Mkuu kama kama Mikaeli alimshinda shetani kwanini hakumuua kabisa ili sisi tusipate tabu?
Sasa kwa nini Mungu asimuue shetani tukawa watu wema wote. Je shetani ana faida gani kwa Mungu?
Bila shaka kuna manufaa makubwa sana kufuatia hekima ya Mungu kumwacha Lusifa aendelee kuwa hai, licha ya uasi wake na kuwalaghai malaika wengine wamfuate.
Sisi kama wanadamu, bado hatujajua kila kitu husika. Lakini kitendo cha Lusifa kutupwa hapa duniani, ni wazi kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya uasi wake mbinguni na upinzani wake dhidi ya mamlaka ya Mungu.
Mungu anaudhihirishia ulimwengu wote wema, huruma, uvumilivu na upendo Wake mkuu kwa viumbe Wake; na pia kuhusiana na ukuu, haki na utakatifu Wake, kwa jinsi anavyoshughulikia suala la Shetani (na waasi wenzie).
Vilevile, Mungu anatuonesha hatari kubwa iliyoambatana na uamuzi Wake wa kutuumba kwa ^sura na mfano^ Wake.
Ni dhahiri kwamba Lusifa na malaika waasi, na wanadamu wadhambi, wameshindwa kutambua thamani ya tunu kuu ya uhuru wa utashi (free will).
Tunaweza kusema kwa hakika kwamba miongoni mwa amana zote adhimu na maridhawa ambazo Mungu angeweza kumpa mwanadamu, uhuru wa utashi ni mojawapo.
Ndicho hutufanya tuwe wanadamu kamili hasa, tukifikiri na kutenda kwa utashi wa nafsi zetu.
Tunu hii bora ilipotumika vibaya, dhambi ikaingia – kwanza mbinguni, na kisha duniani kwa viumbe wa Mungu wapya. Huzuni ilioje!
Kitendo cha Mungu kumwacha Shetani aendelee kuwa hai ni namna fulani ya kumpa nafasi atekeleze hoja za madai yake dhidi ya Mungu.
Ukisoma kuhusu mahojiano ya Mungu na Ayubu katika kitabu cha Ayubu, ni kana kwamba Shetani alidiriki kumpa Muumbaji wake changamoto, na Mungu kwa hekima Yake kuu, akaikubali.
Changamoto hiyo ndiyo jaribio kuu ambalo Ibilisi amekuwa akiifanyia kazi duniani kwa miaka 6,000 sasa.
Ni bayana kwamba hoja mahususi za Lusifa dhidi ya mamlaka ya Mungu zingeweza kujibika kikamilifu na mazima milele (completely and finally forever), kwa mujibu wa hekima kuu ya Mungu na silika Yake takatifu na yenye upendo, kwa kuwaruhusu viumbe Wake wenye utashi huru japo ^wachungulie^ ng’ambo ya pili kwa kuhabiri (experience) maisha nje ya Mungu.
Ingekuwa wengi hawajarukwa akili leo, wangetambua manufaa tele katika uvumilivu huu mkuu wa muda mrefu wa Mungu kwa Ibilisi na jeshi lake, licha ya taabu, maumivu, na mauti ambayo wameyachochea na kuyasababisha tangu ulimwengu kuumbwa.
Hatimaye, baada ya yote, sote tutatambua kwamba kweli Mungu ndiye mwenye mamlaka, kweli, hekima, heshima, haki na ukuu.
^Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo Yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi;
Ni za haki, na za kweli, njia Zako, Ee Mfalme wa mataifa.^ ~Ufunuo wa Yohana 15:3