Tanzania ni miongoni mwa-mataifa yenye elimu duni barani Afrika na hata duniani. Na hili swala si geni kwa viongozi wa Tanzania katika serikali za awamu zote tano. Na kama ni geni, tunaweza wauliza kwa nini viongozi walio-wengi watoto wao husoma nje ya nchi? Wanatambua fikra kuwa nchini mifumo ya elimu na taasisi zake ni duni mpaka miundo mbinu ya taasisi zake nazo ni duni. Sasa katika serikali zote tano zimechukua hatua gani? Jibu ni hamna hatua stahiki iliyochukuliwa ya kuboresha ubora elimu yetu nchini, sana sana ni kujenga shule na kusimika sera duni za elimu.
Lazima tutambue umuhimu wa elimu bora katika dunia ya sasa ya karne ya 21. Pia lazima tutambue ili taifa lolote liendelee kiuchumi, kisiasa, kiteknoljia na kisayansi, kifikra na kimatazamo inategemea wananchi wake wameandaliwa katika mifumo ya elimu gani au ubora wa elimu ya aina gani. Kuna wakufunzi nchini hatuna na hawapo kabisa, hili ni zao la mifumo ya elimu yetu nchini au aina ya elimu yetu na wakufunzi tulionao ni certificate qualified na sio competent na sio practical qualified. Pia tuna wakufunzi wengi wana vyeti vya taaluma lakini utendaji wao haufanani na taaluma zao hili nalo ni zao la mifumo ya elimu yetu nchini au aina ya elimu yetu. Na taifa lolote linaloshindwa kuzalisha wasomi au wakufunzi wake ambao ni taifa la kesho, taifa hilo kuendelea ni kazi n ani ngumu. Ni swala lisilohitaji mtu mwenye upeo mkubwa au mtu mwenye uwezo mkubwa kuchanganua mambo kiundani, elimu ni moja wa nyenzo ya kuandaa taifa la Kesho haoipingiki hilo.
Kupitia elimu tunaweza kuandaa viongozi wa taifa la Kesho wataoweza kubadilisha mifumo ya serikali na mifumo ya utawala na kuongoza taifa hili.
Kupitia elimu tunaweza kuandaa watanzania wenye uelewa juu ya mambo yao kitaifa, ndio hao hao watakaopata uamko wa kubadili katiba ya nchi yetu.
Kupitia elimu tunaweza kuandaa wanauchumi wataoweza kutunga sera na kutafuta nyenzo nyingine za vyanzo vya mapato nchini na sio kutegemea misaada au kodi au mikopo kama ilivyo sasa.
Na pia kupitia elimu tunaweza kuandaa wakufunzi au wataalamu mbali mbali wa tasnia za taaluma mbali mbali wanaohitajika kwenye sekta mbali mbali nchini.
Elimu bora lazima ndio kiwe kipaumbele namba moja katika serikali za kila awamu, na katika kila bajeti ya mwaka kila serikali hasa katika dhama za kuelekea kwenye uchumi wa viwanda au uchumi wa kati. Sasa elimu bora tunaipataje au malengo ya elimu bora tunayafikiaje? Ni lazima tukubali kubadili mifumo ya elimu yetu, mitahara ya elimu yetu, tuboreshe miundo mbinu katika taasisi za elimu yetu, sera za elimu na pia tuboreshe vipaumbele kwa walimu wetu. Haya yote hatuwezi pekeetu kuyafanikisha lazima tukubali kushirikiana na mataifa yaliyoendelea. Sio tu watupatie au tuige sera zao za elimu au mitahara yao au mifumo yao ya elimu bali watupatie fedha aidha kwa kukopa, maana bila fedha haya mambo yote hayawezi tekelezwa.
Haya yafuatao yakitekelezwa au kufanyiwa kazi tunaweza kupata elimu bora na kufikia malengo yake.
- Serikali kusomesha watanzania nje ya nchi, ni jambo jema lakini hili jambo lazima litendeke kwa mipango maalumu. Jambo hili limeanza tekelezwa toka serikali awamu ya kwanza mpaka sasa, lakini matunda yake kwa taifa letu ni madogo sana kiasilimia kulinganisha miaka zaidi ya 50 toka jambo hili lianze tekelezwa. Ni kheri tujenge vyuo nchini na kuajiri walimu toka nchi za magharibi watakaofundishia nchini na kuweza kuzalisha idadi ya wasomi wengi ndani ya mwaka.
