi kwenda kanisani kushuhudia ndoa yao kama nilivyoshauriwa na mwanasaikolojia wangu. Aliniambia hiyo itanisaidia kuamini kuwa yule jamaa si wangu tena. Wakati wanatoka kanisani baada ya ndoa, nilihakikisha maharusi hao tunaonana ana kwa ana, kisha nikatokomea.
Haikuwa rahisi hata kidogo kuendelea na maisha ila kwa msaada wa ushauri wa mwanasaikolojia niliweza kuendelea na maisha japo ilinibidi kubadilisha mtindo wangu wa maisha.
Miezi 6 baada ya ndoa nilipata taarifa kuwa wanandoa wale walipata mtoto wa kiume, ila mtoto mwenyewe ni mwarabu wakati wazazi wake ni Wandengereko wenzangu. Hahahahaaaaa....nacheka kama mazuri mie. Wambea ikawa kutwa kucha wananilitea habari, ile ndoa si ndoa tena bali imegeuka ndoano baada ya kuzaliwa mtoto wa kiarabu. Nikasema pole yao, wavumilie tu maana kitanda hakizai haramu.
Juzi jamaa kanifuata anasema nimsamehe, yalopita si ndwele tugange yajayo. Ameachana na mkewe (rafiki yangu) kama niko tayari tukafunge ndoa ya bomani, niwe mkewe. Ametambua kuwa alifanya kosa kubwa sana kuniacha. Nimemwambia nilishamsamehe kitambo sina kinyongo nae hata kidogo ila "PEMA NI PEMA USIPOPEMA, UKIPEMA SIO PEMA TENA"!