Wakati ushirikiano baina ya China na Afrika ukiendelea kuwa wa karibu zaidi, mipango mbalimbali ya kutokomeza umasikini na kuleta maendeleo kati ya pande zote mbili imeingia katika hatua mpya. Ni kutokana na mtazamo huu ndio maana Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC lilianzishwa ili kujadili njia mpya katika mapambano ya pamoja ya kutokomeza umasikini.
Kila wanapokutana, washiriki wa pande zote mbili wanajaribu kueleza uzoefu wao na kuangalia njia gani mpya za kupambana na umasikini, halikadhalika China pia imekuwa ikitoa msaada wake wa hali na mali. Tunafahamu kuwa shilingi ina pande mbili, na ushirikiano hadi uitwe ushirikiano basi unahitaji upande zaidi ya mmoja. Kupitia FOCAC China imeonesha nia thabiti ya kuisaida Afrika kuondokana na umasikini kwa kuandaa mikakati kabambe kama ilivyofanikiwa kutokomeza umasikini uliokithiri nchini mwake. Kwa kuwa wahenga wanasema “Abebwaye hujikaza” Afrika nayo pia inapaswa kuja na mipango mikakati yake na kuhakikisha bara hilo nalo pia linaondokana na umasikini uliokithiri kwa kufuata nyayo za China. Swali la kujiuliza ni je nchi za Afrika hadi sasa zimekuja na mikakati gani, na kwa zile ambazo tayari zimeshajiwekea mikakati ya kutokomeza umasikini, je imeshaanza kufanyiwa kazi?
Lengo la kwanza la Umoja wa Mataifa katika ajenda ya Maendeleo Endelevu ni kutokomeza umasikini wa aina zote hadi kufikia 2030, kazi ambayo inaonekana kuwa ni kubwa na ngumu sana kwa nchi zinazoendelea hasa za Afrika. Hata Umoja wa Mataifa pia uliwahi kutabiri kwamba itakuwa ngumu sana kufikia malengo ya ajenda ya maendelo endelevu ya kuondoa umasikini hadi kufikia 2030, kwa kuwa janga la COVID-19 limeleta athari mbaya sana za kiuchumi duniani, hasa kwa nchi zinazoendelea. Hivyo ili kukabiliana na kuunganisha nguvu kwa pamoja katika mapambano haya, China siku zote imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kutokomeza umasikini na kuleta maendeleo katika Afrika.
Kuna nchi nyingi tu ambazo zinanufaika na mipango ya China ya kutokomeza umasikini katika Afrika, ikiwa ni pamoja na za Afrika mashariki ikiwemo Uganda. Hivi majuzi rais Yoweri Museveni wa Uganda alipokutana na ujumbe wa China Ikulu, alipongeza na kukaribisha mikakati mipya ya China barani Afrika na baadaye kutaja maeneo mawili muhimu ya Uganda ambayo ni kutokomeza umaskini na kuhamisha teknolojia. Rais Museveni alibainisha kuwa serikali yake sasa inajikita katika kuwaelekeza watu jinsi ya kutokomeza umaskini katika ngazi ya familia ili kupata mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Katika mkutano wa 8 wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano baina ya China na Afrika ulilofanyika huko Dakar, Senegal, mwezi Novemba mwaka jana, balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong, alimwambia rais Museveni kuwa serikali ya China sasa imehamisha mipango yake ya kuisaidia Afrika kutoka kwenye miuondo mbinu hadi kutokomeza umasikini. Kwenye mkutano huo wa mawaziri China ilitangaza mipango tisa ya kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika ikiwa ni pamoja na kusaidia huduma za afya na matibabu, kuondoa umasikini na kuleta mendeleo ya kilimo, kuhimiza biashara, kuhamasisha uwekezaji, uvumbuzi wa kidijitali, maendeleo ya kijani, kuzijengea uwezo nchi za Afrika, mawasiliano ya kiutamaduni na baina ya watu, pamoja na amani na usalama.
Uzoefu mkubwa wa China katika kutokomeza umasikini uliokithiri pia unaweza kuchukuliwa kama kigezo kikubwa cha kuondoa umasikini wakati Afrika inapopambana ili kutokomeza umasikini. Kenya ikiwa imedhamiria kupata mafanikio kama ilivyopata China, tayari imeanza kutuma maafisa wake waandamizi kuja China kujifunza namna nchi hii kubwa ilivyopata maendelo ya kiuchumi hasa kwenye upande wa mabadiliko ya kilimo, utengenezaji na maendeleo ya miundo mbinu.
China inajulikana kwa kuwa na nguvu kubwa kiteknolojia na kiuvumbuzi, hivyo nchi za Afrika zinaweza kufikia maendeleo haya kwa kuiga China ambayo ni mshirika mkubwa wa Afrika. Katika kipengele hiki, kipaumbele kikuu cha China kuisaidia Afrika kuondoa umasikini ni kuhamisha teknolojia. Ushirikiano wa kiteknolojia ni kipengele muhimu katika ushirikiano wa pande mbili, ambao ulijadiliwa na kupitishwa katika mkutano wa 5 wa FOCAC uliofanyika Beijing.
Alipokutana na Rais Museveni, Balozi Lizhong pia alisema China inatarajia kuwa na ushirikiano unaojikita zaidi katika miradi ya teknolojia ambayo itasaida maisha ya watu wa Uganda, ambapo rais Museveni amethibitisha kuwa tayari kuna baadhi ya makampuni ya Uganda kama vile ya utengezaji wa magari yameanza kushirikiana na wenzao wa China, hatua ambayo itakuwa umuhimu sana katika kuendeleza ushirikiano uliopo.