*MKURUGENZI Msaidizi wa miradi katika wizara ya fedha na mipango, Mhandisi Leopold Lwajabe (56), ameripotiwa kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.*
Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Kigogo huyo mwandamizi katika wizara ya fedha, mwili wake umekutwa umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
“Niko hapa hospitali ya Mkuranga mkoani Pwani. Nimeona mwili wa ndugu yangu Leopald Kweyamba Lwajebe, ukiwa umehifadhiwa katika chumba cha maiti,” ameeleza Mugisha Bagoka Brassio, ndugu wa Mhandisi Lwajabe.
Anasema, “tumeambia na viongozi wa hospitali hii, kwamba mwili wa ndugu yetu uliletwa hapa hospitali na askari poli. Uchunguzi wa polisi unaonyesha kuwa kifo chake kimetokana na kunyongwa shingo yake kwa kutumia kamba.”
Kwa mujibu wa Brassio, polisi wamemueleza kuwa mwili wa kaka yake huyo waliukuta kwenye kichaka ukiwa unaning’inia, huku shingo ikiwa imefungwa kamba.
Mhandishi Lwajabe alitoweka ofisini kwake, Alhamisi ya tarehe 25 Julai mwaka huu, baada ya kuwaaga wafanyakazi wenzake, kwamba anatakiwa kuripoti kituo cha Polisi cha Mburahati, kwa ajili ya mahojiano juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
MwanaHALISI ONLINE halijaweza kufahamu, Mhandisi Lwajabe alikuwa anakabiliwa na tuhuma gani.
Mhandisi Lwajabe, kwa muda mrefu amekuwa mfanyakazi katika wizara ya fedha na mipango, akisimamia Idara ya fedha za Nje, kitengo cha mfuko wa maendeleo wa umoja wa Ulaya (EU).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mugisha Bagoka Brassio, ni kwamba kaka yake huyo alianza kupata misukosuko siku 10 zilizopita, baada ya kuhojiwa na polisi kwa masuala ambayo hakuyataja.
Anasema, “Jumanne ya tarehe 16 Julai 2019, majira ya saa tatu asubuhi, Mhandisi Lwajabe aliaga ofisini kwake, kwamba anakwenda kuonana na mtu aliyempigia simu. Hakurejea tena ofisini kwake.”
Anasema, kwa sababu ndugu yao hakurejea nyumbani, familia iliamua kutoa taarifa kesho yake, tarehe 17 Julai 2019 katika Kituo cha Polisi cha Kati, jijini Dar es Salaam na walifanikiwa kufungua jarada la uchunguzi lenye Na. CD/RB/4122/2019.
Mwanandugu huyo anasema, jeshi la polisi liliwambia kuwa watulie na Polisi watafanya jitihada za kumtafuta na ikiwa hajarejea nyumbani baada ya saa 72, warudi tena kuripoti kituoni hapo.
Badala yake, Brassio anasema, “siku iliyofuata, watu wasiojulikana walimrudisha Lwajabe kwa gari na kumshusha nyumbani kwake, alfajiri ya Ijumaa, tarehe 18 Julai 2019.”
Taarifa zinasema, Mhandisi Lwajabe alinukuliwa akiwambia wanafamilia yake – kabla ya kufikwa na mauti – kwamba ameelekezwa na watu waliokuwa naye kuripoti kwenye kituo cha Polisi cha Mburahati kwa mahojiano zaidi.
“Tumefanya jitihada mbalimbali kumtafuta mpendwa wetu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi Kituo cha Kati (Central Police Station), lakini hakuna tulichoambulia,” ameeleza Brassio.
Mhandisi Lwajabe anaingia katika orodha ya watu wanaodaiwa kutekwa na baadaye kupotezwa nchini na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.”
Mhandisi Leopold Kweyamba Lwajabe, amezaliwa katika kijiji cha Ihembe, kata ya Ihembe, wilayani Karagwe, mkoani Kagera. Ameacha mke na mtoto mmoja anayefahamika kwa jina la Doreen Leopald Lwajabe.