Kambota nakushukuru, kwani umevua gamba,
Kumbuka umekufuru, matapishi utaramba,
Siku kweli ikizuru, utajiona mshamba,
Shairi lako la hovyo, kwani wasifu fisadi.
Kwa wachumiao tumbo, Lowassa mtu shujaa,
Wafikirio kwa matumbo, Lowassa tiba ya njaa,
Watapigana vikumbo, kwenda kwake ganga njaa,
Shairi lako la hovyo, kwani wasifu fisadi.
Hebu rudi darasani, jifunze misamiati,
Udhaifu tabaini, uijue tofauti,
Kamanda na marhuni, vina kubwa tofauti,
Shairi lako la hovyo, wamsifia fisadi.
Kama Lowassa Kamanda, basi ni wa mafisadi,
Kwa hili sitamponda, kulhali ni fisadi,
Kwake nilichokipenda, kukubali yu fisadi,
Kamueleza Kikwete, kuwa sote mafisadi.
Kambota nakushangaa, sijaona kicho chako,
Tafuta dawa ya njaa, si kuvua nguo zako,
Kesho kaka ni balaa, mafisadi si wenzako,
watakutumia sana, utatupwa ja nepi.
Kambota umenikuna, kufichua sura yako,
Ila la maana huna, kwa huo mradi wako,
Wamtumikia ngwena, kitoweo mwisho wako,
Uliza waliowini, kihalali si jinai.
Uchangu kimaadili, umegeuka mradi,
Wachovu waona dili, kutumiwa na fisadi,
Watupia senti mbili, kusafisha mafisadi,
Mwisho wa siku walia, warambapo matapishi.
Kaditamati kituo, mbele sitaendelea,
Onyo wapiga chapuo, fisadi kunyenyekea,
Ipo siku mlo huo, puani utatokea,
Kambota u mmojawapo,wapi utaficha sura?