Licha ya fursa inayotokana na teknolojia ya Akili Bandia watu wengi wanaichukulia kama tishio kwa ajira zao

Licha ya fursa inayotokana na teknolojia ya Akili Bandia watu wengi wanaichukulia kama tishio kwa ajira zao

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
1719448826770.png


Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo inavyoonekana kwamba matumizi ya teknolojia ya Akili Bandia (AI) yanashika kasi sana duniani. Maendeleo haya ya haraka yameanza kubadilisha sekta nzima ya teknolojia na kuonesha uwezo wa kugusa nyanja nyingi za maisha ya kisasa. Kwa sasa inaonekana teknolojia ya Akili Bandia imevuka hata uwezo wa utendaji kazi wa binadamu kwenye majukumu kadhaa na inafanikiwa kuwasaidia wafanyakazi kuwa na tija zaidi na kuzalisha kazi yenye ubora zaidi.

Suala hili la teknolojia ya Akili Bandia kuchukua ajira za watu limeanza kutia hofu na kupelekea kuibuka kwa mijadala mikubwa miongoni mwa watu hawa. Kuna watu wengi wanahofia kwamba teknolojia ya Akili Bandia itasababisha watu wengi kupoteza ajira zao. Swala hili limeongelewa na watu wengi sana lakini pamoja na yote, teknolojia ya Akili Bandia inaonekana kwamba kamwe haiwezi kuondolewa duniani kwa sasa.

Teknolojia hii inaendelea kuboreshwa kila siku na inaingizwa kwenye pande mbali mbali za maisha ya binadamu. Kwa mujibu wa uchambuzi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), teknolojia ya Akili Bandia inatarajiwa kuathiri karibu 40% ya kazi za watu mbalimbali. Mkurugenzi mkuu wa IMF Kristalina Georgieva anasema katika hali nyingi, teknolojia ya Akili Bandia itazidisha ukosefu wa usawa kwa ujumla, hivyo amewataka watunga sera kushughulikia “mwenendo unaosumbua” ili kuzuia teknolojia hii isije kuchochea zaidi mivutano ya kijamii.

Ni kweli, kwa sasa teknolojia ya Akili Bandia inaonekana kama tishio kwa idadi kubwa ya ajira za watu, kwasababu ikilinganishwa na binadamu, teknolojia hii itakuwa na uwezo wa kufanya kazi muhimu ambazo kwa sasa zinatekelezwa na haohao binadamu. Hii inaweza kupunguza mahitaji ya wafanyakazi, kuathiri mishahara na hata kumaliza kazi za binadamu.

Hata hivyo tunatakiwa kujua kuwa shilingi ina pande mbili, licha ya hofu inayotawala watu, ikumbukwe kuwa teknolojia ya Akili Bandia inaleta manufaa makubwa sana hasa katika zama hizi za kisasa ambazo tunajitahidi sana kwenda na wakati.

Tukichukulia mfano wa nchi ya China, licha ya kwamba ina idadi kubwa ya watu, na kuhitaji kutoa nafasi nyingi za ajira, lakini ujio wa teknolojia ya Akili Bandia umewafanya vijana wengi kujipatia ajira hasa wale wanaosomea masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA. Licha ya hayo teknolojia hii sasa imetoa urahisi kwa kupunguza misongamano ya watu katika maeneo ya benki hasa watu wanaotaka kufanya shughuli za kibenki ikiwemo kutoa na kuweka pesa benki.

Pia kwenye masuala ya usafiri umepatikana unafuu mkubwa, ambapo sasa nauli ya kusafiria kwenda popote pale unanunua tu kwenye simu huna haja ya kwenda kwenye vituo husika. Kwenye masuala ya manunuzi, kwa sasa imekuwa rahisi zaidi. Watu wananunua kitu chochote mahali popote kwa kubonyeza kwenye simu zao tu, bila ya kuchoma nauli ama kupoteza muda wa kwenda madukani.

Viwanda ambavyo ndio eneo linalotia watu wasiwasi zaidi wa kupoteza ajira zao, saa kiwango cha uzalishaji kimezidi na kuongeza mapato ya kampuni kutokana na uwepo wa teknolojia ya akili bandia. Badala ya wafanyakazi kufanya kazi ngumu na nzito, wamepata msaada mkubwa wa mashine na roboti katika viwanda mbalimbali. Haya yote ni manufaa ya teknolojia ya Akili Bandia.

Ukizunguka baadhi ya maeneo hapa nchini China unaweza kushuhudia magari yanayojiendesha yenyewe, na hivi karibuni hata yameanza majaribio ya teksi zinazoruka juu ili kuepuka msongamano barabarani. Kwa hiyo licha ya watu kuwa na hofu na teknolojia ya Akili Bandia, wanatakiwa kuchangamkia fursa za kuhakikisha kwamba wanaingia katika soko la ajira za teknolojia ya Akili Bandia.

Wakati huohuo kwa nchi zenye mapato ya chini, kwa sasa naona wakati haujafika bado wa kuanza kulalamika ama hata kuwa na wasiwasi, kwasababu nyingi ya nchi hizi hazina miundombinu au nguvu kazi yenye ujuzi wa kutumia teknolojia ya Akili Bandia, jambo ambalo naona linaweza kuongeza hatari ya kwamba, baada ya muda fulani teknolojia ya Akili Bandia itazidisha pengo la ukosefu wa usawa kati ya mataifa mbalimbali duniani.
 
Back
Top Bottom