Dingswayo
JF-Expert Member
- May 26, 2009
- 4,019
- 2,925
Dodoma/Dar. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi ameanza kampeni kanisani kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.
Alisema hayo jana katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Katika hotuba yake, Lukuvi aliwaeleza waumini waliofurika katika ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu wa kanisa hilo katika jimbo kuwa waendelee kuliombea Bunge lifanye uamuzi sahihi wa serikali mbili.
Aliwataka Watanzania kuipuuza Rasimu ya Katiba katika suala la Muungano na Serikali tatu kwa madai kuwa kutaka kuwapo mfumo huo ni kutaka Watanzania waingie vitani.
"Serikali tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi kuwa na amani tena, angalieni nchi ya Korea Kusini na Korea Kaskazini ambao waligawanyika na sasa ni maadui wakubwa wanaokaa mipakani wamenyoosheana bunduki," alisema na kuongeza:
"Waumini ndugu zangu wapendwa, kwa sasa tupo katika hali mbaya sana hapo bungeni, tunaomba mtuombee kuna watu ambao wanataka madaraka kwa nguvu na wameanza kutafuta jinsi ya kuvunja Muungano na kudai kuwapo kwa Serikali tatu, nawaomba sana wapuuzeni wale wote ambao wanataka serikali tatu."
Alisema watu wa aina hiyo wanaonekana kuwa wana huruma na Watanzania na wanadai kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika wakati hiyo Tanganyika wanayoidai ni jina tu ambalo Wajerumani walikaa mezani wakabuni na kutuletea.
Lukuvi alisema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.
Alisema wanaopiga kelele wana ajenda za siri na nia yao kutaka kufanya fujo na kusababisha machafuko... "Kwani ukiwa na mke mmoja akakushinda unafikiri utatuzi ni kuoa mke mwingine?"
Baadaye alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lukuvi alisema alichokizungumza kanisani hapo ni mawazo yake binafsi ambayo yanafanana na Watanzania wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
"Unajua jeshi haliwezi kukaa na bunduki bila fedha. Hiyo Serikali ya tatu ambayo jeshi litakuwa chini yake haina vyanzo vya mapato vya kueleweka, sasa hao wanajeshi watalipwa nini? Wenye mitutu watakubali kuishi bila fedha?"
Alisema hata vyanzo vya mapato ambavyo vimeandikwa katika Rasimu ya Katiba ni lazima visimamiwe na pande mbili za Muungano, akiwa na maana ya Tanganyika na Zanzibar na kwamba kama upande mmoja ukishindwa kuchangia hali itakuwa mbaya.
"Kama tunataka serikali ya tatu ni lazima tuhakikishe kuwa inakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato. Jambo hili siyo ubishi wala ushindani ni suala la kujenga hoja na kujadili kwa kina, ni ngumu sana katika utekelezaji wake," alisema.
Rais Kikwete wakati akizindua Bunge la Katiba mjini Dodoma aligusia suala hilo ambalo Lukuvi alilieleza katika ibada hiyo.
Kwa upande wake, Askofu Bundala alisema kanisani hapo kwamba ili kudumisha Muungano ni vyema Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha Muungano.
Alisema angetamani kumshauri Rais alivunje Bunge la Katiba kutokana na Bunge hilo kukosa mwelekeo na kukosa adabu.
Alipotakiwa kufafanua baadaye kuhusu kauli ya Lukuvi, askofu huyo alisema kuwa Waziri huyo hakutakiwa kutoa kauli nyepesi kama ile ukizingatia yeye ni mtu aliyepo madarakani.
"Kauli ya Lukuvi ilikuwa nyepesi sana kuzungumzia kwamba nchi itaingia kwenye vita. Ilitakiwa aende mbele zaidi kama mtu mwenye madaraka kwa kufafanua zaidi," alisema.
"Mimi nataka serikali mbili kwa sababu tumeshazoea kusali chini ya miti tukiwa na amani na tukiwa na serikali tatu tutasali kwa mtutu. Kama umeshindwa kuwatunza wanawake wawili ulionao je, huyo wa tatu ambaye humjui tabia yake utamtunzaje?" alisema.
