Yesu hana sifa za Mungu
YESU SI MUNGU:
KWA SABABU HANA SIFA ZA MUNGU
Mwenyezi Mungu Anazo sifa zifuatazo ambazo Yesu hanazo hata sifa moja wapo. Mwenyezi Mungu ndiye muumba wetu ni mmoja. Anajulikana na anatambulikana kwa sifa zake.
Biblia inatuelezea sifa Mungu zinazotajwa katika Biblia. Vilevile nitaeleza kwamba Bwana Yesu Kristo hana hata sifa moja sawa na Biblia.
1. MUNGU HAJARIBIWI
Biblia inasema kwamba: “Mtu ajaribiwapo, asiseme, ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala mwenyewe hamjaribu mtu,” (Yakobo 1:13).
Sasa tuone hali ya Bwana Yesu Kristo kwamba yeye anayo sifa hii au ni kinyume chake. Biblia inasema kwamba: “ Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi,” (Mathayo 4:1).
Mungu hajaribiwi lakini Yesu alijaribiwa na Iblisi, kwahiyo hawezi kuwa mungu, kwa sababu ya kukosa sifa hii
ya Mungu.
2 MUNGU ANAJUA KILA KITU
Ni sifa ya Mwenyezi Mungu kujua kila kitu cha dhahiri na cha siri. Kitu chochote hakiwezi kufichika kwake. Kama Biblia inavyosema kwamba: “Basi usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukampe kila mtu kwa kadri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote.” (1Wafalme 8:39).
Sasa tuone kiwango cha Bwana Yesu cha kujua mambo. Biblia inasema kwamba: “Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara.”
(Mathayo 21:18-19).
Mtu ambaye hajui kwamba msimu huu mti fulani haupatikani matunda ilhali hata watoto wadogo wanajua misimu ya matunda mbalimbali, hawezi kuwa Mungu.
Tena aya hii inaonesha tabia ya Bwana Yesu kwamba mwenyewe alikosea kujua msimu wa matunda ya mtini
na kisha akaulaani mti bure.
Pia Bw. Yesu anakiri mwenyewe kwamba hajui chochote kuhusu habari za saa ile (Mathayo 24:36).
3. MUNGU HACHOKI
Mwenyezi Mungu hana kasoro ya udhaifu wowote. Sifa zote njema zinamhusu yeye. Biblia inasema kwamba: Je, wewe hukujua? hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana muumba miisho ya dunia, hasinzii wala hachoki, akili zake hazichunguziki.” (Isaya 40:28).
Sasa tuone hali ya Yesu. Je, yeye anayo sifa hii ya Mungu? Kama hana, basi hawezi kuwa Mungu. Biblia inasema: “Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, Basi Yesu kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo yapata saa sita.” (Yohana 4:6). Basi mwenye kuchoka hawezi kuwa Mungu.