Au ni kheri tuendelee kusomesha watanzania nchi za ughaibuni kwa kiwango kidogo na liwe swala la kila mwaka?
Kwa kuzingatia uchumi wa taifa lazima tujue kuchagua kipi ni bora kwa gharama ipi na kwa manufaa ya muda gani. Kwa uchumi wa taifa letu hatuwezi somesha watanzania wengi sawa na wale wataozalishwa endapo tutajenga vyuo nchini na kuajiri walimu na … toka ughaibuni. Pia kwa kusomesha watanzania nje ya nchi kuna wengine wanarejea ndani ya nchi napo kuna wengine hawataki kurejea kabisa nchini yote ni tokana na mifumo duni katika taifa letu.
Kwa fani zisizotolewa au hazipo kabisa nchini, ni kheri tuajiri wakufunzi au walimu toka nje ya nchi waje kufundisha nchini, kuliko kupeleka watanzania wakasome nje ya nchi kwa gharama kubwa ambapo hupelekea kupata wakufunzi wachache. Tukiajiri wakufunzi au walimu toka nje ya nchi waje kufundisha nchini tutaweza zalisha wakufunzi au wataalamu wengi ndani ya mwaka.
- Mitahara na mifumo ya elimu nchini. Mifumo ya elimu na mitahara yetu ni duni na dhaifu haiendani na mahitaji ya wasomi au wakufunzi wa karne ya 21 na kupitia mifumo hi duni tumekuwa tunapoteza muda mwingi shuleni, bado ukihitimu unatoka na mtazamo wa kuajiriwa yote haya ni mazao ya aina ya elimu ya nchi yetu.
Hakuna sababu ya mwanafunzi kusoma masomo 7 au 13 au 15, kwa ubongo gani tulionao watanzania? Kwa kuzingatia na malezi na mazingira ya kitanzania.
Hakuna sababu wahindi au wazungu wafungue taasisi zao za elimu na wasomi mitahara ya kwao, na sisi tukienda kwao tusome au tufuate mitahara yao ya elimu. Kama wanakiri mifumo yetu au mitahara yetu ni duni basi tukubali kushirikiana nao kuibadilisha.
Au wanafunzi wa sekondari wakifika kidato cha tatu hulazimika kuchagua masomo watakayo kama ni ya sayansi au Sanaa au biashara, mwanafunzi wa sayansi kidato cha tat una nne hulazimika kusoma masomo ya sayansi na Sanaa kwa wakati mmoja ambapo hufika masomo 9. Kwa nini asisome masomo yake husika tu? Ya sayansi tu.
Mitahara ya yetu au mifumo ya elimu yetu inapendekeza uwepo wa masomo mengi, huku mengine hayana tija wala umuhimu mfano mwananafunzi wa degree au diploma ya civil engineering anafundishwa programming language ya faida gani na umuhimu gani?
Kupitia mitahara au mifumo duni ya elimu yetu nchini tumekuwa tukitoa elimu ya nadharia kwa asilimia kubwa sana kulinganisha na elimu ya vitendo.
Hatuna teknolojia ya kwetu au tumeshindwa kuboresha teknolojia zetu tokana na udhaifu wa elimu yetu.
- Sera duni za elimu. Moja wa sera hizo ni sera ya elimu bure, hii sera haiboreshi elimu wala kukuza elimu ila itaongeza wananchi wanaojua kusoma na kuandika tu. Tanzania ni taifa changa sana kiuchumi, haliwezi weza somesha kila mtanzania bure na pia liboreshe elimu kwa wakati mmoja. Ni kheri tupunguze karo shuleni kuliko kusema kila mwanafunzi nchini asome bure, kwa uchumi gani tulionao? Au kwa kutegemea kodi na misaada? Tupate mfano Marekani ni taifa lenye uchumi mkubwa duniani, lakini halitoi elimu bure. Leo serikali inatumia billioni ngapi kutekeleza sera hii? Ni sera inayoigharimu serikali na taifa kiujumla, ndipo hapa tujifunze kuchagua kipi kilicho bora na manufaa kwa taifa? Tuendelee kusomesha watanzania wengi bure ili tuzalisha watanzania wanaojua kusoma na kuandika au tusomeshe watanzania kwa gharama nafuu ili mabillioni yanayotumika kusomesha watanzania watakaojua kusoma na kuandika yatumike kwenye kuboresha mifumo na mitahara ya elimu na kuboresha miundo mbinu katika taasisi zetu za elimu, upi ni uamuzi sahihi hapo. Ni kheri ukawa na watanzania 100,000 (qualified na competent kwa elimu ya karne 21) au ukawa na watanzania 1,000,000 (wanaojua kusoma na kuandika na wamesoma elimu ya kitanzania ya sasa)? Leo kodi zinapandishwa ili sera kama hizi zitekelezwe, kodi sio rafiki kwa mfanyabiashara na tokana wa ukubwa huo wafanyabiashara walio wengi wanashindwa kujiendeleza au kuendeleza biashara zao au kujiwekeza zaidi wanaishia kupata hela ya kula, kuvaa na kusomesha familia zao na wengine wanashindwa.