CHanzo:Mwananchi
Na Nuzulack Dausen, Mwanachi
Jumatano,Aprili16 2014
Kwa ufupi
"Rais Kikwete naye alikuwa mwanajeshi, sasa kuna ubaya gani kama mwanajeshi akitawala nchi. Kuna ubaya gani mwanajeshi mwenye akili akitawala nchi yetu. Mbona Komba (Kapteni John Komba), aliwahi kuwa mwanajeshi na sasa ni Mbunge wa Mbinga Magharibi. Jeshi ni la wananchi na hao wanajeshi wanaowasema wengine huwa tunakutana nao klabu za muziki."
Baadhi ya wasomi wasema Waziri Lukuvi hakustahili kutoa kauli hiyo katika eneo la ibada. Dar es Salaam. Siku chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi kudai kuwa iwapo mfumo wa serikali tatu utapita, jeshi litachukua nchi, wanazuoni wametafsiri kauli hiyo kuwa ni ya kuwajengea hofu wananchi.
Jumapili Lukuvi, akiwa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alikokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, alisema muundo huo utasababisha nchi kutawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano haitakuwa na fedha za kulipa mishahara wanajeshi.
Lakini mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mohammed Bakari amesema kauli hiyo ilitolewa katika jukwaa lisilo sahihi hususan kwa kiongozi kama Lukuvi.
"Kila kauli ina mahala pake. Haikutakiwa kwa mtu mwenye madaraka kama yule kuzungumzia mambo nyeti kama hayo kanisani," alisema Dk Bakari.
"Licha ya kwamba kauli yake si mpya ilishasemwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete, lakini ilibidi ayaseme hayo ndani ya vikao vyao na si kanisani."
Alisema pamoja na kwamba kiongozi huyo alitoa maoni yake binafsi, ilitakiwa aangalie kwanza kauli yake kabla ya kuitoa. "Unapokuwa na nafasi ya juu ya uongozi, uhuru wako wa kutoa maoni binafsi unapungua. Kwa hiyo kupitia nafasi hiyo itabidi uzingatie masuala ya kuzungumza ukiwa raia, pia kiongozi," alisema.
Mwanasheria Harold Sungusia alisema watu wanaodai serikali mbili wamepungukiwa na hoja na ndiyo maana wanaanzisha masuala mengine yasiyo na tija. "Nimepitia sheria zote nikagundua kuwa mtu anayetetea hoja ya serikali mbili anakosa hoja za msingi ukizingatia tayari muundo huo wa Muungano umedumu kwa miaka 50."
Hata hivyo, mhadhiri wa Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema Watanzania hawatakiwi kuacha kufuata hoja za msingi na kutishika na propaganda. "Hizo ni propaganda kwa sababu hakuna utafiti uliofanywa na kugundua kuwa serikali tatu zitaleta vurugu."
Mkazi wa Mbagala Mtongani, Isaiah Solomon alisema alichosema Lukuvi kinaweza kuwatisha raia hususan wale walio na uelewa mdogo juu ya masuala ya siasa.
"Si jambo jema kusemea mambo hayo kanisani. Pia alizungumzia kuhusu kugharimia jeshi, sifikiri kama ni wanajeshi pekee wanaoweza kuleta madhara iwapo fedha za kuwalipa zikiwa pungufu; wapo wafanyakazi wengine watakaoleta balaa," alisema Solomon.
Mwenyekiti wa chama cha UDP Mkoa wa Dar es Salaam, Joackim Mwakitinga alisema woga wa wanasiasa wanaotaka serikali mbili ndiyo unaofanya watoe kauli za kuogofya wananchi.
"Naona ni woga tu wa wanasiasa wanaotaka kuleta mambo ambayo hayapo katika hoja za muundo wa Muungano," alisema. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Joseph Mbilinyi alisema kauli hiyo inadhihirisha jinsi wanaopigia debe serikali mbili walivyo waongo.
Akichangia mjadala bungeni jana, Mbilinyi alisema: "Rais Kikwete naye alikuwa mwanajeshi, sasa kuna ubaya gani kama mwanajeshi akitawala nchi. Kuna ubaya gani mwanajeshi mwenye akili akitawala nchi yetu.
Mbona Komba (Kapteni John Komba), aliwahi kuwa mwanajeshi na sasa ni mbunge wa Mbinga Magharibi. Jeshi ni la wananchi na hao wanajeshi wanaowasema wengine huwa tunakutana nao klabu za muziki."
Chanzo Mwananchi