SoC02 Mabadiliko ya kufanya katika mfumo wetu wa elimu ili uweze kuendana na dunia ya sasa

SoC02 Mabadiliko ya kufanya katika mfumo wetu wa elimu ili uweze kuendana na dunia ya sasa

Stories of Change - 2022 Competition

Lidafo

JF-Expert Member
Joined
Sep 26, 2019
Posts
889
Reaction score
1,789
Tangu Tanzania ipate Uhuru imepita miaka 60 miezi 7 na siku 30 Sasa. Ushawahi jiuliza mfumo wetu wa elimu wa Sasa ni mfumo gani? na je umepitia mabadiliko gani mpaka kufika hapa?

Wakati wa Mwalimu Nyerere tulikuwa na mfumo wa elimu ya kujitegemea, mfumo huu ulikuwa na lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anaweza kusoma na kuandika, Mfumo huu ulisaidia sana hasa ukizingatia ni kipindi ambacho Kama taifa tulihitaji kuwa na watu wa kuongoza na kuleta chachu katika ukuaji wa nchi.

Swala la msingi hapa ni je toka kipindi cha elimu ya kujitegemea mpaka Sasa tuna mfumo gani wa elimu ? na je mfumo uliopo unatufaa?

Ni wazi kuwa dunia Sasa imepitia mabadiliko mengi ya sayansi na teknolojia, uchumi, siasa na sera za kiutawala, Mambo haya ndiyo yanayopelekea kuanza kukagua mifumo yetu ya elimu kuona Kama bado inaweza kuendana na Kasi ya mabadiliko ya dunia.
Katika makala hii nitaeleza mambo ya kuondoa kabisa katika mfumo wetu wa elimu na mambo ya kuboresha.

MAMBO YA KUONDOA KABISA KATIKA MFUMO WETU WA ELIMU
Mambo ya kuondoa kabisa ni haya

Kufuta darasa la saba,

hapa ni lazima tufahamu kuwa kwa Tanzania unachukua miaka 23 mpaka 25 kwa mtu kuhitimu ngazi ya shahada ya kwanza ni muhimu kwa wizara ya elimu kuangalia jinsi ya kupunguza idadi ya madarasa ili kutoa fursa kwa mwanafunzi asome darasa la kwanza mpaka la sita tu, Hapa tutaokoa mwaka mmoja na mwanafunzi huyo atakuwa tayari kujiunga na kidato cha kwanza.

Kuondoa mafundisho yasiyo na faida katika mitaala.
Mafundisho yasiyo na faida katika mitaala ni mzigo kwa mwanafunzi mfano nakumbuka tulifundishwa shule ya msingi kuwa mwanadamu wa kwanza alitokana na nyani lakini pia sekondari kidato cha kwanza katika somo la historia tukafundishwa ujinga huo huo, Sasa hii ina maana gani? Embu serikali iangalie na tija ya kumfundisha Mtoto mambo hayo ambayo hayamjengi kiakili mtanzania.

Kuondoa kabisa ufundishwaji wa case study za nchi nyingine.
Katika mtaala wa somo la jeografia Kuna case study ambazo mwanafunzi wa sekondari anatakiwa kusoma, Mfano uvuvi japani, Ufugaji wa kondoo Argentina, n.k na unakuta kabisa mtihani unatoka wa kidato cha nne au cha sita katika somo la jeografia eti toa Sababu za ukuwaji wa kilimo cha mpunga Burma , hapa tunatoka nje ya dunia yetu. Tukumbuke mwanafunzi huyu yupo kwa ajili ya kuisadia Tanzania Kama ndivo kwanini asifundishwe kilimo cha mpunga mbeya na morogoro, uvuvi manyara ,Mwanza na kigoma , kilimo cha machungwa Tanga n.k Mambo haya yangemsaidia mwanafunzi kwanza kujua jeografia ya nchi yake pili fursa zilizopo katika nchi yake kwa kufanya hivi tutapata vijana imara wa kujenga Tanzania yetu.