- Tupate mfano taifa la Botswana serikali yake imeshusha kodi kwa asilimia kubwa kwa lengo la mbotswana hata awe kipato cha chini aweze kulipa kodi yake na apate faida kwenye biashara yake apate kujiwekeza Zaidi na Zaidi na sio nchini kwetu serikali inategemea kodi, misaada na mikopo kwa asilimia kubwa.
Gharama zikiwa nafuu mashuleni hadi vyuoni watanzania waliowengi wataweza somesha watoto wao na ili iwezakane serikali kuna mengi inabidi ifanye haya.
Moja,Serikali ipunguze kodi kwa asilimia kubwa sana, ili kila mtanzania awe mmachinga au mfanya biashara mdogo au wa kati apate faida kubwa ya kumfanya awekeze zaidi na zaidi, mtanzania huyu akiwekeza Zaidi ndipo ataweza pata fedha Zaidi za hata kumuwezesha kusomesha na kuendeleza familia na hata kutekeleza majukumu yake ya kifamilia na sio kama hivi serikali inataka somesha bure mtoto wa kila familia ya kila mtanzania ambalo si jukumu la serikali ni jukumu la mzazi, jukumu la serikali ni kuhakikisha kuna sera bora za elimu, mifumo bora ya elimu, mitahara bora ya elimu na miundo mbinu bora katika taasisi zake za elimu
.
Mbili sera za ajira ziwekwe sawa na kubadilishwa mfano huwezi sema umpatie kila tenda kubwa mchina, mchina nae humfuatilii anaajiri watanzania asilimia ngapi na wa aina gani, wakandarasi waliowengi wagheni wanaajiri wataalamu toka kwao hizi kazi za udereva au vibarua ndio huajiri watanzania. Bado maslahi ni duni, unategemea mtanzania huyo atakuwa na uwezo wa kumsomesha mtoto wake? Lazima aishabikie na aiunge mkono sera ya elimu bure.
Tunasomesha watanzania hata kama kwa elimu yetu duni lakini haimanishi ndio wasipewe vipaumbele kwenye ajira au tenda, hata kama hawana udhoefu haimanishi ndio tuwaache inakuwa haina maana ya kusomesha sasa. Na ataupataje udhoefu au ubora unaohitajika wakati mifumo ya nchi yake ni duni? Au atapataje udhoefu wakati hata wagheni wakipewa kazi au tenda hawaajiri wazawa na wala serikali kupitia wizara zake husika hazitaki kufuatilia? Mtanzania anakuwa mtumwa kwenye nchi yake au anakuwa kibarua hata kama hana elimu yake. Sawa kuna kazi au tenda mhandisi au mtaalamu wa kitanzania hawezi fanya tokana na udhoefu au teknolojia (ukosefu wa mitambo) au fedha lakini serikali imejipangaje au imewajibika kiasi au imemuwezesha mtanzania huyu kiasi gani?mfano Serikali katika awamu tofauti imejenga viwanja vya ndege kadha wa kadha vikiwemo Songwe airport, JK airport terminal 3 bado saa hivi inaenda kujenga Msalato (DODOMA) tenda zote wanapewa wakandarasi wagheni na bado miaka 5 mbele tutajenga vingine bado tutawapa wakandarasi wagheni, wakati ilifaa hata huu uwanja wa ndege wa Msalato (DODOMA) ndio uwe wa mwisho kupewa wagheni na ili ifanyike hivyo serikali ilibidi ichukue wahindisi wake hata 100 na wengine washiriki mwanzo mwisho kwenye ujenzi huo na ikitokea tenda nyingine wanapewa tenda hiyo. Tunajenga fly overs, madaraja makubwa nchini lakini serikali haichukulii kama fursa ya wahindisi wa kitanzania wajifunze na wapatie udhoefu ili hata mbeleni waweze kupewa wazawa. Serikali inangojea mtanzania aende, na mtanzania wa kawaida akienda ataambiwa hamna ajira lakini serikali ikitoa msaada haya mambo yanawezekana. Serikali ikishindwa tekeleza hivyo kufuatilia ndipo hapo wanasiasa wetu wanakuja na sera za elimu bure.
