Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, amesema chama chake hakitashiriki Uchaguzi Mkuu ujao bila kufanyika mabadiliko sita muhimu ya mfumo wa uchaguzi, akisisitiza kauli yao ya
“No Reforms, No Election” akiwa katika Operesheni ya Kanda ya Kusini wilayani Namtumbo, Ruvuma.
Mambo hayo sita ni:
- Kuzuia wagombea kupita bila kupingwa.
- Kukomesha taratibu za kuwaengua wagombea kiholela.
- Kuzuia kuandikishwa kwa watoto kwenye daftari la wapigakura.
- Kukomesha vurugu dhidi ya kampeni za upinzani.
- Kuwapa uhuru mawakala wa vyama na kuhakikisha ushiriki wao.
- Kuepusha uchaguzi unaosababisha vifo na madhara kwa watu.
Lissu amesema mfumo wa sasa unaipendelea CCM na hauwaruhusu wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka. Ametoa mfano wa chaguzi za 2019 na 2020, akidai wagombea wa upinzani walienguliwa bila sababu. Pia amelaani wizi wa kura, akisema matokeo yake ni kupata viongozi wasiokuwa chaguo la wananchi.
Amesisitiza kuwa Chadema haiwezi kushiriki uchaguzi usio wa haki na huru, akisema:
“Hatuwezi kwenda machinjioni.”
---
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akiwa Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma amesema ili Chama hicho kishiriki uchaguzi Mkuu ujao, yapo mambo sita muhimu ya kufanyiwa kazi.
Akiendelea na Operesheni yake ya ‘No Reforms, No Election’ inayoendelea Kanda ya Kusini Lissu amesema;
“Katika mapendekezo yetu kulikuwa na mambo sita, hatukuyaanzisha sisi, isipokuwa tumeyapigania kutoka katika Tume ya Jaji Nyalali ambayo ilisema tubadilishe mfumo wetu wa uchaguzi kwa sababu uliopo unapendelea upande mmoja. Lakini imepita miaka 30 bado tunaimba wimbo uleule.
“Tunahitaji kubadilisha mfumo wa uchaguzi kusiwe na mgombea anayepita bila kupingwa, pili hatutaki taratibu za uchaguzi zinazoruhusu wagombea wengine kuenguliwa, tatu hatutaki kuandikishwa watoto wadogo kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
“Nne hatutaki kufanyiwa fujo tena kwenye kampeni zetu tunazofanya, tano mawakala wa vyama vyote wawe huru kufanya shughuli zao, ikiwemo kujua kura zao na kama hakuna mawakala uchaguzi usifanyike, sita hatutaki kuona uchaguzi unaotoa kafara za watu ili wapate uongozi,” amesema Lissu.
Mwanasheria huyo amesisitiza bila utaratibu wa uchaguzi kubadilishwa wananchi hawawezi kupata viongozi sahihi watakaowajibika, kuwatetea na kuwasemea changamoto zinazowasibu.
Amesema chaguzi nyingi zinazofanyika zinawanyima wananchi fursa ya kuchagua viongozi, akitolea mfano ule wa serikali za mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 zilizokipendelea chama tawala na wale wanaotoka vyama vya upinzani wakienguliwa bila sababu za msingi.
Amesema kwa kutambua hilo, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 vyama vya upinzani havijakaa kimya, vimekuwa vikipigania mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi lakini hadi sasa havijafanikiwa.
Mbali na mambo hayo, Lissu amezungumzia “wizi wa kura unaofanyika kwenye vituo vya kupigia kura”, kuwa pia ni sababu ya kupatikana viongozi ambao si chaguo la wananchi.
“Haiwezekani tena na chaguzi za namna hii, wanaosema twende tu hatuwezi kwenda machinjioni, wanaenda kukata wagombea wetu, mnasema twende tu, hatuwezi kukubali,” amesema.