MAMBO YA KUBORESHA KATIKA MFUMO WETU WA ELIMU
  • Kutumia walimu wenye uwezo mzuri wa kufundisha,
Hapa nieleweke vizuri, Sote tanafahamu changamoto ya walimu pamoja na kuwa Kuna idadi kubwa ya walimu wahitimu lakini bado changamoto ya upungufu wa walimu ni kubwa hasa masomo ya sayansi hili lisitupelekee kuajiri walimu wasio na vigezo ni vizuri tufahamu kuwa mwalimu ana nafasi kubwa katika ulezi na kumuandaa mwanafunzi aweje , Hapa serikali ingefanya mchujo wa hali ya juu kuhakikisha na kujiridhisha juu ya uwezo wa walimu wake vinginevo tutaendelea pata wahitimu wa ovyo ambao ni zao la walimu wa ovyo waliopewa idhini ya kufundisha kutoka katika serikali isiyo makini. Swala hili lizingatiwe hata katika upatikanaji wa walimu/wahadhiri wa vyuo vya Kati na vyuo vikuu.​
  • Kufundishwa baadhi ya Sheria katika somo la uraia.
Sheria imekuwa ni changamoto sana, Katika dunia ya sasa tuna hitaji angalau mhitimu wa kidato cha nne awe na uwezo wa kujua Sheria za nchi yake na ni vizuri kwa kuwa serikali imefanya somo hili kuwa la lazima kwa wanafunzi wote wa sayansi na sanaa.

Ni wakati sasa wa wizara ya elimu kuandaa mazingira ya kufundishwa kwa sheria za nchi yetu, Hapa nikimaanisha katiba ifundishwe kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita katika somo la General Study hii itasaidia mwanafunzi kuwa na uelewa wa masuala ya sheria na hivo kumuandaa kutoa maoni yake juu ya mabadiliko ya sheria na maboresho ya katiba , Kuliko kumpa haki mwananchi kutoa maoni yake hali ya kuwa katiba iliopo haifahamu .​
  • Kuweka mfumo wa fani mbadala kuanzia kidato Cha nne.
Shule zote za sekondari ziwe na walimu watakao fundisha fani mbadala Kama ufundi , ususi, ufumaji, na umeme hapa tutaweza kusaidia mengi kwanza, tutawajengea wanafunzi wa sekondari uelewa wa fani tofauti pili, Mwanafunzi huyu hata akifeli tayari ana mwanzo mzuri wa fani Kama za ujenzi na umeme kwa hili tutapunguza hata idadi ya vibaka mitaani.​
  • Maboresho katika tume ya vyuo vikuu
Kama Kuna sehemu inahitaji dawa basi ni hapa ni wazi kuwa vyuo vikuu vimekuwa vikitoa wahitimu walio chini ya kiwango, Tukumbuke kuwa tupo katika safari ya kuijenga nchi na hatupo katika mchezo wa karata, Vyuo vikuu Ni sehemu ambayo tunategemea Kupata wasomi na wajuzi wa fani mbalimbali ambao ni Lulu kwa taifa letu lakini leo hii vyuo vikuu vimekuwa Ni sehemu ya kuzalisha wahadhiri wenye roho mbaya na wapenda sifa , wanafunzi wanaojua zaidi kutumia simu janja kuangalia video za ngono na udaku, Lakini ukimwambia andaa Muhtasari wa mada yeyote ni shida.

Mhitimu wa chuo kikuu hawezi kutumia ofisi za kawaida kabisa Kama Excel, power point na words, Alafu tunatakaa kushindana na mataifa ya wenzetu, Tuanze kushindana na akili zetu kwanza tubadili mitazamo yetu.
chukua mfano nchi ina rasilimali za kutosha jumlisha tuna wasomi wa uchumi lakini bado maendeleo ni ya chini sana, Tuna wahandisi lakini hatuna viwanda, Hii ni dhahiri kuwa Kuna shida katika mfumo wetu wa elimu. Tume ya vyuo vikuu(TCU) ifuatilie kwa ukaribu mwenendo wa vyuo na elimu inayotolewa kuhakikisha inaandaa wataalamu kwelikweli.

Mwisho niseme kuwa Nchi inajengwa na mwananchi Kama Serikali haitachukua hatua madhubuti kuboresha mifumo yetu ya elimu tutaendelea kuwa na wasomi wasio na uzalendo kwa nchi yetu na tutakuwa watawaliwa wa fikra kila iitwapo leo. Karibuni kwa Maoni

Mwandishi: Shafii R. Bakari (Lidafo)
 
Upvote 0
Back
Top Bottom