Tatu, Serikali itenge kiasi cha fedha kwenye kila mwaka wa bajeti cha kuwezesha vijana. Katika mwaka huu bajeti ulionza 2018/2019 serikali ingesema itenge trillioni moja na iwezeshe vijana 2000 wa kitanzania waliohitimu vyuo vikuu iwakopeshe kwa dhamana ya vyeti vyao (vyeti vya kuzaliwa, shule na vyuoni) na vitambulisho vyao mbali mbali na wawekwe nchini ya uangalizi mkali, ndani ya miaka 10 serikali itakuwa imewezesha vijana wa ngapi? Na vijana hao watakuwa wameajiri watanzania wangapi ndani ya miaka kumi? Tuchukulie katika vijana hao 2000, kila mmoja akaajiri watanzania 10. Pia serikali itakuwa imetanua wigo wa kukusanya kodi kwa ukubwa gani ndani ya miaka 10? Serikali inapo shindwa kutazama au kuamua maamuzi sahihi tokana na uchumi wetu ndio tunakuja kupata kundi la watanzania maskini kupelekea kusimika sera kama hii ya elimu bure isiokuwa na tija kwa taifa kiujumla sana sana kupata watanzania wanaojua kusoma na kuandika, wana manufaa gani kwa taifa?
Nne, Vigezo na namna ya utoaji wa mikopo ya vyuo vikuu. Hakuna sababu ya kumlazimisha mwanafunzi achague kati ya masomo ya sayansi au biashara au Sanaa, kwamba akichagua masomo ya sayansi au fani za sayansi atazingatiwa sana kwenye kupata mkopo. Kila fani au kila masomo yana umuhimu kwa taifa hili, ila aina ya elimu yetu ndio iliyopelekea kuzalisha aina fulani ya wanataaluma kwa wingi. Sidhani kama tungekuwa na mifumo ya elimu au mitahara ya elimu au miundo mbinu ya taasisi katika zetu ya kueleweka tungekuwa na upungufu wa wakufunzi au wanatalumu waliohitimu masomo ya sayansi. Test tube toka kidato cha kwanza mpaka cha nne unaishiaga kuichora tu kwenye daftari, unakuja kuiona kidato cha nne kwenye practical. Utavutiwa kweli kusoma masomo ya sayansi? Mwalimu anafundisha physics au chemistry au mathematics unaona anafundisha anababaika, anakuambia hii utameza kweli utathubutu kwenda kusoma huko? Watathubutu wachache na ndio matokeo yake tunakuja kuzalisha kundi hili kwa kiasi kidogo.
Kwa namna hii ya utoaji wa mikopo kwamba wazingatiwe sana wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi, itakuja fikia miaka ya mbeleni tutakuja kubadili vigezo kuwa wanafunzi wataokuwa wanaenda kusomea masomo ya biashara au Sanaa wazingatiwe sana. Tunakuwa hatutatui tatizo bali tunakuwa tunaamia upande wenye nafuu wa tatizo.
Tukipata au tukiona upungufu wa wanataaluma tuje chini huku wanakoazwa kuzalishwa tujue kuna tatizo gani, mfano tumeona tuna upungufu wa wanataaluma wa sayansi tu, tujiulize sababu? Je mazingira ni rafiki kwa mwanafunzi mwenye kutaka kusoma masomo haya? Kama hamna tunamsaidiaje huyu mwanafunzi? Tuchukue hatua gani au nini kifanyike?
Swala la kusema umzingatie mwanafunzi wa masomo ya sayansi tu, je vipi mwanafunzi anaetaka kusoma masomo ya biashara au Sanaa huenda ni yatima au ana mzazi mmoja au wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha ndio asisome kisa hakuchagua masomo ya sayansi au hakupenda au hawezi au hataki?
Masomo ya sayansi sio magumu bali mazingira ya kutolea au kupatia masomo hayo ndio magumu na si rafiki.
- Uongozi kwenye wizara ya elimu, sayansi na teknolojia. Mama Joyce Ndalichako amesoma elimu hii ya kitanzania tunayotaka ibadilisha, kweli utalijie mabadiliko makubwa katika mifumo au mitahara ya elimu yetu? Hata kama kasoma ughaibuni bado ana exposure ndogo sana, sana sana utasikia pass mark zimepanda. Hii wizara inahitaji new mind, ni kheri serikali iingie gharama iajiri wakufunzi toka nje wapewe wizara hii kuanzia waziri mpaka katibu wa wizara. Au tukishindwa basi serikali iunde bodi ndani ya wizara, hiyo bodi iwe na wakufunzi toka nje ya nchi wataokuwa wanamshauri Mama Joyce Ndalichako. Serikali ikishindwa fanya hivyo isitarajie mabadiliko makubwa ndani ya wizara hiyo, maana viongozi wote wamesoma elimu hii na kama wamesoma ughaibuni ni kwa muda mdogo sana yani tukishindwa hapo tusitarajie mabadiliko yoyote kielimu, kisayansi na kiteknolojia san asana tutarajie mabadiliko ya pass mark. Maana inakuwa ni kipofu ana muongoza kipofu mwenzie, kwa nini wasiishie wote shimoni?
- Maslahi ya walimu (Mashuleni hadi vyuoni) Tasnia ya ualimu nchini, ni moja wa tasnia zinazodhaurika sana nchini hata mimi mwenyewe siwezi mruhusu hata kumshauri mwanangu akasomee ualimu. Yote hayo ni tokana wanataaluma wa tasnia hii hawajaandaliwa mazingira stahiki kuanzia kwenye maeneo yao ya kazi mpaka maslahi yao. Ila kiuhalisia ni kundi linaloandaa taifa la Kesho na ndio lilotuandaa hadi sisi, lakini halithaminiki, kupuziwa na kusahaulika kwa kiasi kikubwa sana. Lakini tunajua athari za kulipuzia kundi hili? Serikali inabidi ilitazame na kulizingatia kwa umakini sana maana tusingekuwa na wakufunzi au wataalamu nchini mbali mbali bila walimu. Kundi hili linapaswa kupewa hamasa upya wapandishwe mishahara kila baada ya muda fulani, mazingira ya kazi yaboleshwe na sera nzuri zisimikwe kwa ajili ya kundi hili.
- Lugha ya Kufundishia. Kabla ya yoyote tujiulize maswali yafuatayo, tuna lugha ngapi za taifa nchini? Kama ni mmoja na ni Kiswahili, kwa nini kiingereza kitumike kwenye shughuli au nyaraka za serikali au makampuni binafsi au taasisi binafsi? Au kwa nini kiiengereza kinatumika katika sehemu mbali mbali katika jamii zetu? Mfano matangazo n.k. Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), wizara na mamlaka husika zimeshindwa kutatu mkanganyiko huu? Na je kwa vitendo hivyo tunakuza lugha hii changa au tunaididimiza?
Ukosefu wa lugha maalumu ya kufundishia nchini nao umekuwa ukichangangia kudidimiza elimu yetu, katika shule za kata ngazi ya shule za msingi Kiswahili ndio lugha ya kufundishia na kiingereza linakuwa ni somo la kawaida, ukienda sekondari kiingereza ndio lugha ya kufundishia na Kiswahili likiwa kama somo la kawaida. Mpaka hapo ni mkanganyiko alichojifunza shule ya msingi inabidi akibadilishe kwenye kiingereza ndio aelewe, ukija kwenye jamii zinazomnguka mwanafunzi huyo ni Kiswahili kinatumika na kuzungumzwa maanake kiingereza ni lugha ya darasani (mpaka mwalimu akiwa anafundisha), vitabuni na notes kasoro somo la Kiswahili tu.
Ni kheri tuchague lugha moja itumike toka shule za awali mpaka vyuo vikuu, kama kiingereza au Kiswahili, tena tujue tuweke wazi lugha ya taifa ni Kiswahili au kiingereza tujue moja tu.
Kiswahili kinaweza tumika kama lugha ya kufundishia toka shule za awali mpaka vyuo vikuu ila ni swala lenye kuhitaji muda na litalochukua miaka kadhaa na mchakato huo ni wa uanzie darasa la awali, pia haya yakitekelezwa tutafikia malengo,
Moja, Uundaji wa maneno ya Kiswahili na ugumu wa maneno. Ni kweli Kiswahili ni lugha change na ina upungufu wa maneno mengi, hili tatizo tunalitatuaji? Lazima tukubali tukope maneno mengi kutoka lugha za kigheni kama ilivyo lugha ya kiingereza hatuna sababu ya kutunga misimiati migumu ili tupate maneno hayo. Calculator sio mpaka iitwe kikotozi, tulichukue neon kama lilivyo tubadilishe uandishi tu, hamna sababu ya kuunda misamiati migumu.
Mbili, Matumizi ya Kiswahili, Mamlaka husika zikazie matumizi ya Kiswahili kwanzia ngazi ya serikali (nyaraka, shughuli za kiserikali), vyombo vya habari hadi jamii zetu tunazoishi kila siku, hii itasaidia mjengea mwanafunzi mazoea ya misamiati ya Kiswahili inayohesabika kuwa migumu hata ile miepesi pia kunakuwa hamna haja ya yeye kuanza kutafsiri kupelekea atafsiri kwenda Kiswahili ndio aelewe.
- Tunaweza tukawa tunasema Kiswahili ni kigumu, kumbe taasisi husika, mamlaka husika, wizara husika na serikali kwa ujumla haiwajibiki katika kuraihisha lugha hii au kuikuza lugha hii.
- Tanzania ya serikali awamu ya tano ni mfano wa gari jipya lakini lina engine ya zamani, upya wa gari hili hauendani na engine yake. Maanake tupo kwenye mwelekeo mpya wa uchumi wetu, mwelekeo wa kuelekea kwenye uchumi wa viwanda au kati lakini bado tupo kwenye bora elimu na sio elimu bora, na elimu bora ndio engine ya kufikia malengo yetu.
HITIMISHO
Hata tujenge viwanda 1,000,000 bila elimu bora ni sawa tunacheza tu, tutakuwa hatuna wananchi wenye uelewa wa kuvikuza ama kuviendeleza viwanda hivyo au la sivyo watanzania wataishia kuwa vibarua tokana na uduni wa elimu yao. Pia watanzania hawa watashindwa kufungua viwanda vyao, viwanda vitajengwa kwa wingi na wazungu na ndio watakuwa wameshikiria uchumi wa nchi hii na ndio watakuwa na sauti, tunakuwa tunadumisha ukoloni mambo leo.
Serikali na wizara kwa ujumla inapaswa kutambua kuwa wananchi walio-andaliwa kwenye mifumo ya elimu bora ndio msingi wa taifa lolote duniani kuendelea kiuchumi, kisiasa, kielimu, kisayansi na kiteknolojia, hata ijengwe miundo mbinu ya kisasa kiasi gani haiwezi kuwa chachu kubwa kwenye kuendeleza taifa letu.
Swala hili sio jukumu la Chama cha Mapinduzi (CCM) au serikali ya chama tawala au vyama pinzani, ni jukumu la kila mtanzania bila kujali itkadi yake ya aina yoyote, na taifa hili haliwezi jengwa na chama tawala pekee yake lazima tuungane kama taifa moja, lazima serikali ya chama tawala ikubali kuwakusanya watanzania wa kila itkadi. Haya maneno matatu (AMANI, UMOJA NA UPENDO) kwenye nembo ya taifa sio maneno ya kubezwa, lazima tuyatekeleze na waasisi wetu hawa kuyasimika kama mapambo tu ya nembo. Lazima tupendane bila kujali itkadi ya mtu, ndipo tutaweza kupata umoja uliyo imara na ndipo taifa letu litakuwa na amani na sio utulivu tulionao sasa tukidai tuna-amani.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Nakala hii imeandaliwa na,
Jina: Wilson Masika Kaiser,
Tovuti: Wilsonkaisery@gmail.com,
31/07/2018.